MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA)imetangaza kupanda kwa bei za rejareja kwa aina zote za mafuta nchini. Taarifa ya Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Haruna Masebu imesema kuwa bei ya Petroli imepanda kwa asilimia 4.00, Dizeli (5000 ppm) asilimia 4.74, Dizeli (500 ppm) asilimia 3.55 na mafuta ya taa asilimia 7.93.
Taarifa hiyo imesema mabadiliko haya ya bei za mafuta yametokana na mabadiliko ya bei katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani. Hata hivyo, amesema kuwa Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo ya asilimia 7.5 ya bei elekezi kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA hatimaye kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali No. 5 la tarehe 9 Januari 2009.
Mkurugenzi huyo amewataka wanunuzi kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, ambayo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo mteja atauziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
No comments:
Post a Comment