Tuesday, July 28, 2009

`Fichueni wauaji wa albino`

JamiiI imeaswa kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuwafichua watu wanaoendesha mila na imani potofu kwa kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe ili kutokomeza unyama huo.

Aidha jamii imetakiwa imrejee Mwenyezi Mungu kwa kuishi maisha ya kistaarabu ya kupendana, kuheshimiana, kuthaminiana kwani kila kundi lina haki ya kuishi maisha yenye amani na upendo na si kuwindwa kama ndege.

Wito huo ulitolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe, kwenye uzinduzi wa albamu ya Tuhurumie iliyotayarishwa na Nzega Disabled Talent (NDT).

Albamu hiyo ilizinduliwa na kwaya ya watu wenye ulemavu, wakiwemo albino na ilifanyika kwenye uwanja wa Parking wilayani Nzega, mkoani Tabora.

Bashe alisema kila jamii nchini ina wajibu wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe kwani wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kuandamwa, hivyo kupoteza imani kama nao wanastahili kuishi kwa amani kama binadamu wengine.

Alisema vita hiyo ni ya kila mwananchi kwani kama ikiachiwa serikali pekee itakuwa ni vigumu wahusika wa unyama huo kubainika kwani wanajificha ndani ya jamii.

Katika uzinduzi huo, Bashe alisema kitendo cha kualikwa kwenye hafla hiyo kimedhihirishia Tanzania haina matabaka wala mipaka ya kidini katika shughuli za maendeleo yanayohusu jamii kwa ujumla.

Awali kwenye risala ya walemavu kwenye uzinduzi huo, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Christian Church of Tanzania (PCCT) na Mwenyekiti wa NDT, Mchungaji Yohana Nghumba, alisema mfuko huo unaendeshwa chini ya kanisa hilo wilayani Nzega.

Source: Nipashe

No comments: