WAKATI kukiwa na mjadala kuhusu mashirika ya dini kutoa elimu ya uraia, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Shehe Suleimani Lolila, amesema elimu hiyo ni haki ya jamii na kwamba itasaidia kupatikana viongozi bora.
Amesema mpaka sasa, Bakwata imeshatoa elimu hiyo katika wilaya zipatazo 16 katika mikoa ya Pwani, Iringa, Dodoma na sasa elimu hiyo itaanza kutolewa mkoani hapa. Shehe Lolila alisema hayo juzi wakati akizungumza na viongozi wa Bakwata kutoka Nachingwea, Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini, Lindi Vijijini na Kilwa.
Awali Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Larry Andre, ambaye alikuwa katika mazungumzo hayo, alisema Marekani imetoa msaada wa Sh milioni 38, kuisaidia Bakwata kutoa elimu hiyo kwa jamii mwaka huu. Balozi Andre alisema fedha hizo zilitolewa na watu wa Marekani ili kudumisha demokrasia ya kweli ambayo italeta amani ndani na nje ya nchi.
Alisema elimu hiyo inahusisha zaidi kufahamu utawala bora, sheria, Katiba, uwajibikaji na haki ya jamii kusikilizwa na kumchagua kiongozi bora atakayeonekana anafaa. Aliongeza kuwa nchi nyingi zinakuwa katika uchaguzi baada ya muda kunatokea vurugu, hali inayosababishwa na uelewa mdogo wa elimu hiyo.
“Mimi nimekaa nchi nyingi za Afrika, utaona mwananchi anakwenda kupiga kura akiwa mnyonge na hana furaha yoyote ile kutokana kutokuwa huru. Hali hiyo inasababishwa na ufahamu mdogo wa elimu ya uraia,” alisema Balozi huyo.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment