-Mashehe wataka nao wahusishwe
-Askofu asema ni mkataba usiobagua
-Serikali ya Kikwete njia panda
SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete, imezidi kuingiwa na misukosuko inayogusa waumini wa dini mbalimbali, na sasa kumeibuliwa hati ya makubaliano (MoU) ambayo Serikali iliingia na makanisa nchini. Makubaliano hayo yalikuwa hayafahamiki kwa Watanzania wengi.
Hati hiyo ya makubaliano, ambayo ilisainiwa na Serikali wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, inaelezwa kuzipendelea zaidi taasisi za Kikristo zinazotoa huduma nchini.
Baadhi ya viongozi wa Kiislamu nchini, wameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba mkataba kama huo waliouandaa ulipata kukataliwa na serikali pamoja na kuwa ulifanana kwa kila kitu na huo.
Tayari mjadala wa serikali kujiingiza katika masuala ya dini unazidi kupamba moto ukihusisha uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya Waislamu na kuwapo Waraka wa Kanisa Katoliki unaoelimisha waumini wake kuhusu uchaguzi.
Serikali iliutia saini rasmi hati ya makubaliano kati yake na Baraza la Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (CPT), huku Serikali ikiwakilishwa na Edward Lowassa ambaye wakati huo alikuwa waziri mwandamizi.
Hati hiyo, ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, iliandaliwa na Profesa Costa Mahalu alipokuwa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika hati hiyo, iliyotiwa saini Februari 21, mwaka 1992, upande wa serikali uliwakilishwa na mmoja wa mawaziri wake waandamizi wa wakati huo.
Makubaliano hayo yalifanyika kwa kuzingatia mambo kadhaa, ambayo ni pamoja na hali ya uchumi nchini kutomudu kuiwezesha serikali kutoa huduma za elimu na afya kwa kiwango bora.
Msingi mwingine wa makubaliano hayo ni makanisa kuhakikishiwa kuwa serikali itaweka mazingira mazuri kwao kutoa huduma za elimu na afya.
Makubaliano hayo yamegawanywa katika maeneo makubwa mawili, ambayo ni sekta ya elimu na afya na kila sekta ikiwa imetengenezewa bodi yake ndani ya mtandao wa makanisa kupitia CCT na TEC.
Kwa mfano, sehemu ya kwanza ya hati ya makubaliano hayo, kifungu cha kwanza, kinaeleza kuwa makanisa yataanzisha kamisheni ya uratibu wa utoaji huduma hizo.
Katika kifungu hicho cha kwanza, sehemu ‘a’ hati hiyo inaeleza kuwa jukumu la kamisheni hiyo ni kuandaa sera zinazohusiana na huduma za afya na elimu zinazotolewa na makanisa.
Kifungu kidogo cha nne, sehemu hiyo ya kwanza ya hati hiyo, kinaeleza kuwa kamisheni hiyo itakuwa ikiratibu na kusimamia matumizi ya fedha, mikopo kwa ajili ya kuboresha huduma za elimu na afya.
Hati hiyo pia inaeleza kuwa wajumbe wa kamisheni hiyo watatoka katika CCT na TEC na mashirika wafadhili na kwamba ni lazima shughuli zote ziendeshwe kwa mujibu wa sera na sheria za nchi.
Serikali kupitia hati hiyo pia imekubaliana na makanisa kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Kijamii ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kupokea mikopo na misaada.
Pia kwa upande wa elimu, serikali ilikubali kutoa nafasi za masomo ya mafunzo wa ualimu kwa wanafunzi wa ualimu.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment