Hapa hakuna kulia
Japo ni kali hisia
Janga lilotufikia
Lino limepindukia
Katika za sasa zama
Tumezipata zahama
Mwenzetu anapohama
Kutuachia dunia
Ni wengi walotutoka
Walotambuka mpaka
Na huko walikofika
Tumeshawasabilia
Jeraha lilo moyoni
Na fundo lilo kooni
In’sani hatuoni
Tutavyoyavumilia
Ela tujipe nafasi
Tupunguze zetu kasi
Mola tusije muasi
Kwa chazi lilozidia
Kenda zake kwa Manani
Atakayebisha nani
Ilobaki ni kuhani
Wale waliobakia
Harubu kenda harudi
Ndiyo yetu sote sudi
Kifo kwetu sote budi
Ahadi ikiwadia
Ela tukome kulia
Matama kujishikia
Tuweze kufurahia
Urithi alotwachia
Japo hakuna rufaa
Kaenda ali shujaa
Na nyingi zake shufaa
Rijali alotimia
Harubu alo azizi
Katimiza yake kazi
Bila kufanya ajizi
Sote tumemridhia
Mwanazuoni mahiri
Wanojua wamekiri
Kaacha wake muhuri
Kila alikopitia
Kawafunza wengi wana
Kwa mawazo yenye kina
Bila kufanya hiyana
Na wala kujivunia
Aliwapenda talibu
Naye hakuwapa tabu
Kuwaonyesha vitabu
Vitavyowasaidia
Nje ya lake darasa
Vichwa alivitakasa
Akijadili siasa
Nchini pia dunia
Alipinga ubeberu
Siasa za makaburu
Akitetea uhuru
Wa insani jumuiya
Tulochunguza kwa dhati
Twajua yake sauti
Mashariki ilo Kati
Akitufafanulia
Wahanga wa Palestina
Na Amerika Latina
Walijua lake jina
Kazi alowafanyia
Mzanzibari halisi
Hakupoteza nafasi
Kuwanasihi watesi
Ghadhabu kupunguzia
Upemba na Uunguja
Hakuiona ni hoja
Nyie nyote ni wamoja
Na mimi ni wenu pia
Muhimu tutende haki
Tusitumie bunduki
Wala pinde na mikuki
Hazitufai ghasia
Lino sanduku la kura
Ndiyo njia ya busara
La sivyo twala hasara
Tutaja likumbukia
Masanduku msibebe
Kura hizo msiibe
Acheni wenu ubabe
Harubu kawaambia
Raia wakihamaki
Wakidai zao haki
Mbona mwaleta mikiki
Moto kuwafyatulia
Wakubwa hakuogopa
Ukweli wao kuwapa
Na waliotoka kapa
Hilo wamejitakia
Kituo ameanzisha
Raia kuwakumbusha
Ari zao kuamsha
Waweze jisimamia
Iko siku inakuja
Wapemba na Waunguja
Watapeana faraja
Harubu alinambia
Leo kinachotuzuga
Na akili kuvuruga
Siasa za lugaluga
Bado twazishabikia
Umma utapoamka
Na hekima kucharuka
Dunia itazinduka
Kuja kutushangilia
Kwa upole akinena
Hajawahi kutukana
Alikuwa muungwana
Wote wanashuhudia
Letu si kuomboleza
Bali ni kumpongeza
Ngwe yake kamaliza
Nyingine katuachia
Kazize tuendeleze
Kiporo tusikilaze
Mpaka nchi ipendeze
Alivyokiitakia
Tumshukuru Saida
Kwa alotupa faida
Mume aso kawaida
Umma kuutumikia
Salamu, binti Yahaya
Pokea za jumuiya
Kwa hii kubwa hidaya
Uliyotutunukia
Ya Harubu buriani
Buriani ya Harubu
Ya Harubu buriani
Sote twakushangilia
Utenzi na: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment