CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema suala la Mwafaka wa kisiasa kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM), limekwisha na walikuwa wakijipanga, na sasa wako tayari kuwapa Watanzania fursa ya kuchagua Dira ya Mabadiliko na kuitumia kuongoza harakati za kuing’oa madarakani CCM kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.
Aidha, chama hicho kimeeleza kushangazwa na hatua ya CCM ‘kuchumpa’ katika suala la kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, suala ambalo liliwekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala ya mwaka 2005, na katika siku za karibuni, kuzua mjadala nchini.
“Mwafaka ulikwisha. Tulikuwa tumeshafikia makubaliano na wenzetu na kilichobaki ni ceremony (sherehe) za kusaini Mwafaka, lakini wenzetu wakachumpa. Hatuzungumzii tena suala hili. Tutaicheza ngoma kwa kadri itakavyokuwa inadundwa,” ilikuwa kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ‘Operesheni Zinduka’.
Profesa Lipumba akiwa na viongozi wengine wakuu wa CUF, alisema suala la Mwafaka halina nafasi tena, bali chama hicho kitakabiliana na mambo kwa kadri yatakavyokuwa yakitokeza, lakini muhimu kwa sasa ni kuwapelekea wananchi Dira ya Mabadiliko ambayo inatilia mkazo mambo 13.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kila raia popote alipo kuwa na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi; kujenga umoja wa kitaifa wa kweli; kuhakikisha kuwa kila mwananchi ana uwezo na anawezeshwa kupata milo mitatu kwa siku; kuhakikisha kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya; kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee na watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi na ya sekondari.
Mambo mengine ni motisha maalumu utolewe kwa wasichana na familia zao ili wamalize elimu ya msingi na waendelee na sekondari; kuwaelimisha wasichana na wanawake washiriki katika soko la ajira; Taifa litoe kipaumbele maalumu katika kuendeleza elimu ya sayansi na teknolojia.
“Kujenga uchumi wa kisasa wenye ushindani wa kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi; wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa Taifa unatoa fursa kwa wananchi wote; kukuza uchumi na kuongeza ajira na kuwapo kwa uongozi imara na utawala bora katika kukuza uchumi,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza kuwa CUF imeandaa dira huyo ya kuleta mabadiliko kupitia mijadala.
Alisema kwa kuanzia, CUF itazindua ‘Operesheni Zinduka’ Julai 11, mwaka huu katika Jiji la Mwanza, na itafanya kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza katika mikoa 11 ya Bara itakayohusisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora na Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya na Morogoro.
Alisema CUF itaongoza kampeni hiyo ya mabadiliko kwa sababu ndicho chama kikuu cha upinzani Tanzania, kiko imara na kina viongozi makini. “Vyama vingine vya siasa vimejionyesha kuwa ni vyama vilivyopo kwa maslahi ya viongozi wake wachache wanaovifanya kama ni miliki yao na ambao hawawezi kuhojiwa na hivyo kupelekea vyenyewe kuzama katika ufisadi na kushindwa kujiendesha.
Vingine ni dhaifu na visivyo na mtandao wa kitaifa wa kuweza kuleta mabadiliko ya maana yatakayoleta tija,” alisema Lipumba na kuongeza: “Kwa chama makini cha siasa kinachopigania mabadiliko, kufichua maovu na ufisadi au kwa lugha ya mtaani ‘kulipua mabomu’ pekee hakutoshi kuleta ukombozi wa kweli wa Mtanzania. Kauli za hamasa na jazba ni muhimu kuwapa wananchi ari ya kujiletea mabadiliko katika maisha yao.”
Alisema mabadiliko wanayotaka Watanzania hayawezi kuja kwa njia za kushitukiza na kuongeza kuwa “Watanzania wanastahili kuwa na Dira ya Taifa ya kujenga nchini inayoheshimu haki za binadamu, yenye misingi mizuri ya demokrasia ambapo raia wote watu wazima wenye akili timamu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa masuala yanayohusu maisha yao na hatma ya nchi yao.”
Akijibu maswali mbalimbali ya wahariri, Profesa Lipumba alisema CUF itaendelea kudai Katiba na Tume huru ya uchaguzi, huku akimtupia lawama Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame akidai ni ‘goigoi’ ambaye atastaafu wadhifa huo akiwa hana la kukumbukwa.
Aligusia suala la Mahakama ya Kadhi, akisema, “Hili limewekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na wenzetu, tena wasomi baada ya kuisoma wakasifu sana, lakini sasa wanachumpa. Hili litaleta vurumai.”
Aidha, Profesa Lipumba pia alimsifu Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM) kwa hoja yake bungeni kuhusu mgawanyo wa fedha za barabara, ingawa alisema kumekuwa na vituko vingi bungeni kutoka kwa wabunge wa chama tawala katika michango yao hivi sasa.
Kuhusu Operesheni Zinduka na pigo la hivi karibuni la CUF kuondokewa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, Wilfred Lwakatare aliyehamia Chadema, Profesa Lipumba alisema muhimu ni kujenga chama kama taasisi na siyo kutegemea sifa ya mtu binafsi.
“CUF inaamini katika kujenga chama kama taasisi, chama ni demokrasia, personality ni muhimu katika siasa, lakini chama kijengwe kama taasisi, ili anapoondoka mtu hakiathiriki. Hili la kuondoka kwa watu tunaowajenga, linasikitisha, linanifedhehesha, lakini huwezi kulikwepa,” alisema mchumi huyo.
No comments:
Post a Comment