Thursday, October 18, 2012

Dk Ulimboka: Mfanyakazi Ikulu Alihusika Kuniteka

HATIMAYE Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka ameamua kuvunja ukimya, baada ya kumtaja kinara wa tukio la kutekwa kwake na kisha kutupwa kwenye Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam usiku wa Julai 26, mwaka huu.

Dk Ulimboka amemtaja mtu huyo katika taarifa yake iliyosomwa jana jijini Dar es Salaam na wakili wake, Nyoronyo Kicheere. Maelezo katika taarifa ya Dk Ulimboka, yanadaiwa kushuhudiwa na wakili mwingine wa kujitegemea, Rugemeleza Nshala. Taarifa hiyo pia ilisema mtu aliyekuwa na Dk Ulimboka kabla ya kukamatwa kwake alitambulishwa kwao na kigogo ambaye hakumtaja jina, kwa makubaliano kuwa atakuwa anachukua madai ya madaktari dhidi ya Serikali.

“Nathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu na kuniita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa,” inaeleza taarifa hiyo na kuonyesha namba za simu za mtu huyo anayedaiwa ni mfanyakazi wa Ikulu.

“Ninamfahamu sana bwana (jina tunalihifadhi kwa sasa), kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile. Nakumbuka alitambulishwa kwetu na kigogo mmoja nikiwa pamoja na wawakilishi wengine wa madaktari,” alisema.
Katika taarifa hiyo iliyoainisha namba iliyokuwa inatumiwa na Dk Ulimboka kuwasiliana na mtu huyo, inaeleza pia kuwa mpaka sasa mtu huyo yupo hai na kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano kwa chombo huru ili kuhakikisha haki inatendeka.

Taarifa inaeleza pia kuwa kwa nyakati tofauti mtu huyo alikuwa akitumwa kwa Dk Ulimboka na mtu ambaye tamko hilo halikumtaja, lengo likiwa ni kuchukua nyaraka mbalimbali na vyeti vya kuthibitisha taaluma za masomo yake.

“Wale wote waliotuhumiwa na ninaowatuhumu kunitendea unyama huu wako huru na hakuna aliyeguswa. Je uhai na maisha yangu, yana thamani ndogo kama ya mnyama anayekwenda machinjioni? alihoji Dk Ulimboka katika taarifa hiyo na kuendelea:
“Je Serikali ya nchi yangu itakubali lini kuundwa kwa tume huru kuchunguza unyama huu na kuhakikisha kuwa haki inatendeka?”

Dk Ulimboka amesema katika taarifa hiyo kuwa: “Niko tayari kuhojiwa na kutoa ushirikiano wangu kwa vyombo huru na makini vya uchunguzi ambavyo vitaundwa ili kuweza kuubaini ukweli.”

Maelezo ya wakili wake
Akisoma taarifa hiyo jana, Kicheere alisema kwa sasa Dk Ulimboka yupo nje ya nchi kwa matibabu zaidi na aliandika tamko hilo mbele ya Wakili Nshala, ambaye pia ameweka saini na mhuri wake. Hata hivyo, tamko hilo ambalo Kicheere alilisoma mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, linaonyesha lilitolewa Oktoba 7, mwaka 2011, jambo ambalo Nshala akizungumza na gazeti hili alisema ni makosa ya uchapaji.
“Hilo tamko lilisomwa mbele yangu Oktoba 7, mwaka huu, hiyo ya kuandikwa mwaka 2011 ni makosa ya uchapaji tu.” alisema Nshala.

Naye Kicheere alisema, Dk Ulimboka yupo tayari kusema ukweli wote wa kilichomkuta endapo itaundwa tume huru ya kuchunguza tukio hilo. Alisema taarifa ambazo alizitoa na kurekodiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo mtandao ya kijamii, ni za kweli na alizotoa akiwa na akili na kumbukumbu nzuri.

Tamko hilo linaeleza kwamba, moja ya uthibitisho kuwa taarifa hizo alizozitoa kabla ya kufika kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (Moi), na zile alizozitoa akiwa hapo, ni kule kuweza kumwita na kumshawishi mtu aliyemsaidia kutoka Msitu wa Pande.

“Uthibitisho wa kumbukumbu nzuri niliyonayo, ni pale nilipokutana na Juma Mganza katika Msitu wa Mabwepande asubuhi ya siku ya tukio. Pamoja na maumivu makali niliokuwa nayo kutoka kila sehemu ya mwili wangu, niliweza kumshawishi Mganza kunifungua kamba za mikono nilizokuwa nimefungwa,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza;

“Pia kukumbuka namba ya simu ya rafiki yangu Dk Deogratias ambapo Mganza aliweza kuitumia kuwasiliana naye kumpa taarifa kuhusu tukio hilo. Ni kupitia taarifa hiyo ndipo suala la mimi kufikishwa Moi lilipofikiwa.”

Aliendelea: “Na kama niliweza kukumbuka namba ya rafiki yangu, mambo hayo yanatosha kuthibitisha kuwa ninachokisema ni ukweli na kuwa utimamu na kumbukumbu zangu ni sahihi”.
Usiku wa Julai 26, mwaka huu, Dk Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana na kupigwa vibaya ambapo Julai 27, alikutwa kwenye Msitu wa Pande uliopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Baada ya tukio hilo, alisafirishwa mpaka Moi ambapo baadaye alipelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz

No comments: