Monday, July 13, 2009

Mwezesheni mwanamke kuleta maendeleo-Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka wananchi kuwekeza zaidi katika kulinda uwezo wa kipato kwa mwanamke hasa watoto wa kike kwa kuwapeleka shule na kuwapatia taarifa zinazowawezesha kukua na kumaliza masomo yao katika misingi imara ili wachangie kuondoa umaskini.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani yaliyofanyika Kkitaifa Mkoani Shinyanga.

Pinda alisema endapo jamii ikimwezesha mwanamke katika kuleta maendeleo ya jamii hasa kwa wale wenye kipato cha chini kutasaidia kuondoa umaskini na kuleta maendeleo endelevu ya Taifa.

Pinda alisema kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu duniani inayokadiriwa kufikia billioni 6.77 na kwamba katika idadi hiyo inakadiriwa kuwa wanawake ni zaidi ya nusu, ni dhahiri kuwa maendeleo ya dunia yatapata misukosuko zaidi.

Alisema kuwa maadhimisho haya yanatoa tathmini kwa Taifa mafanikio ya juhudi pamoja na mikakati katika kumwekeza mwanamke na kuhakikisha kuwa mwanamke anapewa nafasi inayostahili katika kumwezesha kushiriki katika kujiletea maendeleo.

Waziri Pinda alisema kulingana na kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka huu inayosema kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani:kuwekeza katika kuwaendeleza wanawake ni chaguo sahihi, inaelezea umuhimu wa mwanamke katika kumwendeleza kwa lengo la kuinua maendeleo ya jamii.

Mkoa wa Shinyanga una watu milioni 3.6 na ndio mkoa unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu tofauti na mikoa mingine ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza.

No comments: