Wednesday, July 15, 2009

JK ateua majaji wa mahakama kuu wapya 10

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameteua Majaji Wapya Kumi (10) wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uteuzi huo ulianza Juni 26, mwaka huu, 2009.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo Jumatatu Ikulu, Dar es Salaam imewataja majaji hao kuwa ni Bwana Ferdinand Leons Katipwa Wambali, aliyekuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani; Bibi Eliamnani Godfrey Mbise, aliyekuwa Msajili Mahakama Kuu na Bibi Sekela Cyril Moshi, aliyekuwa Mkurugenzi Mahakama za Wilaya hadi Rufani.

Wengine ni Bibi Fatuma Hamisi Masengi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo, Bwana Sivangilwa Mwangesi, aliyekuwa Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani; Bibi Pellagia Barnabas Khaday, aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Bwana Moses Gunga Mzuna, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Iringa.

Taarifa hiyo iliwataja Majaji wengine wapya wa Mahakama Kuu kuwa ni Bibi Hamisa Hamisi Kalombola, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Mbeya; Bibi Fredrica William Mgaya, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Mwanza na Profesa Ibrahim Hamisi Juma aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments: