KUMEIBUKA upotoshaji wa makusudi wenye malengo ya kuwakatisha tamaa wabunge kutimiza jukumu la msingi, kwa mujibu wa Katiba, la kuishauri na kuisimamia serikali, Raia Mwema limedokezwa.
Upotoshaji huo unaolenga kuwaondoa katika jukumu hilo wabunge wanaohoji ufisadi dhidi ya maliasili za Taifa unatajwa kutumia mbinu mbalimbali.
Moja ya mbinu hizo ni kufanya propaganda ili kugeuza misimamo ya wabunge hao ya kuhoji vitendo vya ufisadi serikalini ili iaminike kwa Watanzania kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa chuki binafsi dhidi ya mawaziri.
Mbali na mbinu hiyo, mbinu nyingine ni kuhusisha suala la udini kwa kulinganisha dini ya mbunge na waziri anayeshambuliwa.
Baadhi ya wabunge walioanza kushughulikiwa na mkakati huo usio na tija kwa Taifa ni pamoja na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango-Malecela, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, Jenista Mhagama na Mbunge wa Ilemela, Antony Diallo.
Kwa nyakati tofauti, wabunge hao waliwabana baadhi ya mawaziri, wakiwamo Dk. Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Shamsha Mwangunga.
Hata hivyo, mbinu hizo zinazotajwa kuwa ni chafu na zisizo na maslahi yoyote kwa Taifa kwa kuwa wabunge hawashambulii mawaziri binafsi, bali wanachoshambulia ni madaraka ya uwaziri kutotumika kulinda maslahi ya nchi, zimeanza kugonga mwamba miongoni mwa wananchi.
Taarifa zaidi zilizotufikia zinaeleza kuwa baadhi ya mawaziri walifikia hatua ya kutaka kuhujumu mpango wa Anne Kilango, kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu wizi wa pembe za ndovu zilizosafirishwa kwenye makontena mawili na kukamatwa nchini Vietnam.
Mawaziri hao wanadaiwa kupiga kampeni kwa wabunge wasio na msimamo wa kutetea raslimali za Taifa ili kama Kilango angewasilisha hoja hiyo siku ya pili ya mjadala wa bajeti wa Wizara ya Maliasili na Utalii, akwamishwe bungeni.
Inadaiwa kuwa usiku wa kuamkia siku ya pili ya mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, mawaziri hao walipiga kampeni kwa wabunge hao ili wampigie makofi Waziri wa Maliasili na Utalii, dhidi ya Kilango.
Ingawa mkakati huo unatajwa kufanikiwa kwa kiasi fulani, lakini umezua maswali mengi ikiwa ni pamoja na ufahamu wa wabunge waliofanikisha mpango huo.
Inaelezwa kuwa kutokana na kasi ya Bunge katika kuhoji ufisadi, viongozi waovu serikalini wameanza kujipanga kukabili hali hiyo kwa kutumia mbinu hizo.
“Tunawashangaa wenzetu, wanashawishiwa kwa kampeni ya kupuuzi eti wapige makofi kwa wingi kum-support waziri dhidi ya Kilango, na wanajenga hoja yao katika msingi kwamba wabunge wenye misimamo mikali wana wivu.”
“Hivi ni wivu gani huo mtu anapohoji kuvushwa kwa pembe za ndovu kontena mbili na maofisa wa Tanzania wakitoa nyaraka feki, halafu mbali kontena zinakatamwa nje ya nchi?” alisema mmoja wa wabunge aliyezungumza na Raia Mwema na kuongeza kuwa;
“Mimi niseme tu kwamba ingawa tupo wabunge takriban 300 lakini tija inayotokana na wingi huu ni ndogo kulinganisha na idadi. Wengine ndiyo hao wanashawishiwa kwa hoja za kipuuzi.”
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment