Thursday, July 2, 2009

Washitakiwa mauaji ya albino kuanza kujitetea

Upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji ya albino inayoendelea Mahakama Kuu inayoketi mjini Kahama imefunga ushahidi wake baada ya shahidi wa 15 kutoa ushahidi na kielelezo cha ungamo la mshitakiwa wa tatu, Charles Kalamuji (42) na leo unaanza kusikiliza upande wa utetezi.

Akitoa taarifa ya kufunga ushahidi huo mbele ya Jaji Gabriel Rwakibalila, wakili mwandamizi wa serikali, Neema Ringo, alisema upande wa Jamhuri sasa hauna shahidi mwingine.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Masumbuko Madata wa kijiji cha Ituga na wenzake Emmanuel Masangwa wa kijiji cha Bunyihuna na Charles Kalamuji wa kijiji cha Nand Wilayani Bukombe kwa kumuua kwa makusudi mtoto albino, Matatizo Dunia (13) katika kijiji cha Bunyihuna.

Shahidi wa 15 katika kesi hiyo, F296 Sajenti Nasibu, aliwasilisha maelezo ya mshitakiwa wa tatu, Charles Kalamuji aliyoyatoa polisi kama kielelezo cha 15 na mahakama ilikubali kuyapokea licha upande wa utetezi kutoa pingamizi ambalo hata hivyo lilitupiliwa mbali. Mbali na washitakiwa kujitetea, mashahidi wengi wanatazamiwa kuwa ndugu zao.

CHANZO: NIPASHE

No comments: