Thursday, July 2, 2009

‘Jeneza’ la Tarime, Rorya lachongwa

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametangaza azma yake kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuzifuta wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, kutokana na viongozi wa wilaya hizo kushindwa kusimamia amani.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati akihutubia maelfu ya wananchi na viongozi wa wilaya, mikoa, halmashauri na manispaa nchini, walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Sherehe za Serikali za Mitaa kitaifa ambazo zilifanyikia mkoani Mara.

Waziri Pinda ambaye alionesha kukasirishwa na mapigano ya koo na makabila mkoani humo, alisema serikali imechoka kuona maisha ya watu yanapotea na mali zao kuharibiwa huku viongozi wakiwapo, lakini wameshindwa kusimamia wananchi wao kwa kuwakalisha chini na kumaliza tofauti zao na kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo mikoa mingine.

Sambamba na kutishia kuzifuta wilaya hizo na kuteua wanajeshi kuziongoza, alitoa miezi sita ya huruma kwa wakuu wa wilaya hizo na wa halmashauri, kuhakikisha wanaandaa taarifa za mikakati yao ya kukomesha mapigano ya koo chini ya uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Enos Mfuru, vinginevyo hawatakuwa na kazi.

Pinda alisema kwa mwaka jana pekee yalikuwapo matukio 66 ya mapigano ya koo ambapo ng’ombe 601 waliporwa na watu wengi kupoteza maisha.Na katika mapigano ya sasa baina ya watu kutoka Tarime na Rorya, alisema watu 32 wamekufa, zaidi ya nyumba 400 zimechomwa moto na watu zaidi ya 3,000 hawana makazi kutokana na upuuzi wa wizi wa ng’ombe watano ambao kati yao watatu walipatikana na kuzua balaa la vita.

Alieleza mikakati ya kukomesha uhalifu katika wilaya hizo kuwa ni kuanza utekelezaji wa kuzifanya Tarime na Rorya kuwa mikoa ya kipolisi, kuanzisha kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Tarime, kudhibiti fujo na wizi wa mifugo.

Mikakati mingine ni ya kuimarisha barabara za mipakani na kuwasisitizia viongozi wasikwepe majukumu ya kufanya wilaya hizo zikalike. “Nasema suala hili si la kuchezea hata kidogo, Rorya Rais kamweka mwanajeshi mstaafu na Tarime tumempeleka kada wa CCM, kama anapwaya tutambadilishia kituo cha kazi apelekwe mwanajeshi,” alisema Pinda.

No comments: