Na: Matern Kayera
MWENYEKITI
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hakuna
nchi duniani inayotengeneza katiba kwa kuchukua maoni ya kila mwananchi
kama wanavyodai baadhi ya watu na asasi za kiraia hapa nchini.
Warioba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na
waandishi wa habari kwenye ofisi za Tume hiyo.
Alisema
Tume yake inajitahidi kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kupata maoni
yenye mitazamo tofauti kwa nia ya kujenga mwafaka wa kitaifa.
Warioba
alisema hayo baada ya waandishi wa habari kutaka ufafanuzi kuhusiana na
taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Katiba hivi karibuni kuwa kuna hali ya
kusuasua katika mchakato unaoendelea wa ukusanyaji maoni kutokna na
Tume kuchukua maoni kwenye kata chache huku nyingi zikiachwa.
Alisema
Tanzania ni nchi kubwa na idadi ya watu ni wengi, hivyo kumfikia kila
mwananchi aliko kama baadhi ya watu wanavyosema, siyo kitu rahisi.
Alisema mpaka sasa Tume inaridhishwa na hamasa waliyonayo wananchi kwa
kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao katika mikutano inayoendelea
maeneo mbalimbali nchini.
“Jumla
ya mikutano 842 imefanyika ambapo jumla ya watu 517,427 walihudhuria.
Awamu ya kwanza zaidi ya watu 189,000 walihudhuria na awamu ya pili watu
327,000. Wananchi waliotoa maoni kwa maandishi ni 77,405; waliozungumza
ni 29,514.
Waliotoa
maoni kwa njia ya tovuti 3,577 kati yao 12 wanaishi ughaibuni, kwa njia
ya mtandao wa facebook 2,338, kwa njia ya barua 2,500 na kwa njia ya
magazeti tumepata maoni 670 hadi sasa,” alisema Jaji Warioba.
Warioba
alisema kwamba maoni yaliyotolewa na wananchi ni mengi na yana uzito
mkubwa kwani yamegusa maeneo mbalimbali kama vile utawala na maendeleo.
Alisema mwamko huu wa wananchi unaonyesha ni aina gani ya utawala
wanautaka katika Tanzania.
Alisema
makundi maalumu kama vile wanawake, walemavu na wafungwa pia wamepata
fursa ya kutoa maoni yao kwenye mikutano inayoendelea kwa maandishi au
kwa kuzungumza. Alisema ushiriki huu wa wananchi kwa makundi mbalimbali
utasaidia kupata katiba inayowakilisha wananchi wote.
Pia
alisema kuwa NGOs zina wajibu wa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi
ili washiriki kwa wingi katika kutoa maoni yao na siyo kutafuta upungufu
tu.
Warioba alisema kuwa Tume imepewa miezi 18 kukamilisha kazi ya kuandika
katiba Mpya, ila akafafanua kuwa muda unaweza kuongezwa kama kazi
haijakamilika.
Pia
aliviomba vyombo vya habari viendelee kuisaidia Tume kwa kuwahamasisha
wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao.
No comments:
Post a Comment