-Hekta milioni 6 za ardhi Afrika zimeshamegwa kwa wageni
MWANZONI mwa Julai mwaka huu, mawaziri wa kilimo barani Afrika watakutana kujadili pamoja na mambo mengine, uwekezaji katika kilimo.
Mkutano huu utafanyika miezi michache tu baada ya Tanzania kushinikizwa na baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuifanya ardhi iwe mali ya kila mwanajamii bila kujali mipaka ya nchi.
Ajenda ya kuifanya ardhi kuwa ya mali stahiki ya kila mwana Afrika ya Mashariki ilikuwa na jambo lililojificha; nalo ni ile dhana ya ukoloni mambo leo.
Baada ya ajenda ya mwaka 1885 iliyoligawa bara la Afrika (kule Berlin, Ujerumani) kwa wakoloni na kufuatiwa na harakati za uchimbaji wa madini (Gold Rush)za miaka ya 1900, sasa ardhi ndiyo lulu na tunu inayokimbiliwa kwa kasi na raia kutoka nje ya nchi katika jina la wawekezaji.
Katika kipindi cha miaka miwili tu iliyopita (2007-09) zaidi ya hekta milioni sita na ushee barani Afrika, zimemegwa na kupewa wanaojiita wawekezaji kutoka Ulaya, China, India, Arabuni na Korea.
Nchi za Uingereza, China, Falme za Kiarabu, India na Korea ya Kusini ndizo nchi zinazoongoza kwa kuingia mikataba ya uwezekaji katika ardhi katika nchi za Afrika.
Lengo kuu la wawekezaji hao ni kuzalisha chakula na nishati ya mafuta itokanayo na mimea (biofuel). Wenye uchungu na Afrika wanawaita “wakoloni mambo leo” ingawa watawala wengi wa Afrika wanawaita “wawekezaji”. Tofauti ya maneno haya inatokana na dhana na nia ya wageni hao wanaokuja Afrika-kama wanakuja kuchuma na kuondoka au ni wadau wa maendeleo wa Waafrika?
Huko Sudan, kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya mwenendo wa kiuchumi (Economic Bureau) ya Uingereza, kwa mwezi Mei 2009, Korea ya Kusini imepata hekta 690,000 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha ngano. Sio ngano ya wana-Sudan; la hasha ni ya Wakorea.
Falme za Kiarabu tayari zinalima hekta 30,000 na majuzi imeongeza hekta 378,000 kulima mtama, nyasi za ng’ombe, ngano, viazi na maharage kwa ajili ya wananchi wake.
China nayo imepewa hekta milioni 2.8 huko Congo (Brazaville) ili kuanzisha shamba kubwa zaidi la michikichi duniani na bado imo mbioni kuitaka Zambia iipe hekta milioni mbili kwa ajili ya kulima mibono (minyonyo).
Hapa Tanzania bado hakuna wawekezaji wakubwa katika kilimo kama ilivyo katika nchi hizo, lakini viwango vya ukubwa wa eneo la kulima vinazidi kukua kila siku.
Mamilioni ya hekta za ardhi nzuri huko Morogororo, Rukwa, Tabora, Lindi, Pwani, Kigoma, Manyara na Ruvuma yameanza kukodolewa macho, na yataendelea kukodolewa na wanaojiita wawekezaji kwa kushirikiana na baadhi ya wenye dhamana hapa nchini.
Tayari bonde la mto Kilombero, mkoani Morogoro, limeanza kunyemelewa kwa kasi na wawekezaji na wananchi wameanza kulionja joto na adha ya uwekezaji wa kilimo cha sukari na mpunga.
Kwa nini wawekezaji hao wanakuja Afrika na sio Asia au Marekani ya Kati au Kusini? Sababu ni kuwa Afrika ndilo bara pekee lililosalia na ardhi nzuri inayoweza kulimwa kila zao kwa gharama ndogo. Ni bara ambalo mwekezaji anahitaji kuja na mkoba mtupu na pesa kiduchu kulala hotelini siku tatu tu na baada ya muda mfupi anakuwa bilionea.
Mataifa ya nje yanataka kupata faida kubwa ya kuuza chakula na mazao ya mafuta (petroli inapanda bei) wakati huu ambapo uhaba wa chakula na mtikisiko wa uchumi ndizo ajenda za kila siku za kimataifa na kitaifa.
Nchi za nje ya Afrika zinakuja kulima Afrika ili kuwalisha watu wao na ziada ikiuze tena kwenye nchi hizo hizo zinazowakaribisha kulima! Hata mafuta ya mitambo na magari yatokanayo na mimea inayolimwa barani Afrika, yatauzwa tena kwa nchi waalika.
Tangu kuanza kushuka kwa uzalishaji wa chakula kati ya 2007/08 na ongezeko la idadi ya watu kwa asilimia tatu tangu 1945, ardhi haijaongezeka kwa eneo. Akiba ya chakula duniani imeshuka kutoka ya siku 116 mwaka 1995 hadi akiba ya siku 57 mwaka 2008, alibainisha Gwynne Dyer mwanahabari wa Economic Bureau.
Ndiyo maana nchi za wenzetu “wenye akili” zimeanza kuja Afrika kulima wakati sisi Waafrika tukiendelea kuimba nyimbo za “kilimo kwanza” na ‘kuruka hewani kwa kutumia ungo’, au kupigana wenyewe kwa wenyewe. Wao watakapokuwa wanavuna sebuleni kwetu, sisi Waafrika tutakuwa tunaugulia njaa, umaskini na kuomba chakula na mafuta! Kweli wajinga ndio tuliwao. Tutaanzishaji Kilimo Kwanza kabla ya kutathmini Siasa ni Kilimo” ?
Kama China itaendelea na sera yake ya kuwatawanya raia wake milioni 5 kila mwaka hasa barani Afrika, ni dhahiri kutakuwa na msukomo wa kupata ardhi kupitia kwa watawala wenye kutafuta ufadhili binafsi na wa familia zao tu - yale yale ya akina Chifu Mangungu wa Mvomero! Lesotho tayari ina raia wa kichina zaidi ya 150,000; huku yenyewe ikiwa na wananchi milioni 1.8 tu.
Kwa upande wa pili, kumekuwa na wawekezaji wachache sana katika kilimo. Haishangazi kuona takwimu za Vituo vya Uwekezaji kama cha Tanzania (TIC) vina taarifa finyu za wawekezaji wanaolima kuliko waliojikita katika fani nyingine za utalii, biashara na madini. Wapo wanaoogopa kuwekeza katika kilimo kwa hofu ya kuogopa yale ya mwaka 1967 yalipotaifishwa mashamba makubwa. Lakini hawataki walime halafu Tanzania ijitosheleze kwa chakula. Watatuhadaa vipi tukishiba?
Lakini kwa jinsi upepo unavyokwenda, utakaposikia Falme za Kiarabu, India, China, Korea na wengine wanataka kupewa mamilioni ya hekta, basi ujue kiama kimekaribia.
Kwa nini kiama? Kwanza, wageni hawafahamu sana aina ya migongano iliyopo kati ya watawala wa nchi na wananchi kuhusu ajira na ardhi kama rasilimali yao kuu hasa kwa vijana. Wageni watakapoanza kununua ardhi kwa wingi, vijana wa kiafrika nao hawatakubali na watafanya mawili: ama kuwavaa wageni au kuwapa wakati mgumu viongozi wao kwa kuwapa wageni ardhi ya mababu zao.
Vijana wao hawatakubali kukosa ajira, elimu, afya bora, na sasa hata ardhi. Wataanzisha mapambano dhidi ya watawala na wageni.
Kabla ya kufikia hatua hiyo, inafaa sasa watawala wa Afrika ikiwemo Tanzania watambue kuwa wawekezaji wa nje katika ardhi wanataka kulima kwa ajili ya chakula chao na kupitia mazao kupata mafuta ya mitambo na magari kwa bei poa. Lakini hawatalima tu, kuna siku watakuja kuishi wao na watoto wao.
Watakapokuwa wanajadili mipango ya uwekezaji katika kilimo mwezi Julai mwaka huu, mawaziri wa Afrika watambue mwelekeo wa dunia na mikakati ya mataifa ya nje ya kurubuni bara la Afrika katika jina la uwekezaji.
Afrika ikae chonjo kweli kweli na mwelekeo huu wa mamilioni ya ardhi yetu kuhodhiwa na wageni huku tukiendelea kuzaa ili tusije kuwa na ulazima wa kukaribisha awamu ya pili ya mapambano mbele ya safari ndani ya nchi kati ya wasio na ardhi na wawekezaji ardhi.
Chanzo: RaiaMwema
No comments:
Post a Comment