Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
P.O Box 8921 Dar es Salaam
RIPOTI YA UFUATILIAJI WA MCHAKATO
WA UKUSANYAJI MAONI KWA AJILI YA UUNDAJI WA KATIBA MPYA TANZANIA (AWAMU YA PILI).
Tume
ya mabadiliko ya Katiba mpya iko katika awamu ya pili ya ukusanyaji wa maoni ya
wananchi kwa ajili ya uundaji wa katiba mpya. Zoezi hili limekwenda vizuri hasa kwenye
maandalizi na kuwepo kwa vifaa vya kuwezesha wananchi kuendelea kushiriki
katika kutoa maoni yao ya masuala ambayo wangependa yaingie katika katuba mpya. Vile vile
kumekuwepo na utulivu na ukarimu kwa wananchi walioweza kuhudhuria zoezi la
kutoa maoni hasa kwenye mikoa ambayo wajumbe wa Jukwaa la Katiba wameweza
kufikia.
Pamoja na mambo kadhaa
mazuri, bado kumeendelea kujitokeza mapungufu ambayo yanahitaji kurekebishwa
ili kuweza kuboresha ufanisi wa ukusanywaji wa maoni katika mikoa 15 ambayo
imesalia sawa na Asilimia 50 ya mikoa yote ya Tanzania.
- MUDA AMBAO MIKUTANO HUITISHWA BADO NI MBAYA !
Ilibainika kwamba mikutano
mingi ilifanyika muda wa asubuhi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na
baadaye mchana kuanzia saa 8 hadi 11. Kwa uhalisia mikutano ya asubuhi haijawa
muafaka hasa kwa wakazi wa vijijini, ambao wako katika uzalishaji mali.
Katika kata ya Mwakaleli mkoani Mbeya JUKWAA LA KATIBA lililalamikiwa kuwa
mikutano ya asubuhi iliwanyima fursa wananchi wengi sana waliokuwa katika
shughuli za uzalishaji mashambani. Hata katika maeneo ya mijini kama vile
Manispaa ya Morogoro na wilaya ya Mvomero, watumishi wengi wakiwemo wa umma na
serikali walilalamikia kutokuwepo utaratibu unaojulikana kuwa siku Tume
inapokusanya maoni katika maeneo yao basi wawe na ruhusa ya kutofika kazini au
kuruhusiwa mapema
- VITUO VYA KUKUSANYA MAONI KUWA VICHACHE KILA WILAYA
Waangalizi wetu walipokea
malalamiko toka kwa wananchi juu ya Tume kuruka Kata nyingi mno katika
kukusanya maoni. Hii ilichangia sana kwa Wananchi wengi hasa katika vijiji
visivyopitiwa na barabara kuu za lami kutojua hata endapo wilaya zao zilikuwa
zimeshapitiwa na Tume au bado. Katika moja ya Ziara ambazo JUKWAA LA KATIBA
lilifanya katika mikoa ya Singida na Simiyu kupitia iguguno, Mwando, Nduguti,
Kamlungu, Maheli, Gumanga, Igunia, Mkalama, Ibaga, Chemchem, Bukundi, Itaba
hadi Meatu, wanavijiji wengi walionekana kutojua kabisa kama kuna mchakato
unaoendelea wa Katiba Mpya na endapo mikoa na wilaya zao zilikuwa
zimekwishafikiwa au bado.
- RATIBA ZA TUME KUBANA UHAMASISHAJI NA MATANGAZO KUHUSU MIKUTANO YA UKUSANYAJI MAONI KABLA YA SIKU.
Pamoja na Tume kuchelewa
kutoa Ratiba ya awamu ya pili, kwa maeneo mengi Tume ilitoa kwa kuchelewa
matangazo ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya
kutoa maoni hivyo kusababisha wananchi wachache kuhudhuria mikutano hiyo
tofauti na ilivyotarajiwa. Katika maeneo mengi ya Mkoa wa Morogoro, kulikuwa na
malalamiko kuwa Tume ilichelewa sana kutangaza kuwa kutakuwa na mikutano na
hivyo kusababisha wananchi wengi kukosa fursa ya kutoa maoni yao..
- USHIRIKI MDOGO WA WANAWAKE
Katika Mkoa wa Ruvuma, tatizo lilipelekea
uwiano wa wanawake na wanaume katika kushiriki mchakato wa utoaji maoni kuwa
mbovu sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, idadi ya wanawake
walioshiriki mikutano katika mikutano takribani 21 ya wilaya za Tunduru na
Namtumbo mkoani Ruvuma ilikuwa ni 1,949 tu kati ya jumla ya wananchi 8,915 sawa
na asilimia 22% tu. Aidha, kutokana
na makosa hayo ya uhamasishaji duni kwa wanawake, hata uchangiaji katika kutoa
maoni ulishuhudia wanawake wakichangia kwa idadi ndogo sana ya 198 tu kati ya
wananchi wote 2,074 waliotoa maoni kwa Tume, sawa na asilimia 9.5% tu, ambayo
ni aibu.
- MAKUNDI YENYE MAHITAJI MAALUM HASA WATU WENYE ULEMAVU BADO YAMESHINDWA KUSHIRIKI KATIKA KUTOA MAONI
Katika awamu hii pia bado
watu wenye ulemavu wa kuona, kusikia na kuongea hawajaweza kupewa fursa kubwa
ya kuweza kushiriki vema kutoa maoni yao. Hii ni kutokana na Tume kuendelea
kuitisha mikutano hii mbali na makazi ya wananchi walio wengi. Pia Tume
haijaweza kuandaa miundombinu kama vyombo maalum kwa wasioona na wakalimani wa
lugha za alama kwa wale wasio na uwezo wa kusikia na kuzungumza. Katika hatua
za awali za kupanga awamu hii ya ukusanyaji maoni, Tume ilijaribu kuwasiliana
na wataalamu wa lugha za alama lakini kwa mshangao mkubwa Tume ikabadilika
ghafla na kusema ingekuwa gharama mno kutumia wataalam hao wa lugha za alama
kuongozana nao mikoani na mawilayani.
Hii imewanyima wananchi
hawa haki yao ya kikatiba ya kuweza kuchangia maoni yao kwa ufasaha. Hivyo,
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA bado linaishauri Tume kurekebisha suala hili nyeti
kwa haraka iwezekanavyo ili kutoa fursa kwa kundi hili la wananchi kutoa maoni
yao kwa ufasaha, kwa kuwa fedha zipo tena kwa kiasi cha bajeti ya shilingi
bilioni 34 kwa mwaka huu tu wa Fedha. Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha
kinacholingana na hata kuzidi baadhi ya wizara za serikali ya Tanzania!
- MAKADIRIO YA KATIBA MPYA KUPATIKANA IFIKAPO APRILI 2014 SI HALISIA.
Kutokana
na kusuasua kwa mchakato unaendelea wa ukusanyaji maoni, na hamasa ndogo
miongoni mwa wananchi juu ya Mchakato wenyewe wa Katiba Mpya huku sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83 ya Sheria (2012) ikiipa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba mamlaka hodhi ya kufanya karibu kila kitu katika Mchakato huu, inaanza
kujidhihirisha wazi kuwa ni jambo lisilowezekana kukamilisha hatua zote za
Mchakato wa Kupata Katiba Mpya ifikapo mwezi Aprili, 2014. Kwa mfano elimu ya
uraia inayotolewa ni finyu na haba kutokana na kubanwa na sheria husika
MAPENDEKEZO
1) Mchakato wa Katiba
Tanzania hautazaa Katiba Mpya ifikapo Aprili, 2014 na hivyo ipo haja ya kuanza
kujiandaa kwa hilo.
2) Kwa kuwa sababu kubwa ya
kukimbiza mchakato wa katiba Mpya ni haja ya wanasiasa kupata Katiba Mpya
itakayotumika katika uchaguzi wa mwaka 2015, JUKWAA LA KATIBA tunapendekeza
kuwa zipo njia mbadala za kuwezesha uchaguzi ufanyike kwa salama, amani na
utulivu hata bila kulazimika kukimbiza mchakato wa Katiba mpya
3) Kwa kuwa kikwazo kikubwa
katika kufanyika kwa uchaguzi kwa kutumia Katiba ya sasa ni Tume ya sasa ya
Taifa ya Uchaguzi ambayo uhuru na ufanisi wake unatiliwa mashaka, JUKWAA LA
KATIBA tunapendekeza kuwa kufanyike marekebisho makubwa kupitia ibara ya 98 ya
Katiba ya sasa katika vipengele vinavyohusiana na Tume ya Uchaguzi na usimamizi
mzima wa uchaguzi ili ifikapo April 2014 tuwe tuna ibara za Katiba zinazoweka
Tume huru na yenye ufanisi ili hatimaye ipewe jukumu la kusimamia chaguzi zote
zitakazofuata baada ya April, 2014 ikiwemo: Uchaguzi wa serikali za Mitaa,
mwishoni mwa 2014; uchaguzi mkuu 2015 na uchaguzi wa wajumbe watakaohitajika
katika vyombo vya kujadili na kupitisha Katiba Mpya ya Tanzania.
4) Kuhusu Mchakato wa
utungaji wa Katiba Mpya, JUKWAA tunapendekeza kuwa uendelee lakini kwa kasi ya
kawaida na kwa umakini mkubwa bila kukimbizana ili tuweze kupitia hatua zote za
uandishi wa Katiba ya Kidemokrasia hata baada ya uchaguzi Mkuu wa wa 2015.
No comments:
Post a Comment