Tuesday, March 3, 2009

Kina Kitine na watukwazao Tanzania!

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2007 ilionyesha kuwa Tanzania ni nchi ya 14 kwa umasikini zaidi duniani (kuna umasikini na umasikini zaidi!). Nina hakika ripoti ya miaka ya karibuni itaonyesha picha mbaya zaidi ya hiyo.

Lakini hata kama wewe si muumini wa ripoti hizo za UN, utasema nini kuhusu ripoti nyingine ya hapa hapa nyumbani iliyoandaliwa na watawala wenyewe ambayo nayo kwa kiasi kikubwa inafanana na ripoti hiyo ya UN?

Nazungumzia ile ripoti iliyotokana na utafiti wa Ofisi ya Takwimu ambayo matokeo yake yalitangazwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, mwaka jana, Oktoba 3. Kwa mujibu wa Mkullo, utafiti huo – Household Budget Survey ulionyesha kuwa Watanzania masikini wameongezeka hadi kufikia milioni 12, na kwamba kipato cha Watanzania walio wengi kwa siku ni wastani wa Sh. 460 tu!

Kama hali ni hiyo, jiulize tena: Yawezekanaje nchi iliyobarikiwa na mwenyenzi Mungu kwa kupewa maliasili hizo kibao, raia wake walio wengi wawe na kipato cha siku cha wastani wa Sh. 460 tu? Sh. 460 ambazo wala hazitoshi kukupa mlo mmoja tu uliokamilika kwa siku!

Ukitafakari kwa kina maswali hayo, majibu yako hayatakuwa tofauti na yale yaliyosemwa wiki iliyopita na mtu aliyeongoza Usalama wa Taifa kwa miaka 30, Hassy Kitine; yaani kinachotuponza sisi Watanzania ni uongozi mbovu.

Hata kama integrity ya Kitine ilipungua kutokana na kashfa ile ya matibabu ya mkewe, lakini kwa mtazamo wangu, hajakosea sana anaposema kuwa uongozi wa nchi ni mbovu. Na wala yeye si wa kwanza kusema hivyo. Wamekuwepo wazito wengi tu kabla yake waliojenga ujasiri wa kueleza kusikitishwa kwao na namna mambo yanavyokwenda nchini. Watu kama Jaji Warioba, Cleopa Msuya, Rashid Kawawa, Joseph Butiku, Chediel Mgonja (marehemu) n.k.

Hebu jiulize: Kama hatuponzwi na uongozi mbovu, inakuaje tushikilie nafasi za mwanzo katika orodha ya nchi masikini duniani; ilhali tuna utajiri mkubwa mno wa maliasili ambazo Mungu ametuzawadia?

Ndugu zangu, nihitimishe tafakuri yangu kwa kusema kwamba mpaka hapo Watanzania tutakapozinduka usingizini na kuwang’oa madarakani viongozi wabovu kwa njia ya kura zetu, tutaendelea kuishi kwenye nyumba za udongo na majani; ilhali wenzetu mafisadi serikalini na kwenye asasi za umma wanaishi katika mahekalu ya Sh. milioni 800 au Sh. bilioni 3!

Watanzania masikini tutaendelea kula mlo mmoja dhaifu kwa siku wa Sh. 460; ilhali watawala huwapeleka wake na watoto zao kula dinner kwenye hoteli za kitalii nchini!

Kina Kitine na wengine kadhaa wanaosononeshwa na umasikini wa Watanzania vijijini, wamenena na kusema kwamba tatizo letu ni uongozi mbovu. Wakati tunasubiri wengine nao walonge; hebu natujiulize: Miaka nenda rudi tunashindwaje kutumia kura zetu kuwaondoa madarakani watawala wabovu na nafasi zao tukawachagua viongozi? Maana; hakika, tunahitaji viongozi na si watawala!

Tafakari!!!

1 comment:

Anonymous said...

ipo safari ndefu bado kuelekea maisha bora kwa watanzania umasikini unaondelea bado utadumu kwa muda mrefu kwani viongozi hawa hawataki kuachia madaraka na kuzidi kuendeleza unyonyaji wao, kweli kazi ipo...