Na Kenny Ngomuo - TGNP
Watanzania
tumeingia katika historia ya mchakato wa kuandika Katiba mpya ambao ni
shirikishi huku wengi wetu tukiwepo
katika harakati mbalimbali za
kimaendeleo hasa zile zakutafuta kipato na kuwakomboa kutokana na maisha duni yaliyojaa mifumo
kandamizi inayotokana na mila na tamaduni zilizowazunguka hasa watanzania
walioko pembezoni.
Pamoja na wanawake kuwa wazalishaji wakuu katika jamii
kuanzia ngazi ya familia wanawake wamekuwa waathirika wakubwa na michango yao imekuwa
hautambuliki katika pato la taifa. Suala la kwa nini wanawake na wasichana
wamebakia pembezoni katika nchi nyingi zinazoendelea ni dhana pana yenye mizizi
ya kihistoria, utamaduni, dini na hata saikolojia yenyewe. Matokeo ya utafiti
uliofanyika katika nchi za dunia ya tatu na Umoja wa Mataifa, yameonesha kuwa
wanawake walio wengi katika nchi nyingi
zinazoendelea bado wanazidi kuishi
maisha duni siku hadi siku ikiongozwa na mifumo kandamizi..
Utafiti
uliofanyika na Mtandao wa Jinsia Tanzania mwaka 2009 kuhusu kazi
wanazofanya wanawake zisizo na malipo, mfano kuhudumia wagonjwa
majumbani, kulea watoto na wazee ulionesha
wazi kuwa wanawake wanatumia nguvu na muda mwingi ambao hautambuliki popote
katika pato la taifa. Utafiti uliofanywa na Programu ya Chakula Duniani (World Food Programme) pia umeonesha kuwa mwanamke anatumia zaidi ya asilimia 90% ya pato lake kila
mwezi katika familia kwa njia ya aidha
kununua chakula, vitabu na madaftari ya
watoto, dawa , neti za kujikinga na mbu kwa ajili ya watoto wao na huduma
nyinginezo zinazofanana na hizo.
Pamoja
na changamoto nyingi ambazo wanawake wamekumbana nazo katika harakati zao za
kujikomboa, wanawake wamekuwa msitari wa mbele katika shughuli zote za
kimaendeleo katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Mchakato
wa ukusanyaji wa maoni ya kuandika Katiba mpya iko katika awamu ya pili . Zoezi hili limekwenda vizuri hasa kwenye
maandalizi na kuwepo kwa vifaa vya kuwezesha wananchi kuendelea kushiriki
katika kutoa maoni yao ya masuala ambayo wangependa yaingie katika Katiba mpya. Pamoja na mambo kadhaa mazuri, bado kumeendelea
kujitokeza mapungufu ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuweza kuboresha
ufanisi wa ukusanywaji wa maoni katika mikoa ambayo imesalia ambayo ni takrikbali mikoa 15 sawa na asilimia
50% ya mikoa yote ya Tanzania. Hii ni kutokana na utafiti uliofanyika mwezi Agosti na Septemba 2012 na Jukwaa la Katiba Tanzania.
Hata hivyo, imebainika kwamba mikutano mingi inafanyika
muda wa asubuhi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na baadaye mchana
kuanzia saa 8 hadi 11. Kwa uhalisia mikutano ya asubuhi haijawa rafiki kwa
wanawake hasa wale wanaoishi vijijini, ambao muda mwingi wa asubuhi wako katika shughuli za uzalishaji mali na kujitafutia
kipato, ambapo hata mijini pia muda bado ni changamoto.
Mfano, Jukwaa la Katiba
Tanzania lilipewa taarifa walipotembelea Kata ya Mwakaleli mkoani Mbeya, kuwa mikutano
ya asubuhi iliwanyima fursa ya kutoa
maoni wananchi wengi sana waliokuwa katika shughuli za uzalishaji mashambani
ambao wengi wao ni wanawake. Katika Mkoa wa Ruvuma, tatizo lilipelekea uwiano
wa wanawake na wanaume katika kushiriki mchakato wa utoaji maoni kuwa mbovu
sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, idadi ya wanawake walioshiriki
katika takribani mikutano 21 ya wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma
ilikuwa ni 1,949 tu kati ya jumla ya wananchi 8,915 sawa na asilimia 22% tu. Aidha, kutokana na uhamasishaji duni
kwa wanawake, hata uchangiaji katika kutoa maoni ulishuhudia wanawake
wakichangia kwa idadi ndogo sana ya 198 tu kati ya wananchi wote 2,074 waliotoa
maoni kwa Tume, sawa na asilimia 9.5% tu.
Kundi lingine ambalo limesahaulika ni hili lenye
mahitaji muhimu hasa watu wanaoishi na ulemavu wa aina mbali mbali. Bado watu
wenye ulemavu wa kuona, kusikia na kuongea hawajaweza kupewa fursa kubwa ya
kuweza kushiriki vema kutoa maoni yao. Hii ni kutokana na Tume kuendelea
kuitisha mikutano hii mbali na makazi ya wananchi walio wengi. Pia Tume
haijaweza kuandaa miundombinu kama vyombo maalum kwa wasioona na wakalimani wa
lugha za alama kwa wale wasio na uwezo wa kusikia na kuzungumza.
Natoa mapendekezo yafuatayo kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba mpya:
1) Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ihakikishe inawafikia
wananchi walioko pembezoni hasa wanawake
ambao kero zao nyingi zimekuwepo kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi kutokana na
mifumo, sera na sheria ambazo bado kandamizi na mfumo dume uliokithiri
2) Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni lazima iwasiliane
na wataalam wa lugha za alama na wataalam wengine na kuongozana nao mikoani na
wilayani ili watanzania wote wakiwemo walemavu waweze kufikiwa na kutoa maoni
yao kwa ajili ya Katiba mpya ijayo
3) Tume ifanye
utafiti kwa kila eneo wanalokwenda ili
kubainisha muda ambao ni rafiki kwa kila mwananchi aweze kushiriki na hili liende sambamba na matangazo ya
kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kutoa maoni
4) Mchakato wa
Katiba Mpya, uendelee kwa kasi ya kawaida na kwa umakini mkubwa bila kukimbizana
ili tuweze kupitia hatua zote za kuandika Katiba mpya ambayo ni shirikishi ya
kihistoria na ya kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment