Na Magreth Kinabo- MAELEZO
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC), imelionya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuacha mtindo wa
kutumia fedha pasipo kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) katika
utekelezaji wa shughuli zake. Kamati hiyo ya Bunge inayosimamia hesabu
za mashirika ya Umma imelazimika kulionya shirika hilo baada ya kutumia
kiasi cha sh. bilioni 25 nje ya utaratibu wa PPRA.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa POAC, Kabwe Zitto wakati
kamati yake ilipokutana na baadhi ya viongozi wa NHC kuzungumzia
utendaji wa shirika hilo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Bunge jijini
Dar es Salaam.
Katika taarifa yake POAC ilibainisha kuwa NHC kwa mwaka wa fedha
2010/2011 mbali na kupanga kutumia sh. bilioni 31 katika shughuli zake,
sh. bilioni 25 zimebainika kutumika nje ya taratibu za PPRA kitendo
ambacho ni kinyume cha utaratibu kwa mashirika ya umma.
Akijitetea kufuatia tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Nyumba Tanzania, Nehemiah Mchechu alisema suala hilo limetokana na
kuwepo kwa miradi ya dharura iliyoangalia masuala ya kibiashara zaidi.
Hata hivyo amekiri kuwa eneo hilo ni moja ya changamoto wanayokabiliana
nayo, hivyo wameshaanza kuifanyia kazi wakishirikiana na PPRA.
Kamati hiyo pia imelitaka shirika hilo, kuwakilisha matumizi ya fedha
ya mwaka huu unaoishia Juni, 2012 kwa kuonesha mchanganuo sahihi kabla
kikao kijacho na kubadilisha mfumo wa utaratibu wa malipo ya fedha
taslimu, badala yake watumie benki ili kulinda mapato ya shirika.
Licha ya kuwepo kwa kasoro hizo, Mwenyekiti wa Kamati POAC, Zotto
alilipongeza shirika hilo kwa kujiendesha kifaida kutoka sh. bilioni
tatu hadi kufikia sh. bilioni sita na thamani ya mali za shirika hilo
kwa sasa imefikia sh. trilioni 1.75.
Zitto aliongeza kuwa shirika hilo linatakiwa kuendelea mchakato wa
kujiendesha kama kampuni ili liweze kupata mtaji wa kutosha. Kamati hiyo
ilitaka shirika hilo, kuzingatia mpango wa kujenga nyumba zenye gharama
nafuu kwa watu wenye kipato cha chini hususan maeneo ya vijijini.
No comments:
Post a Comment