Monday, October 15, 2012

Siku ya Nyerere: Uadilifu, uadilifu

Katika kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, Vijana nchini wametakiwa kuachana na woga, badala yake wajitokeze kwa wingi kushiriki kwenye michakato ya kugombea ama kuingiza viongozi madarakani wakiongozwa na hoja na utaratibu ili taifa lipate viongozi waadilifu watakaojali maslahi ya wananchi kama alivyofanya Mwalimu Nyerere.

Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na watoa mada Esther Wasira na Jerry Silaa ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ilala kwenye Kongamano la Kumbukumbu ya miaka 13 ya Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa).

Wasira alisema kwamba kuendekeza woga kunakofanywa na vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wote nchini ndiko kulikosababisha taifa kuingizwa kwenye mikataba ya kifisadi ambayo imeneemesha viongozi wasio waadilifu na familia zao kwa gharama ya taifa.

“Katika moja ya maandishi ya Mwalimu alitahadharisha vijana kuwa wasipoondoa woga kwenye akili zao, kuna siku watakuta viongozi wao wakimiliki mali nyingi bila ya kujua walikozitoa na mwisho wa siku wakakuta nchi ikimilikiwa na mtu binafsi,” alisema.

Wasira alisema siyo vema kwa vijana kukubali kuhadaika na hoja isiyo na mashiko kwamba harakati za kisiasa zinaweza kuhatarisha amani ya nchi kwa kuwa amani ya Tanzania ni urithi wa Watanzania wote ambayo imejengwa na wazee kwa lengo la kudumisha haki na usawa na kwamba pasipo vitu hivyo viwili, basi vijana wasiogope kuvigharimia.

Kwa upande wake, Silaa aliwakumbusha vijana kuutumia ujana wao katika kutimiza wajibu wa kuchangia maendeleo chanya katika siasa za nchi kwa kugombea nafasi za kisiasa ama za kuwaweka viongozi waadilifu madarakani, wakiwa bado na damu inayochemka kama alivyofanya Mwalimu Nyerere ambaye katika umri wa miaka 40 tayari alikuwa amefikia ngazi ya urais wa nchi.

“Tukubaliane kwamba harakati za kudai uhuru wa Tanganyika ndiyo harakati kubwa aliyoifanya Mwalimu, lakini pengine cha kujifunza katika harakati hii ni namna alivyodai uhuru kwa kuongozwa na utaratibu, hoja na akili ya juu,” alisema.

Silaa alisema kwamba Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuuleta uhuru bila ya kuwashawishi wananchi wake kuingia barabarani kwa kuandamana au kuwahamasisha wamwage damu, na kwa hali hiyo akawahimiza vijana wamwige Mwalimu kwa kuendesha harakati zao za kusaka uongozi, kuingiza viongozi ama kudai haki kwa kuongozwa na hoja.

Naye mmoja wa wachangia mada katika kongamano hilo, Njipay Saroni, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayesomea Shahada ya Takwimu, alisema kwamba tatizo lililotokea juzi Mbagala jijini Dar es Salaam ambalo lilisababisha makanisa kuharibiwa na mengine kuchomwa moto na wanaodhaniwa kuwa ni waumini wa dini ya Kiislamu linatokana na kupuuza misingi imara ya kuishi kindugu aliyoijenga Mwalimu Nyerere.

Saroni alisema kwamba Mwalimu alipiga vita ubaguzi wa kikabila na kidini na akafaulu kujenga umoja kwa watu wote na kwamba watu waliishi kwa kushirikiana, msingi ambao kwa sasa umeanza kuvunjwa taratibu na hali itakuwa ni mbaya kama Watanzania wasipoheshimu msingi alioujenga.

Mada iliyojadiliwa katika Kongamano hilo ilihusu ‘Jukumu walililonalo vijana katika kumuenzi Mwalimu Nyerere’ na iliongozwa na Dk. Kitila Mkumbo.

KATOLIKI OMBEENI VIONGOZI


Katika hatua nyingine, waumini wa Kanisa Katoliki nchini wameaswa kuwaombea viongozi wawe watumishi badala ya mabwana lengo likiwa ni kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Hayo yalisemwa jana na Padri Ambrose Kitui kutoka nchini Kenya, wakati akitoa mahubiri katika misa ya kwanza aliyoiendesha kwenye Parokia ya Kiwanja cha Ndege mjini Dodoma.

“Mwalimu hakuwa fisadi, hakuwa mroho wa mali, alikuwa mtu safi na hata sisi Wakenya tunamheshimu na kumthamini, alikuwa ni mtumishi badala ya kuwa bwana,” alisema Padri Kitui katika mahubiri yake.

Alisema Mwalimu Nyerere leo hii atakumbukwa kwa upendo, utumishi ambao hakujali kabila wala dini ya mtu.

Alisema ili kumuenzi wakati Watanzania wanaadhimisha miaka 13 tangu kifo chake, inawapasa kuwaombea viongozi ili wawe watumishi badala ya mabwana kama alivyokuwa yeye.

Alisema hata Biblia takatifu katika kitabu cha Marko 10: 17-30 unazungumzia juu ya Wakristo kuhakikisha wanapata utajiri wa roho kuliko ule wa mali.

Kwa upande wake, Paroko wa Kiwanja cha Ndege, Padri Luyembe Sosthenes, alisema kuwa Watanzania wanalo jukumu kubwa katika kuwezesha mchakato wa kumfanya Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu unafanikiwa mapema.
“Binafsi nasema mimi nampenda Mwalimu, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu, lakini tunalo jukumu kubwa la kuwa mashuhuda katika kuwezesha kutangazwa mtakatifu,” alisema.

NAPE: RUSHWA INATUSUMBUA


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekiri kuwa rushwa na kukosa uadilifu miongoni mwa viongozi wa chama hicho na Serikali bado ni changamoto.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Nnauye alisema tangu kifo cha Mwalimu Nyerere viongozi wengi wa kiserikali na wa Chama hicho wamekuwa wakiandamwa na tuhuma za rushwa pamoja na kukosa uadilifu na hata wengine kufikishwa katika mikono ya sheria.

Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Mary Geofrey, Gwanaka Alipipi, Dar na Sharon Sauwa, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

No comments: