Tuesday, March 31, 2009

Tujikumbushe ya rada, tusijesahau

SASA imedhihirika kwamba Mkataba wa Ununuzi wa Rada wa mwaka 1999, kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uingereza ya BAE Systems, uligubikwa na rushwa kubwa, kwa mujibu wa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya nchini Uingereza – Serious Fraud Office (SFO).

Wapelelezi wa ofisi hiyo juu ya mkataba wa ununuzi wa chombo hicho kwa Sh. bilioni 40 wamekuwa wakipeleleza kampuni hiyo na washukiwa wanane, wakiwamo Waingereza wanne - Sir Richard Harry Evans (67), Michael Peter Rouse (61), Michael John Turner (61), John Aldridge (52), na Watanzania watatu (majina tunayo, umri miaka 63, 44 na 45).

Katika taarifa yao ya awali ya Machi 2008, walisema: “Kuna kila sababu kuamini kwamba watu wote hao na Kampuni ya BAE Systems walitenda makosa ya rushwa katika ununuzi warada hiyo”.

Wakibainisha jinsi sehemu ya mavuno ya rushwa hiyo yalivyogawanywa kupitia benki mbili za kigeni, kati ya Juni 19, 1997 na April 17, 1998, taarifa hiyo inasema hivi kuhusu Wa/Mtanzania hao/huyo: “SFO inahitimisha kwamba kuna kila sababu na kwa ushahidi tosha kwamba kwa kufanya hivyo (watu/mtu hao/huyo) alikuwa akiuweka uchumi wa Tanzania hatarini”.

Ni dhahiri pia kuwa Serikali inawajua watu hao nao wanajijua; na ingekuwa kwa Nchi Zilizoendelea, zenye kuheshimu dhana ya kuwajibika, wangekuwa wameachia ngazi zamani kuponya nyuso zao. Lakini si kwa Mtanzania, ambaye kwake wizi, ubadhirifu na ufisadi ni ushujaa wa kupokelewa kwa kutandikiwa zulia jekundu.

Ningekuwa mimi ndiye Rais, ningewashauri watu hao kuachia ngazi kiungwana ili kutoipaka tope serikali yangu. Ningekuwa mimi ndimi mshukiwa, nafsi yangu ingenisuta na kujiuzulu sawia. Huu ndio uungwana; huu ndio ustaarabu wa binadamu, wa kuweka mbele maslahi ya walio wengi, tofauti na wanyama kama Nyang’au, wanaoweka maslahi binafsi mbele kwa maana ya “Rule of the Jungle”- Kanuni za mwituni”. Na haya yanapotokea, tuliowaweka kusimamia serikali, wako wapi?. Au wametusahau kwa kujichongea mzinga wa asali?

Tabia ya kikundi cha viongozi wachache ya kulishwa asali kidogo na wawekezaji kwa kutumia mamluki wa ndani, ili kutetea manunuzi na uwekezaji usio na maslahi kwa taifa, inaendelea kuitafuna nchi. Tumejionea hili kwa mradi wa IPTL, ununuzi wa ndege mbovu ya Rais, mbuga za wanyama (Ortello), Richmond, mikataba ya madini na sasa Dowans, bila kusahau sakata hili la Ununuzi wa Rada.

Miradi yote hii imethibitika kuwa bomu la maangamizi kwa Taifa kiuchumi na kijamii. Na kwa nguvu ya fedha ya kifisadi, imeweza kuingiza “wateule” Bungeni, Chama tawala, Taasisi nyeti za serikali na serikali kuu. Ndiyo maana kero za wananchi hazipati majibu kutokana na jeuri za kifisadi, eti kwamba “dua la kuku halimpati mwewe”.

Ungekuwa mmoja wa waliotetea ununuzi wa rada na ndege ya Rais kwa maneno makali ya kutunisha mishipa ya shingo; kisha unagundua kwamba kwa kufanya hivyo uliudanganya umma, ungefanyaje? Ungekuwa na ujasiri tena kusimama kadamnasini, macho makavu, na kuusalimia umma unaoteseka kiuchumi kwa ulaghai wako?.

Rais Richard Nixon wa Marekani, kwa ustaarabu, alijiuzulu urais kwa kashfa ya Watergate. Naye Waziri Mkuu wa Israeli, amejiuzulu hivi karibuni kwa kashfa ya rushwa; wengi walipita njia ulimwenguni, kwa ustaarabu wao; wewe je? Utetezi wa matusi kwa kujificha ndani ya mbawa za chama kinalisaidia nini Taifa lako?.

Rushwa ya mtu mmoja ni mbaya vya kutosha, lakini Serikali nzima inapohusishwa na rushwa kwa matendo ya wachache ndani yake wasioguswa, kwa sababu tu wanaonekana kukipenda chama tawala kuliko Taifa, hili si jambo la kufumbia macho.

Tuangalie mfano wa sakata la rada. Wakati hoja ya utapeli wa mkataba huo ilipoibuliwa na wapinzani, Naibu Waziri wa Fedha, Abdulsalaam Issa Khatibu; Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mark Mwandosya na Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi ya Usafiri wa Anga, Margareth Munyangi, ndio waliokuwa wa kwanza kutetea mradi huo wakisema: “Rais hawezi kudiriki kamwe kuacha usalama wa wasafiri wa ndege, mikononi mwa bahati nasibu”.

Hakuna aliyekuwa akipinga hili, bali kilichopingwa ni bei kubwa na ubora hafifu wa kifaa hicho mtumba, kwa sababu tayari jumuiya za kimataifa na Waziri Clare Short wa Uingereza, walikwishaonya na kuitahadharisha Serikali juu ya ulaghai wa dili hilo. Kwa nini hawakuamka kwa tahadhari hiyo?

Naye Rais Benjamin William Mkapa, kwa kuambukizwa na watu waliomzunguka, na pengine kwa kutumia Chama, akiwa ziarani Mbeya alitetea ufisadi huo akisema: “Wanaoikosoa Serikali si tu wanaibeza Serikali na Chama chake, bali wanawabeza Watanzania waliokipatia Chama cha Mapinduzi mamlaka ya kutawala kwa wingi wa kura (bila kujali zilivyopatikana) ili kiweze kutekeleza ilani na sera sahihi, zenye kulenga kumletea maendeleo mwananchi….. Hao ni vipofu na viziwi”.

Baada ya kuthibitika kwamba ndege ya Rais na rada aliyokuwa akitetea ni mabomu na kikwazo kwa maendeleo ya mwananchi; kati ya yeye na hao aliowaita eti ni vipofu na viziwi, ni yupi aliyekuwa akiwabeza Watanzania?.

Tangu mwanzo, Baraza la Mawaziri la Uingereza lilikuwa limegawanyika juu ya Uingerza kuiuzia Tanzania ndege mbovu, licha ya kwamba zoezi zima lilikuwa la udanganyifu. Waziri wa Fedha, Gordon Brown (sasa ni PM) na Mama Clare Short, Waziri wa Ushirikiano na Misaada ya Kimataifa, Mashirika ya Oxfam, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Shirika la Kimataifa la Usalama wa Anga (ICAO), Jane’s Air Traffic Control na wengine, wote waliweza kubainisha mapema juu ya udanganyifu wa mkataba huo, kiasi kwamba Benki ya Dunia ikatishia kuzuia misaada kwa Tanzania.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, alijua yote haya; lakini aliishinikiza Kabineti yake imruhusu kutoa kibali cha mauzo kwa BAE Systems ili kuokoa ajira za Waingereza 280 wa Kampuni hiyo, iliyopo katika kisiwa cha Isle of Weight, ili Chama chake kisipoteze ushindi katika jimbo lililohusika. Rais Mkapa alipeleka salaam kwa Blair, kumshukuru kwa kuweza kuifanya Serikali yake iidhinishe mauzo ya mtambo huo mbovu chini ya mkataba wa kitapeli.

Juni 21, 2002 Waziri wetu wa Fedha wa wakati ule, Basil Pesambili Mramba, katika kauli iliyoonekana kutowakilisha maslahi ya Taifa, alitamka Bungeni maneno yafuatayo ambayo itawachukua Watanzania muda mrefu kuyasahau: “Tunakataa kuambiwa mambo yakufanya hata kama sisi ni masikini … Wanawezaje kuwa na ujasiri wa kutuambia kwamba rada hiyo ni aghali sana kwetu?... Tuko tayari kula majani, na kama wanataka, waache kutupa misaada yao”.

Kuonyesha kwamba hoja za wananchi hazikuwa na uzito kwake, Mramba, kwa wakati tofauti, alisema: “Baadhi ya watu wanaokota okota maneno baa na kuyafanya wimbo rada … rada … rada kwa kujisumbua; hawajui kwamba Serikali ya Uingereza imekwishatoa leseni ya kuiuzia Tanzania rada; na kinachotokea Uingerza sasa ni mgogoro ndani ya Serikali ya huko ambayo wanataka kuuleta katika Serikali ya Tanzania”.

Mramba na wenzake waliilewa vizuri Kampuni ya BAE Systems na malengo yake; kwani wakati huo ilikuwa imekumbwa na kashfa ya madai ya kutoa rushwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, baada ya nchi hiyo kutiliana sahihi mkataba wa kampuni hiyo kuiuzia silaha za kijeshi. Na kufuatia upelelezi wa SFO, kama inavyofanya hapa kwetu kwa sakata la rada, ilibainika kuwa BAE Systems, iliweka Pauni za Kingereza milioni saba katika Akaunti ya Mifuko (Trusts) huko Jersey, katika Visiwa vya Channel, na kutokana na uchunguzi zilimilikiwa na Waziri huyo.

Baada ya kuonekana mambo yanamwendea vibaya, Waziri huyo aliutema mfupa, akalipa Pauni milioni sita kwa mamlaka za utawala wa visiwa hivyo kama fidia ya usumbufu walioupata kutokana na upelelezi huo, na kwa maelewano ya kusimamishwa kwa upelelezi.

Kwa kufanya hivyo, inaweza kutafsiriwa kuwa, ama Waziri huyo alikuwa anautema mlungula kwa nafsi yake kumsuta, au naye alikuwa anatoa rushwa ili upelelezi usitishwe.

Hakuna shaka yoyote sasa kwamba wabeba mikoba ya ufisadi wa rada ya Tanzania, wanafahamika kwa mujibu wa taarifa ya SFO kwamba: “There is every reasonable cause to believe that all the above named persons and Company have committed offences of corruption …. The SFO concludes to believe that in taking this stance….. (name/s) was putting the economic interest of Tanzania at risk”, ni maneno ambayo tafsiri yake tumeitoa hapo mwanzo.

Je, kwa taarifa hii ya SFO, wahusika wa kashfa ya rada nao sasa wanaweza kuitema milungula kama alivyofanya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar; au watazuia wasiwajibishwe, au Sheria kuchukua mkondo wake, kwa nguvu ya fedha walizo nazo? Hivi ni mpaka SFO waje Tanzania ndipo tubaini vitendo vya ufisadi vyenye kuangamiza uchumi wa nchi yetu?

Source: www.raiamwema.co.tz

Monday, March 30, 2009

GDSS this week 01-04-2009

Gender and Development Seminar Series

You are invited to the weekly Gender and Development Seminar Series session in which GDSS discussion will focus on the;


Will The new Budget Work for women?A Feminist Critique of the Budget 2009/10-2011/12

Date: 1 April, 2009

Time: 3:00 pm - 5:00 pm

Venue: TGNP Grounds / Adj.NIT

Please confirm your participation through
info@tgnp.org


Come One Come All !!!!!!

Friday, March 27, 2009

Mrejesho wa GDSS: Tathimini ya Kampeni ya Maji; Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea.

Jumatano ya tarehe 25/03/2009, katika kuadhimisha wiki ya maji (16/03 – 22/03), semina za GDSS walifanya tathimini ya kampeni ya maji ambayo ilizinduliwa mwaka 2005 kufuatiwa na sera ya ubinafsishwaji wa maji. Lengo la tathimini hiyo ilikuwa ni kuangalia kampeni hiyo iliyokuwa ikiongozwa na TGNP, FemAct, na wanaharakati wengine imefikia wapi mpaka sasa. Muwasilishaji wa mada hii alikuwa ni Badi Darusi (KWYDP). Mwezeshaji aliweza kueleza Chimbuko, Mafanikio na Changamoto zilizotokana na utekelezaji wa kampeni hiyo.

Chimbuko la kampeni ya maji ya mwaka 2005 ilikuwa ni sera ya mpya ya Ubinafsishaji wa maji ambayo ilishinikizwa na IMF/WB kwa serikali za nchi masikini kama masharti ya kupatiwa mikopo/misaada. Sera hiyo ambayo ilitaka kutambua maji kama bidhaa zingine na iuzwe kama huduma zingine zinavyouzwa, ilipelekea wanaharakati waanzishe kampeni ya kupinga sera hiyo na kuishinikia serikali iachane na mipango hiyo ya kuuza maji kwa raia wake. Kauli mbinu ya kampeni hii ilikuwa ni “Maji Sio Bidhaa, Maji ni Uhai”

Ahadi za Rais wa Nne katika Kampeni za uongozi, ambaye aliahidi 65% ya wananchi kupata maji ndani ya mita 30 ifikapo mwaka 2010 ilichochea wanaharakati kuwa na kampeni hii ili kuweza kufanya tathimini ya hali ya maji nchini. Katika Kampeni hii wanaharakati walikuwa na madai saba ambayo ni;

1. Maji yatambulike kama haki muhimu ya binadamu.
2. Haki za kimataifa ziweze kutambua mchango wa wanawake katika utafutaji wa maji.
3. Kupinga shinikizo la IMF na WB kwa serikali la kubinafisha sekta ya maji.
4. Kuwepo na mjadala wa kitaifa kuhusiana na swala zima la maji.
5. Ongezeko la Bajeti ya Maji.
6. Uchangiaji wa huduma ya maji usitishwe.
7. Kuwa na wizara ya maji inayojitegemea.

Mwaka 2005/06 TGNP na wanachama wa GDSS walifanya utafiti katika baadhi ya maeneo ya Mabibo, Kigogo, Kisarawe, Mwanayamala, Salasala, Tabata, na Kiwalani. Utafiti ambao ulionyesha baadhi ya maeneo hayana miundo mbinu ya maji, ama iliyopo ni chakavu, ama haitoshelezi, wakazi kutegemea maji yanayouzwa katika magari, au kuchota umbali mrefu. Bado katika maeneo mengi wanawake ndio watafutaji wa maji na wanatumia muda na umbali mrefu kutafuta na kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Utafiti huo ulisaidia kutengenezwa kwa mpango kazi kwa vikundi vilivyoshiriki, ambapo walikubaliana yafuatayo; kufanya tafiti ndogondogo katika mitaa yao; kuangalia na kushirikiana na kamati za maji katika maeneo yao; kuandaa mikutano ya hadhara juu swala la maji ili kupata maoni ya wananchi; na kupeana mirejesho juu ya kinachoendelea katika maeneo mbalimbali mara kwa mara.

Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na;
Muingiliano wa Shughuli za maendeleo na siasa –kwa mfano, wenyeviti wa serikali za mitaa kutumia mikutano ya maji kujinadi; Uwiano usio sawa wa jinsia katika kamati za maji-ambapo kamati nyingi zina wanaume watupu; Ufinyu wa raslimali kwa vikundi vinavyofanya kampeni hizi; Ufinyu wa elimu ya ushawishi na utetezi kwa vikundi; Ushirikiano mdogo kati ya serikali za mitaa na vikundi vya wanaharakati; na kuwepo kwa mianya ya rushwa katika baadhi ya maofisa wa serikali za mitaa.

Tufanye nini?

• Tuchambue muongozo wa bajeti wa mwaka huu na kuangalia ni jinsi gani maji yalivyotengewa fedha na zitatumika vipi, wapi na kwa akina nani, ili tuweze kufanya kampeni mapema kushinikiza serikali kuongeza bajeti ya maji katika mwaka huu wa fedha wa 2009/10 kuhakikisha bidhaa hii adimu inawafikia walengwa.
• Wanaharakati wakae na kamati za maji za mitaa yao na waweze kuwafichua wahujumu wa maji katika mitaa yao kwa kupiga kura za siri ama njia yoyote itakayoleta mafanikio kuwafichua wahujumu wa maji.
• Wanaharakati wametakiwa kufanya vitendo vya utekelezaji na kuacha maneno mengi kama inavyoonekana sasa, hivyo wanapaswa kuchukua hatua katika maadhimio wanayofikia kila mara.

Kama wanaharakati tunashiriki vipi katika kuhakikisha Maji yanapatikana kwa wananchi wote na kwa urahisi?

Raza: Nchi imeoza

-Asema tatizo ni uongozi wa juu wa CCM
-Ashauri viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakae pembeni

ALIYEKUWA Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mohamed Raza, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘kimeoza’ katika safu ya uongozi wa juu.

Hata hivyo, Raza anasema pia kwamba CCM bado ni imara katika ngazi ya matawi na ameshauri kufanywa kwa mabadiliko ya uongozi, na kusisitiza viporo vya kashfa za ufisadi vikamilishwe kabla ya Uchaguzi Mkuu, mwakani, ili chama hicho kipate wepesi wa kujinadi kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, kada huyo machachari kutoka Zanzibar amesema ni busara zaidi vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ambao wanachunguzwa, lakini bado wakiendelea kushika madaraka ya juu katika CCM, waachie ngazi ili kukipa nguvu na heshima chama hicho mbele ya wapiga kura nchini.

Raza (pichani), aliyekuwa akimshauri aliyekuwa Rais wa SMZ, Dk. Salmin Amour Juma katika masuala ya michezo, alitoa msimamo na ushauri wake huo katika mahojiano maalumu na Raia Mwema, wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam, huku akiweka bayana kuwa tegemeo pekee la wananchi kwa sasa katika kulinda maslahi yao ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Huko CCM juu watu wakae kitako, umaarufu wa mtu unatokana na chama na si mtu. Huko ndiko kumeharibika. Nafasi ipo watu wazoefu pia wapo, sasa warekebishe huko juu,” alisema Raza bila kutaja ni nafasi gani za juu zilizopwaya katika kukiongoza chama hicho kikongwe nchini.

Hata hivyo, alidokeza kwa namna nyingine akisema ; “Mimi nafikiri mfano huu wa Dowans, Bunge limetoa ushauri wake suala hili liachwe, ofisa waandamizi wametoka wanataka kununua Dowans, lakini tayari Richmond imetokana na Dowans.

“Hadi Spika wa Bunge, ambaye ni mwana-CCM anatoka kusisitiza ushauri anasema hapana sasa wote hawa wanaovutana ni CCM hakuna Chadema wala CUF. Kwa hiyo tatizo lipo katika uongozi wa juu wa CCM.

“Kuna mbunge anamwambia mbunge mwenzake wa CCM…bwana hapo ulipofika tulizana kuna mambo nikizungumza patakuwa hatari nchi inaweza kuingia katika zahma. Sasa hii ni one system, hakuna Chadema, CUF wala TLP. Kwa hiyo katika hali hiyo tatizo lipo na kama tatizo lipo tusilifungie macho tu.

“…kama Tanzania kungelikuwa na upinzani bora, imara na wa kweli CCM isingelibakia…believe me, kama tungelikuwa na upinzani uliokuwa wa ujasiri loo! Kwa hivyo tushukuru kwamba CCM, chama changu, hatuna upinzani, lakini CCM tunajivunia tunakubalika kwenye grass root wanatukubali na wanaendelea kutukubali,” anasema katika mahojiano hayo yatakayochapishwa katika toleo la wiki ijayo.

Kwa upande mwingine aliwageukia waandishi wa habari nchini akisema; “Nataka kuwasihi waandishi wa habari, bora wale mhogo na viazi, lakini waweke mbele nchi yao. Bora wale mhogo lakini wajiamulie mambo yao kwa maslahi ya Taifa. Nasi Watanzania bora tule mhogo na viazi, lakini tujiamulie mambo yetu wenyewe.”

Lakini pia anawazungumzia viongozi waandamizi serikalini na wananchi akisema; “Mtu anakuja anakwambia mimi natoa milioni 600 au 700 katika uchaguzi…huyu ana lake…atakuumiza. Nilisema mimi katika uchaguzi mwaka 2005, nendeni mkasome magazeti, nilisema bwana hizi pesa zinazotoka hawa wanatakiwa kuja kuzilipa na watakapoanza kuzilipa watakuwa wana-command sasa leo ndiyo haya.”

Anashauri wana-CCM wenzake na hasa viongozi kwamba ni vema ufumbuzi wa viporo vya ufisadi ukapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Kwa sababu tunataka kurudi kwa wananchi najua kuna mambo ya Mahakama huwezi kuingilia, lakini katika yale mambo ambayo unaweza kuyafanya mapema, tuyakamilishe kabla ya kuingia katika uchaguzi,” anasema.

Katika mahojiano hayo, Raza anaonekana kuwashangaa viongozi wa Serikali wanaolalamikia watendaji wanaovujisha siri za Serikali.

Katika kuwashangaa anasema; “Leo mimi nashangaa viongozi na watendaji wengine wanalalamika siri zinavuja. Hivi unachota bilioni 100, mimi pango na ada ya mtoto sina, sehemu nyingine za nchi hakuna huduma ya maji, shule nyingine hazina madawati. Watoto wanakaa chini, mbavu zinawauma; wewe unachota mabilioni halafu unalalama siri zinavuja?!”

“Mtu sasa utakuta kazikusanya kwa ubinafsi wake mabilioni kwa mabilioni ya shilingi; huku wananchi wakiwa na umasikini, wanahitaji huduma za msingi za maji, umeme na barabara. Halafu tunasema Tanzania ni nchi masikini, ndiyo…sawa nchi masikini lakini sisi wenyewe tunajisimamia vipi?”, anahoji.

Katika kuthibitisha imani aliyokuwa nayo kwa Bunge, Raza anasema; “Kama si Bunge, nchi ingekuwa pabaya sana…nafikiri watendaji kama wanataka kuvaa kanzu nzuri basi hiyo fulana yao ya ndani waioshe isitoe harufu, lakini usivae kanzu una fulana inatoa harufu ndani au unavaa koti shati yako inatoa harufu ndani. Kwa hiyo kama unataka kuvaa kanzu basi fulana yako isafishe na kama ni suti pia shati yako isafishwe.”

Source: www.raiamwema.co.tz

Mkanganyiko Kura za Albino Mwanza

ZOEZI la kupiga kura za maoni kuwabaini watu wanaojihusisha na mauaji ya walemavu wa ngozi (albino) na vikongwe lililofanyika Machi 10 mwaka huu, kwa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, huenda lisisaidie katika kudhibiti mauaji hayo.

Hali hiyo inatokana na mwitiko mdogo wa wananchi hasa maeneo ya mijini ambako kuna vituo ambavyo havikupata kabisa wapiga kura. Zoezi hilo ambalo lilianza saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni lilipangwa kufanyika siku moja lakini kama wananchi wangejitokeza kwa wingi, lingeendelea siku inayofuata.

Hata hivyo, vituo vingi vilikamilisha zoezi hilo na kufungwa hata kabla ya muda huo kufika. Kudorora kwa zoezi hilo hususan maeneo ya mijini, kulifanya uzinduzi wake uliokuwa ufanywe na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. James Msekela uchelewe kutokana na watu wachache kujitokeza katika kituo cha Shule ya Msingi Mwenge.

Dk. Msekela anakiri kwamba watu katika maeneo ya mijini walijotokeza wachache lakini vijijini, hasa kwenye maeneo ambayo kuna mauaji ya maalbino na vikongwe, watu wengi walijitokeza.

“Ni kweli turnout hasa maeneo ya mijini haikuwa nzuri labda ni kwa vile hata mauaji ya vikongwe na maalbino pia ni kidogo. Sana sana watakuwa wanapigia kura majambazi na madawa ya kulevya. Lakini kule vijijini watu walikuwa wengi. Kuna mahali waliishiwa mpaka karatasi za kura ikabidi tuwaongeze”,” alisema Dk. Msekela.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa anasema kuwa tathmini ya zoezi hilo bado inaendelea kufanyika kwa kila wilaya na kwamba baada ya tathmini hiyo kukamilika ndipo itajulikana kama zoezi limefanikiwa au la.

“Tulipeana siku saba za tathmini ambazo ziliisha Jumanne iliyopita lakini zoezi hilo ni kubwa kidogo hivyo huenda wakaendelea. Unajua upigaji kura ulikuwa wa hiari hivyo kila mtu alikuwa na uhuru wa kwenda kupiga au kutokwenda”, aliongeza.

Mkoa wa Mwanza ambao unaongoza kwa mauaji ya vikongwe na albino, ulitarajia kuwa asilimia 40 ya wakazi wake watapiga kura hiyo.

Wananchi walitakiwa kupiga kura za siri katika maeneo manne ambayo ni mauaji ya albino, vikongwe, madawa ya kulevya pamoja ujambazi. Kutojitokeza huko kwa wananchi kunatokana na uhamaishaji mdogo uliofanyika na uoga wa baadhi ya watu.

Kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo hapakuwapo na kampeni ya kutosha kuhamasisha wananchi pamoja na kuwaelimisha juu ya zoezi hilo .

Ofisa mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa wananchi wengi walikuwa hajui kuhusu zoezi hilo na hata wale wachache waliojua, walifahamu kupitia vyombo vya habari.

“Hapakuwa na maandalizi ya kutosha ukilinganisha na unyeti wa zoezi lenyewe. Ukitaka mwananchi akupe taarifa nyeti kama hizi lazima umwandae kwa kumwelimisha na kumhamasisha vya kutosha, jambo ambalo halikufanyika zaidi ya kuwatumia viongozi wa serikali za mitaa,” alisema ofisa huyo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaona kuwa zoezi hilo huenda lisisaidie sana katika kudhibiti mauaji ya albino na vikongwe ambayo yameshamiri katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Hata kama ukitaja fulani anahusika ni vigumu kumchukulia hatua za kisheria. Pia zinaweza kuwa zimepigwa kura za chuki au labda watu kadhaa wanamhisi fulani kuwa ni jambazi lakini wanampigia kura kuwa ni muaji wa maalbino au vikongwe,” anasema John Shija.

Anaongeza kuwa Serikali lazima iwe makini, vinginevyo itakuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu iwapo watamchukulia mtu hatua za kisheria kwa kupigiwa kura hizo za maoni.

Mwanasheria mmoja wa Serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa ni vigumu kumfungulia mtu mashitaka kutokana na kupigiwa kura za maoni na wananchi.

“Kisheria ni vigumu kupata ushahidi wa kuithibitishia Mahakama (beyond reasonable doubt) kwa kutumia tu kura za maoni, tena za siri. Hivi hao mashahidi watatoka wapi wakati hizo kura ni za siri?, alihoji.

Kauli hiyo ya mwanasheria inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, ambaye amewahi kukaririwa kuwa pamoja na kuunga mkono kura hiyo ya maoni hadhani kama itasaidia kuwakamata wahusika wa mauaji hayo na kuwachukulia hatua za kisheria.

Alihoji Kapole: “Iwapo watu wamekamatwa wakiwa na viungo vya albino (ushahidi wa kutosha) lakini hadi leo hatujawahi kusikia mtu kafungwa itakuaje kwa aliyepigiwa kura tu?”.

Baadhi ya wananchi pia wanaona kama kufanyika kwa zoezi hilo ni kielelezo cha vyombo vya usalama nchini kushindwa kufanya kazi yake.

Lakini ofisa mmoja wa polisi amesema kuwa taarifa hizo ni muhimu kiitelijensia na kwamba zitasaidia katika mapambano dhidi ya mauaji ya maalbino, vikongwe pamoja na uhalifu mwingine.

“Kwetu sisi (vyombo vya usalama) hizi taarifa za wananchi ni muhimu na zitatusaidia sana . Unajua bila taarifa ni vigumu kupambana na uhalifu wowote na wenye hizi taarifa ni wananchi wenyewe ndiyo maana tunahimiza ulinzi shirikishi au polisi jamii,” alisema.

Hata hivyo tayari Chama cha Maalbino nchini (TAS) kwa kushirikiana na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu, na Shirika la Under-the Same Sun, wamefungua kesi dhidi ya Serikali wakidai imeshindwa kulinda maisha yao .

Katika shauri hilo la kikatiba, mashirika hayo, yanatumia ibara ya 12, 14, 18(2),na 29(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazotamka haki ya kuishi, kutambuliwa, kuheshimiwa, kupata na kutoa habari pamoja na kulindwa kisheria.

Wakili wa LHRC Clarence Kipobota, anasema wanamlalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa kukiuka haki za binadamu.

Kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahusu kushindwa kutoa taarifa rasmi kwa walalamikaji na kwa umma, kuhusu mwenendo wa mauaji ya maalbino.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inalalamikiwa kwa kushindwa kulinda heshima na maisha ya walemavu hao wa ngozi.

Wakili huyo anaongeza kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inalalamikiwa kwa kutopatikana kwa kinga ya ngozi za maalbino katika vituo vyake vya afya, ambayo ingewasaidia dhidi ya kansa ya ngozi.

Aidha, Kipobota anasema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inalalamikiwa kwa kushindwa kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya maalbino, kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi.

Kutokana na malalamiko hayo, na kwa mujibu wa wakili Kipobota wanaiomba Mahakama itoe tamko kwa Serikali kukubali kushindwa kuwalinda na kuwaheshimu, kutoa taarifa kwa walalamikaji na kwa umma kuhusu mwenendo wa mauaji ya maalbino, na kuitaka kutoa tamko la kuwafidia walioathiriwa na mauaji hayo.

Mengine ni kutoa tamko la kupatikana kwa kinga ya ngozi za maalbino katika vituo vya afya, kukubali kutunga sheria zitakazowawezesha wao, na wengine wenye ulemavu kufurahia haki zao za kikatiba.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizindua upigaji kura za siri, kuwabaini wanaojihusisha na mauaji ya hayo, ili wachukuliwe hatua za kisheria. Kura hizo zinapigwa kikanda.

Shehena kubwa ya almasi yazuiwa



-Ni ya mgodi wa Williamson, Shinyanga
-Kisa ni hali tete ya kuuzwa kwa mgodi

SHEHENA ya almasi inayotajwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 4.5 (zaidi ya Sh bilioni 4.5) iliyopo katika Mgodi wa Almasi wa Wiliamson, uliopo eneo la Maganzo, mkoani Shinyanga, imezuiwa kuuzwa.

Hatua ya kuzuiwa kwa shehena hiyo kuuzwa inatokana na hali tete iliyopo baada ya kuuzwa kwa mgodi huo uliokuwa chini ya kampuni ya kimataifa ya Willcroft, iliyokuwa na ubia na Serikali, kupitia kampuni yake ya De Beers.

Kamishna wa Madini nchini, Dk. Peter Kafumu, amethibitisha kuhusu kuzuiwa kwa kwa shehena hiyo ya almasi na kusema kwamba uamuzi huo umetokana na mchakato wa kuhamisha umiliki wa mgodi huo baada ya shughuli za kampuni ya Wilcroft kupitia De Beers kuuzwa kwa kampuni ya Petra Diamonds.

Alisema kutokana na hatua hiyo, Serikali imezuia kwa muda uuzwaji wa almasi katika mgodi huo ili kupisha mchakato mpya wa maelewano baada ya shughuli za mgodi huo kuuzwa.

Dk. Kafumu pia alikiri kuzuiwa kwa karati 45,000 za almasi zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.5. Thamani hiyo imetokana na bei ya soko kuwa dola za Marekani milioni 100 kwa kila karati moja.

“Kinachofanyika sasa ni kuendelea kwa mchakato wa maelewano baada ya mabadiliko ya mbia kati ya Serikali na mwekezaji. Kama unavyojua serikali ina hisa asilimia 25 na mbia asilimia 75,” anasema Dk. Kafumu.

Katika uendeshaji wa mgodi huo, Serikali ilikuwa na hisa asilimia 25 wakati kampuni hiyo kwa kutumia kampuni ya De Beers, ikiwa na hisa asilimia 75.

Kwa sasa shughuli za mgodi huo zimeuzwa kwa kampuni ya Petra Diamonds kutoka Willcroft, kwa dola za Marekani milioni 10, katika uuzaji ambao unatajwa kutoipatia nchi mapato yaliyostahili, yakiwamo ya ushuru (Stamp Duty).

“Kimsingi migodi yote iliyofanya mabadiliko (kuuziana), Serikali imekuwa haipati fedha yoyote, kumbuka mgodi wa North Mara wa kampuni ya Placer Dome ya Canada kutoka kwa kampuni ya Afrika Mashariki ya Australia, na baadaye mgodi huo kuwa mikononi mwa Barrick ya Canada,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Inaelezwa kuwa katika mgodi wa Williamson, licha ya Serikali kuwa na hisa asilimia 25, tangu mwaka 1994, imekuwa haina mwakilishi wake kwa upande wa uendeshaji hadi Mei, mwaka jana, na badala yake uwakilishi wa Serikali ulikuwa katika ngazi ya bodi ya wakurugenzi tu.

Habari zaidi zinaeleza kuwa katika kipindi hicho mgodi huo kupitia De Beers, umekuwa ukikopa fedha zilizofikia Dola za Marekani milioni 100 (zaidi ya sh bilioni 100), na kubwa zaidi imekuwa ikikopa fedha hizo kutoka kampuni ya Willcroft, ambayo ndiyo mama wa De Beers.

Mkopo umekuwa ukichukuliwa kwa awamu kwa madai kuwa mgodi umekuwa ukijiendesha kwa hasara, jambo ambalo ni vigumu kwa Serikali kuthibitisha kutokana na kutokuwa na mwakilishi wake katika uendeshaji.

“Kwa miaka kadhaa, De Beers wamekuwa wakidai kujiendesha kwa hasara, lakini wamekuwa wakiendelea kukopa. Mkopo sasa umefikia Dola za Marekani milioni 100. Inashangaza kuendelea kukopa huku ukilalamika kupata hasara.

“Mbali na De Beers kukopa kutoka katika kampuni yake mama ya Willcroft, pia iliweka masharti kwamba ni lazima almasi yote iuzwe katika kampuni yake nyingine ya DTC, hali ambayo watalaamu wanamini ni kuweka ukiritimba usio wa lazima.

“Kwa hiyo, De Beers ilikuwa ikieleza kuwa inapata hasara lakini ilikuwa ikikopa kutoka katika kampuni yake mama ya Willcroft lakini pia ilikuwa ikilazimisha almasi ziuzwe katika kampuni yake nyingine ya DTC. Wakati wote huu tangu mwaka 1994 hadi mwaka jana, Serikali haikuwa na mwakilishi katika shughuli za uendeshaji,” kinadokeza chanzo chetu cha habari.

‘Wazee wa Mbeya wana darubini za kutambua watu wanaotia mimba wanafunzi’

Darubini ni kifaa kinachotumika kutazamia vitu vilivyo mbali. Lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kifaa hicho kimekuwa kikitumika kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo shughuli za kisayansi, kivita na hata kutazama vitu vilivyopo angani, kama vile mwezi, jua na nyota. Darubini ya kwanza inayojulikana, ilitengenezwa mwaka 1608 na Mholanzi Hans Lipperhey, aliyekuwa fundi miwani.

Mfano wake ulichukuliwa na kuboreshwa na raia wa Italia, Galileo Galilei, aliyeanza kuitumia mwaka 1610 kwa kuangalia nyota. Darubini ziliendelea kuboreshwa katika karne zilizofuata. Mtambo mpya ulipatikana katika Karne ya 20, kwa kutumia mnunurisho wa sumaku umeme kutoka nyota, iliyoendelezwa kuwa darubini redio.

Lakini, nchi za Magharibi zikiwa zimepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, nchini Tanzania, hususani wilaya ya Mbeya, baadhi ya wazee wa mila kupitia kamati zao za ufundi, wanazo darubini zinazowawezesha kutambua watu wanaowapa mimba wanafunzi, wezi na wapiga nondo.

Hivi karibuni wazee wa mila wa kabila la Wasafwa, wakiwemo Machifu na Mamwene, waliitisha mkutano uliomshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, uliokuwa una lengo la kujadili masuala mbalimbali, ikiwamo kudhibiti mimba za wanafunzi, mauaji ya albino na wapiga nondo, ulinzi kwa viongozi wa ngazi ya wilaya hadi Taifa na kuomba Serikali iwatambue.

Mwenyekiti wa Mila wa Wilaya ya Mbeya (Mwene Mkuu), Shao Soja Masoko, anasema wazee wa mila wanakerwa na vitendo vya wanaume kuwapa mimba wanafunzi na kisha kukana mimba hizo. Anasema hali hiyo imesababisha wasichana wengi wakatishe masomo, hivyo kuwa chanzo cha watoto hao kushindwa kupata elimu.

Anasema wazee wa mila, wana uwezo wa kukabiliana na tatizo la wanafunzi kupata mimba, kwa kuwapa adhabu wanaume wanaowapa mimba wanafunzi. Adhabu hiyo itakuwa ni fundisho kwa wanaume wote; na watakaogopa kuwagusa wanafunzi, kwa kuwa madhara ya kufanya hivyo, yatakuwa yanaeleweka.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunachoomba serikali ya mkoa itupatie kibali cha kuwadhibiti watu wanaowapa mimba wanafunzi na kukana kuwa na uhusiano na wasichana hao, kwa kuwapa adhabu ya kuwahamishia mimba hizo katika matumbo yao na wasichana kuendelea na masomo kama kawaida,” anasema. Anasema mimba kwa wanafunzi imekuwa ni kero kubwa katika jamii.

Anasema kwamba badala ya serikali kuendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu nchini, sasa inalazimika kukabiliana na mimba kwa wanafunzi na utoro, mambo yanayopaswa kudhibitiwa na wananchi wenyewe katika maeneo wanayoishi. Anaomba serikali iwape kibali cha kudhibiti mimba, kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

"Machifu na Mamwene tuna darubini zetu, tuna uwezo wa kuona mbali. Ukitupa kibali tunaweza kuwadhibiti wanaowapa mimba wanafunzi, kwa kuzihamishia mimba hizo kwao na mwanafunzi kuendelea na masomo salama salimini, huku akiwa si mjamzito tena," anasema na kuongeza kuwa hilo litakuwa fundisho kwa wengine.

Chifu Roketi Mwashinga anasema wazee wa mila, wana uwezo wa kusaidia shughuli mbalimbali katika jamii, ikiwamo kudhibiti watu waovu. Hata hivyo, anasema kuwa serikali imewasahau na kuwatenga, hali inayosababisha washindwe kutoa ushirikiano, hata pale wanaposhuhudia maovu yanatendeka mbele yao.

Anasema miaka ya nyuma walikuwa wakishirikishwa, lakini hivi sasa hawashirikishwi katika mambo mbalimbali, hali inayofanya wasiheshimike katika jamii na hivyo kutopewa nafasi. "Tukishirikishwa, tunaweza kusaidiana na viongozi wa serikali, lakini kama tutaendelea kubaguliwa, basi hatutakuwa na la kufanya," anasema. Wanaiomba serikali iwatambue na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali.

Anasema kutofuatiliwa kwa wahamiaji wageni katika mitaa na kudharauliwa kwa wazee wa mila, ndio chanzo cha kuongezeka kwa vitendo viovu katika jamii, ikiwamo mauaji ya albino na raia wema kushambuliwa kwa kupigwa nondo na kunyang'anywa mali walizonazo. Anasema kukithiri kwa vitendo viovu katika jamii, kunachangiwa na Serikali kutowathamini wazee wa mila na kuwashirikisha katika kudhibiti vitendo hivyo.

Anasema kupitia darubini zao, wazee wa mila wanaweza kuwadhibiti wanaofanya vitendo hivyo, kwa kuwafanya wawe vichaa au wajipeleke wenyewe katika vituo vya polisi na kujieleza. Hata hivyo, anasema tabia ya baadhi ya polisi kushindwa kutunza siri, zinazotolewa na raia wema, imekuwa ni kikwazo kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo. Anaitaka Serikali kuwadhibiti askari wasio waaminifu ili maovu yadhibitiwe katika jamii.

"Kama serikali itakuwa tayari kushirikiana na sisi, tunakuomba wewe na sisi tuongozane katika operesheni ya kukamata wapiga nondo kutoka eneo moja hadi jingine. Kwa kutumia kamati zetu za ufundi, wote watapatikana na wengine watajipeleka wao wenyewe katika vituo vya polisi, wakiwa na viungo vya binadamu na kuanza kutoa maelezo wao wenyewe bila kuhojiwa," anasema.

Akizungumzia mauaji ya albino, anasema ili vitendo hivyo vidhibitiwe, ni lazima serikali ishirikiane na waganga wa kienyeji. "Ukitaka kumkamata mwizi ni lazima umtumie mwizi mwenzake," anasema. Anaongeza kuwa waganga wa jadi, ndio wanaoweza kusaidia kukomesha mauaji ya albino.

Mwashinga anaitaka serikali, kuangalia upya utaratibu wa usajili wa waganga wa kienyeji. Anasema utafiti wao wamebaini kuwa waganga wanaohusika na mauaji hayo, wengi wanatoka nje ya mkoa wa Mbeya, sanjari na wapiga nondo. Anawataka machifu na mamwene, kuwaonya watoto wao wasijihusishe na vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Jadi Mkoa wa Mbeya, Jeiko Ngurunguru, anasema waganga wanaotuma watu wakaue albino, si waganga wa jadi, bali ni wanamazingaombwe na matapeli wanaotoka nje ya Mkoa wa Mbeya. Anasema ikiwa serikali itahakikisha kuwa waganga wasio na vibali, hawaruhusiwi kufanya shughuli za tiba asili, mauaji hayo yatadhibitiwa.

Anasema uganga ni jambo la kurithi na waganga wa kweli, wanafahamika katika jamii na historia yao inafahamika, wanafanya kazi kwa uwazi na pale wanawatumia dawa za asili katika kutoa tiba na si vinginevyo. Hata hivyo, anasema hivi sasa yameibuka makundi ya wanamazingaombwe na wapiga ramli, ambao wanawadanganya wananchi na kufanya vitendo vingi viovu katika jamii.

“Hawa ni sawa na wanaokula nyama za watu, mganga wa kweli utatumaje mtu akaue binadamu mwenzake, hawa si waganga, hakuna mganga anayeweza kumwambia mtu akanajisi watoto, akaue vikongwe,” anasema. Anaongeza kuwa kuwafumbia macho wapiga ramli, ipo hatari kwa vitendo viovu kuendelea kuongezeka katika jamii. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, anasema jeshi la polisi limekuwa likiboreshwa kiutendaji.

Anasema kwamba wananchi wanatakiwa kutoa taarifa za siri kwa viongozi wa jeshi hilo; na zitafanyiwa kazi kwa haraka; na mwananchi aliyetoa siri, hatatajwa popote pale. Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mbeya, John Mwakipesile, anawapongeza mamwene na machifu, kwa kuanzisha umoja wao, ambapo anasema serikali inawatambua na kwamba inaelewa mchango wao katika shughuli za maendeleo.

"Serikali haijasahau, inawatambua na inaelewa mchango wenu katika shughuli za maendeleo," anasema. Mwakipesile anasema Serikali itaendelea kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na viongozi wa kitaifa, wanaotembelea Mkoa wa Mbeya kwa ziara za kikazi. Baadhi ya wananchi wanasema teknolojia hiyo ya kuhamishia mimba, itakuwa ya kwanza na ya aina yake kutokea duniani.

Solomoni Mwansele anasema kuwa ikiwa jambo hilo ni la kweli; na ikatokea kweli mwanaume akahamishiwa mimba kwa njia za kimaajabu na wazee hao wa mila, Tanzania inaweza kuushangaza ulimwengu. Anasema ubunifu huo, unaweza kusaidia kukabiliana na mimba za wanafunzi. Brandy Nelson anasema kuwa Serikali haiamini katika masuala ya ushirikina na ni ndoto kwa serikali kutoa kibali kama hicho.

“Siamini kama kinachoongelewa kinawezekana, wapo watoto wa machifu na wazee wa mila wanapata mimba, lakini hatujawahi kushuhudia wakiwa wamewahamishia mimba wanaume waliowapa mimba watoto wao,” anasema. Anahoji kwa nini wazee hao wa mila, waibuke leo wakati tatizo la mimba limepigiwa kelele kwa muda mrefu?

Mnasemaje wanaharakati kuhusu hili?

Wednesday, March 25, 2009

Mauaji ya Albino:Kura ndio ufumbuzi wa matatizo yetu?

ZOEZI la upigaji kura ili ‘kuwachagua’ wanaoshukiwa kuhusika na vitendo vya mauaji ya albino lilizinduliwa kwa ving’ora kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, wiki iliyopita. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndiye alikuwa mgeni wa heshima aliyeliza king’ora katika uzinduzi huo.

Kwa kawaida katika shughuli zinazohusu upigaji kura, tulitegemea kumuona mgeni wa heshima akitumbukiza kura yake kwenye sanduku la kupigia kura kama ishara ya ufunguzi wa zoezi hilo, lakini badala yake tukaonyeshwa akibonyeza kitufe cha king’ora.

Naamini ingeleta uzito zaidi iwapo mgeni wetu wa heshima angeonyeshwa akitumbukiza kura yake kwenye sanduku hata kama kura yenyewe ingekuwa haijaandikwa kitu kuashiria kuwa hamfahamu yoyote anayeshukiwa kuhusika na biashara hiyo haramu!

Nimejiuliza pia juu ya uamuzi wa kufanyia uzinduzi wa zoezi la kupiga kura jijini Dar es Salaam badala ya mji wowote wa Kanda ya Ziwa ambako mauaji ya maalbino yamekithiri kwa kiwango cha kutisha. Ni uamuzi ambao pengine ungeongeza hamasa ya wananchi wa maeneo hayo yaliyokithiri kwa vitendo hivyo kushiriki kikamilifu zoezi hilo.

Hilo pembeni, tumeambiwa kwamba kura hiyo ambayo ina vipengele vinne itasaidia kubainisha wale wote wanaohusika na uovu wa kuua albino kwa ajili ya viungo vyao. Vipengele vingine vya kura hiyo ni pamoja na kuwataja wanaoua vikongwe, majambazi na pia wauzaji madawa ya kulevya.

Pengine hapa tunapaswa kujiuliza kama kweli tupo serious na tatizo hili. Kwa nini kura ya maoni ya kuwatambua wanaohusika na mauaji ya ndugu zetu maalibino na wazee wetu ichanganywe na kura ya kuwatambua majambazi na wauza dawa za kulevya ambao majina yao tayari yapo mpaka ofisi ya juu kabisa ya nchi na hayajafanyiwa kazi?

Tunatoa picha gani hapa kwa ndugu zetu maalbino? Kwamba mwisho wa siku orodha ya watakaotajwa kuhusika na kuwaua haitashughulikiwa kama ambavyo hazijashughulikiwa orodha za majambazi na wauza madawa ya kulevya ambazo zimefungiwa kwenye makabati na watuhumiwa kupewa muda wa kujirekebisha?

Kwa hakika, kipengele cha kuwataja wauza madawa ya kulevya kitaongeza tu idadi ya watuhumiwa ambao tayari wako kwenye orodha mbali mbali ambazo viongozi wetu wamekaririwa mara kadhaa wakisema kuwa wanazo.

Sio vibaya iwapo wakati watu wanapiga kura kuongeza idadi hiyo, viongozi wetu nao wakaanza kuipunguza kwa kushughulikia yale majina yaliyomo tayari kwenye orodha ambazo wao wenyewe wamekiri mara kadhaa kuwa wanazo!

Hilo ni moja, lakini pia nimejiuliza sana iwapo kuna Juhudi zozote zimefanyika ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wamepata elimu ya kutosha kuhusiana na zoezi hili kabla halijazinduliwa rasmi.

Tukumbuke kwamba wengi wa wananchi wetu tunaotegemea wapige kura kuwataja wanaohusika na mauaji ya albino, ndio hao hao ambao hupata tabu hata wakati wa kupiga kura muhimu zaidi ya kuchagua viongozi wao.

Je, wananchi wetu hawa wamepata elimu na muda wa kutosha wa kujiandaa na zoezi hili ambalo kwa hakika, kwa namna moja ama nyingine, limekuja kwa namna ya ‘ghafla bin vuu’?

Sio nia yangu kubeza juhudi zinazofanywa ili kuhakikisha kuwa ndugu zetu maalibino wanaishi kwa amani kwenye nchi yao wenyewe kama ilivyo kwa raia wengine, lakini ni lazima niseme wazi kuwa nina wasiwasi sana kama zoezi hili litaleta matokeo yanayotarajiwa.

Kuna maswali kadhaa ya kawaida kabisa ambayo yanataka majibu. Je, kwa kututaka wananchi tupige kura ya maoni ‘kuchagua’ wale tunaodhani kuwa wanahusika na ushenzi huu, ndio kusema kuwa vyombo vyetu vya usalama vimeshindwa kuwaona na kwa maana hiyo kutaka msaada kutoka kwa wananchi?

Je, zoezi hili likijumlishwa na ile kauli ya ‘jino kwa jino’ iliyopata kutolewa na Pinda ya kutaka wanaoua ndugu zetu maalibino nao wauawe, ichukuliwe kama ushahidi kwamba vyombo vyetu vya usalama vimeshindwa kazi na hivyo kuurudisha kwetu mzigo wa kuwatafuta wahalifu hawa wanaowaua maalbino?

Kama tunakubaliana kwamba kila mwananchi wetu ni mlinzi wa nchi yetu na anawajibika kutoa taarifa kuhusu uhalifu wowote, ni kitu gani kinachowafanya wananchi wetu wasifanye hivyo kwa hiyari yao wenyewe mpaka tuzindue zoezi la kupiga kura ya maoni kuwataja watuhumiwa ambao wanawafahamu siku nyingi? Tatizo ni nini?

Je, zoezi hili na kauli ya Pinda ni ushahidi kwamba viongozi wetu sasa hawajui cha kufanya kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili, na matokeo yake kuwa haya ya kuwa wafa maji wanaokumbatia hata nyasi katika juhudi zao za kujiokoa wasizame?

Kwa utaratibu huu wa kupiga kura za maoni ili kuwapata wanaohusika na mauaji ya albino, je huko mbele ya safari tutegemee rundo la mazoezi ya kupiga kura za maoni kubaini wezi wa mitihani ya taifa, makampuni ya mabasi yanayoongoza kwa kusababisha ajali, viongozi wenye shahada feki na kadhalika!?

Niko tayari kukosolewa, lakini nina uhakika kwamba hakuna sheria ya nchi inayosema kuwa kuna mhalifu anaweza kutiwa hatiani kutokana na ‘kuchaguliwa’ na kura za maoni za wananchi wenzake.

Hii ina maana kwamba baada ya kupiga kura majina yatakayopatikana yatarudishwa tena kwenye vyombo vyetu vya usalama ambavyo vitalazimika kufanya tena uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao ili kupata ushahidi unaotosha kuwasimamisha kizimbani!

Mwisho wa yote tunajikuta tumerudi tena kule kule. Ni vyombo vyetu hivi hivi vya usalama ambavyo hadi leo hii vimeshindwa kungurumisha angalau kesi moja tu ya wahalifu wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya albino, halafu leo tunatakiwa kupiga kura ili kuwaongezea mzigo mwingine wa majina ya mabazazi tunaowashuku!

Nakubaliana na kauli ya Mkurugenzi wa Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu Tanzania (SHIJAWATA), Christopher Andelekisye aliyotoa siku ya uzinduzi wa zoezi la kupiga kura za kuwatambua wanaohusika na mauaji ya maalibino.

Mkurugenzi huyu alionekana kutofautiana na Waziri Mkuu kwa kusema kuwa zoezi hilo halitakuwa na tija iwapo mwenendo wa kesi za wauaji wa maalbino hautabadilishwa.

Mkurugenzi huyo alishauri kuwepo kwa marekebisho ya sheria ya uchawi na ile ya adhabu (penal code). Sheria iliyopo na ambayo tumerithi kutoka kwa wakoloni inapinga kuwepo kwa uchawi.

Ni kweli kwamba mpaka sasa hakuna sheria tofauti kwa ajili ya kesi zinazohusu mauaji ya albino. Zinaendeshwa kama zinavyoendeshwa kesi za mauaji ya mtu mwingine yoyote.

Labda tungeazia hapo; kwamba Bunge na asasi za serikali zinazohusika zitunge na kupitisha sheria maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi zinazohusu mauaji ya albino, ikiwezekana hata kuanzisha vitengo maalumu kwenye mahakama na ofisi za waendesha mashitaka wa serikali kwa ajili ya hilo.

Lakini wakati tukisubiri hilo, tunaweza kuamua kuwa kesi yoyote inayohusu mauaji ya albino ni priority. Aidha, yanapotokea mauaji hayo, polisi wa eneo husika waruhusiwe kuweka pembeni uchunguzi wa mauaji mengine yoyote waliokuwa wakiendelea nayo ili kushughulikia yale ya albino.

Kwa hatua hizi, tunaweza tukafika mahali tukagundua ni nani anayesababisha kesi za mauji ya albino kusuasua na tukamchukulia hatua zinazostahili, mbali ya kwamba tutafika mahali tukajikuta hatulazimiki kupoteza muda kupiga kura ya ‘kuwachagua’ watuhumiwa wa mauaji ya ndugu zetu.

Tuesday, March 24, 2009

Mkutano wa IMF-Afrika: Rais Kikwete utatanishi mtupu


KWANZA nawaomba radhi wapenzi wasomaji wa safu hii kwa kutokuandika kwa muda mrefu kwa sababu ya kutingwa na majukumu binafsi.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete alikuwa mwenyeji wa mkutano wa IMF-Afrika, uliohudhuriwa na Rais wa Shirika la Fedha Duniani, Dominique Strauss-Kahn, mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Mkutano huo, pamoja na mambo mengine, ulijadili mikakati ya kukinga uchumi wa nchi za Afrika dhidi ya mgogoro wa kifedha uliosababishwa na mtikisiko wa uchumi duniani.

Mshiriki Jeffrey Sachs alitoa kauli kwamba utawala wa Washington katika uchumi wa dunia (Washington consensus), umefika kikomo. Mwandishi wa CNN, Isha Sesay aliwataka washiriki walioamini kauli hiyo wanyooshe mikono. Rais Kikwete alinyoosha mkono kuashiria kwamba anakubaliana na kauli hiyo. Waziri wa fedha na uchumi, Mustafa Mkullo hakunyoosha mkono.

Ili kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani, mkutano uliazimia kuwa sekta binafsi katika Afrika inahitaji fursa nzuri ya uwekezaji ili ichukuwe nafasi ya injini kubwa katika kukuza uchumi. Katika msukosuko wa namna hii wa kiuchumi duniani, Isha Sesay alitaka kujua Rais Kikwete anafanya nini ambacho ni tofauti ili kuvutia wawekezaji katika sekta binafsi?
Kwa ufupi, Rais Kikwete alijibu kuwa anaendeleza sera na mipango ileile iliyokuwapo.

Hakika mtikisiko wa uchumi duniani umewaacha viongozi wetu katika njia panda. Natatanishwa na imani ya Rais Kikwete kuwa Washington hawatatawala tena uchumi wa dunia, lakini wakati huo huo hana mipango na sera mpya zaidi ya kuendeleza zilezile zilizotungwa Washington!

Na kama sera zilizotungwa Washington ndizo zilizoutikisa uchumi wa dunia, kwa nini tuziendeleze? Je, sera zinazoutikisa uchumi imara wa Marekani, hazitauzika kabisa uchumi wetu mahututi?

Utatanishi wa namna hii umeibua maswali mengi kichwani mwangu. Je tumetoka wapi, tupo wapi sasa hivi na kwa nini? Je, Washington ni akina nani? Wametoka wapi na wapo wapi sasa hivi? Lengo langu ni kuchokoza mjadala ili tuweze kupata mwanga wa wapi tunakwenda. Katika waraka wa leo na wiki ijayo nitajadili kwa ufupi maswali yote haya.

Tangu mwaka 1967 mpaka 1992, mwongozo na dira ya Serikali ya Tanzania ilikuwa ni Azimio la Arusha. Liligawanyika katika sehemu tano, lakini zinazohusu mada hii ni tatu; Ujamaa, Kujitegemea na Maadili ya viongozi.

Chini ya Ujamaa, njia kuu za uchumi zilimilikiwa na umma. Nguzo kubwa ya uchumi ilikuwa ni wawekezaji ambao walikuwa ni umma. Makampuni na mabenki yalimilikiwa na umma chini ya uendeshaji na usimamizi wa serikali. Yalipopata faida, yalilipa kodi serikalini na salio lilikuwa la umma ambalo lilitumika, ama kukuza mtaji wa biashara katika kampuni na benki husika au katika huduma za jamii kama elimu na afya. Hasara iliyopatikana ilikuwa ni ya umma pia.

Hii ni tofauti na nchi za kibepari ambapo chanzo cha mapato serikalini ni kwa njia ya kutoza kodi tu, kwa sababu faida au hasara siyo ya umma, bali ni ya wanahisa au wamiliki binafsi wa makampuni na mabenki.

Siasa ya kujitegemea ilitahadharisha suala la mikopo, kwa hoja kwamba kuwabebesha watu masikini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Kwamba “haiwezekani kutegemea nchi za nje na kampuni za nje kwa misaada, mikopo na rasilimali kwa maendeleo ya Watanzania bila kuhatarisha uhuru wa Tanzania. Haikuamini dhana ya wageni kumiliki uchumi wa Tanzania kwa ajili ya kupata faida kupeleka nchini kwao.

Maendeleo huletwa na watu hayaletwi na fedha. Fedha ni matokeo siyo msingi wa maendeleo na unyonge wa Mtanzania usingeweza kuondolewa na fedha kutoka nje bali kutoka kwa Watanzania wenyewe.

Masharti ya maendeleo yalikuwa juhudi na maarifa. Na ili kuendelea walihitajika watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora” (kitabu cha Azimio la Arusha).

Kimaadili, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa mashirika ya kiserikali, madiwani na watumishi wa serikali waliokuwa na vyeo vya kati na juu, hawakuruhusiwa kuwa na hisa katika kampuni yoyote. Hawakutakiwa kuwa na mishahara miwili au zaidi na hawakuruhusiwa kuwa wakurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.

Ingawa ilikuwapo mipango na maazimio na mikakati ya muda mfupi kama vile; Azimio la Musoma lililohimiza umuhimu wa Watanzania wote kupata elimu, msisitizo ulilenga kukuza maarifa ya ufundi na sayansi na Azimio la Iringa la kilimo cha kufa na kupona.

Ardhi ya Tanzania ni kubwa yenye udongo wenye rutuba, hivyo kilimo kilikuwa uti wa mgongo. Mikakati ya muda mrefu iliwekwa katika ujenzi wa viwanda vya mazao ya biashara na zana za kilimo.

Mifano michache ni viwanda vya majani ya chai, kahawa, nguo, pareto, mkonge, bia, sigara, sukari na zana za kilimo. Viwanda vingine vilihusu bidhaa muhimu kama sabuni, saruji na kiwanda cha kusindika nyama cha Kawe.

Ilianzishwa benki ya taifa ya biashara (NBC) iliyokuwa na matawi mpaka vijijini. Nyingine ni Benki ya Nyumba (THB) na Posta (TPB). Pia, yalianzishwa mashirika mbalimbali ya umma kama Shirika la Ndege (ATC) na Shirika Bima la Taifa (NIC).

Misingi hii ya uchumi iliiwezesha serikali kugharamia elimu kuanzia chekechea, kisomo cha watu wazima, msingi, sekondari mpaka chuo kikuu. Wanafunzi wote walipatiwa huduma za afya, chakula, nauli, na fedha ya kujikimu. Shule zote za serikali zilikuwa na vifaa vya mahabara na nyenzo muhimu za kufundishia.

Walimu, wauguzi na madaktari walilipwa mishahara yao. Serikali iliweza kununua madawa kwa ajili ya dispensari mashuleni, vijijini na mahospitalini.

Misingi ya uchumi wa Tanzania ilianza kujaribiwa na dhoruba kutoka ndani na nje ya nchi. Mfano, Mwaka 1973 kulikuwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya petroli duniani. Gharama za uzalishaji zilipanda na thamani ya shilingi iliathiriwa.

Kuanzia 1973 mpaka mwishoni mwa 1974 ulitokea ukame uliosababisha upungufu wa chakula. Na mwaka 1977 jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika na hivyo Serikali kulazimika kugharamia huduma zilizotolewa na jumuiya hiyo.

Aidha kuanzia 1978 mpaka 1979 Tanzania ilipigana vita dhidi ya majeshi ya Iddi Amin wa Uganda. Vita hiyo, kwa kiasi kikubwa, iligharamiwa na Tanzania.

Matukio haya katika ujumla wake yaliutikisa uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa. Bidhaa muhimu kama sukari, unga wa ngano, mahindi, na vifaa vya ujenzi kama mabati na simenti, viliadimika. Ili kulinda wananchi wasio na uwezo, Serikali iliingilia mgao wa chakula na mafuta ya petroli kwa kutoa vibali.

Baadhi ya watendaji serikalini na wafanyabiashara wachache walitumia mpango wa vibali kulangua bidhaa na kuziuza kwa magendo. Serikali ilitangaza vita dhidi wahujumu uchumi iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine (Mungu airehemu roho yake).

Kumwagia tindikali kwenye kidonda, hata uzalishaji katika viwanda ulianza kudhoofika, na ufanisi katika uendeshaji wa mashirika na mabenki ulianza kulegalega.

Viwanda, mabenki na mashirika mengi ya umma yalianza kuwa msalaba kwa serikali kwa sababu yalikuwa yanaendeshwa kwa hasara wakati yakipokea ruzuku kutoka serikalini. Hali hii ilisababishwa na mambo mengi, lakini baadhi ni uzembe, wizi na ubadhilifu wa mali ya umma. Mashirika kuendeshwa kisiasa badala ya kibiashara, kwa sababu wakurugenzi wengi walikuwa ni wanasiasa bila kuwa na ujuzi wa kuendesha shirika.

Halikadhalika utamaduni wa kuwazawadia na kuwalea vihiyo, wabadhirifu, na wazembe uliharakisha msambaratiko wa mashirika mengi. Mfano, mkurugenzi aliyevurunda shirika moja alihamishiwa shirika jingine bila kuadhibiwa.

Kuanzia katikati ya kipindi cha awamu ya pili mwaka 1985, serikali ilikuwa na uhaba mkubwa wa fedha za kujiendesha, kulipa madeni yaliyojenga baadhi ya viwanda na kutoa huduma muhimu kwa jamii.

Katika kipindi hicho, hali ya kisiasa duniani ilikuwa imebadilika. Vita baridi kati ya Urusi na Marekani, ambayo ilizitesa na kuzinufaisha baadhi ya nchi ilikwisha kumalizika. Katika vita hiyo, mabepari walitoka vifua mbele.

Kwa bahati mbaya, ni wakati huo huo, ambapo serikali ya Tanzania na nchi nyingine ambazo uchumi wake ulikuwa taabani, zilikimbilia Washington kuomba fedha kama zawadi au mikopo.

Je, huko Washington kuna akina nani? Hasa zinazoumiza kichwa ni asasi kubwa mbili za fedha. Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB). Hizi asasi zilianzishwa 1944 mjini Bretton Woods, New Hampshire (Marekani) na ndiyo maana zinaitwa Bretton Woods System.

Mataifa 44 waanzilishi waliunda taasisi hizo ili waweze kupata mikopo ya muda mfupi baada ya kuathiriwa vibaya na vita kuu ya pili ya dunia.

Dhumuni la mikopo lilikuwa kuyajenga upya mataifa yao yaliyokuwa yamebomolewa na vita. Wakati huo hayakuwapo makundi ya nchi za dunia ya kwanza na nchi za dunia ya tatu au nchi masikini kama ilivyo sasa. Zilikuwapo dola kubwa ambazo zilitawala maeneo makubwa duniani.

Kwa hiyo, hizi taasisi ambazo ni kubwa kwa sasa hazikuundwa na jumuia ya kimataifa. Ziliundwa kwa maslahi ya wale waliozianzisha.

Mathalani, muundo wa Shirika la Fedha Duniani bado unayapa nguvu mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi. Kura ya kila taifa inategemea na ukubwa wa uchumi wake. Marekani bado inaongoza kwa kuwa na zaidi ya asilimia 17 ya kura zote, ikifuatiwa na Japan na Ujerumani.

Kikatiba, ili kuathiri maamuzi ya IMF, kubadili muundo au sera zake, kunahitaji asilimia 80 ya kura zote. Hata hivyo, Marekani na nchi za ulaya peke yake zina zaidi ya asilimia 80 ya kura zote.

Idadi ya wanachama wa IMF imeongezeka kutoka 44 tangu ianzishwe mpaka 185 sasa hivi. Uchumi wa Afrika ni takriban asilimia mbili ya uchumi wa dunia. Kwa hiyo, pamoja na ongezeko hilo la wanachama, na kutokana na kanuni za IMF, hata mataifa yote masikini duniani yakiungananisha kura zao, hayawezi kubadilisha sera au masharti ya hili shirika. Kubadili kitu chochote ndani ya IMF lazima kwanza upate baraka za mataifa makubwa.

Je, uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania ulipotikiswa, Washington walitoa ushauri gani kwa serikali kuhusu kilimo, mashirika ya umma, mfumo wa biashara, utoaji wa huduma muhimu kwa jamii kama elimu na afya? Je ushauri huo ulikuja na dira?

Na je, uti wa mgongo wa uchumi wa nchi za Magharibi ulipotikiswa, walikimbilia IFM kwa ushauri? Je, wanatekeleza waliyoishauri serikali ya Tanzania au wameiacha kwenye mataa kwa kutenda waliyotukataza?


Mfano, mabenki, viwanda vya magari, shirika kubwa la bima la Marekani yaliposhindwa kujiendesha, serikali ilifanya nini?

Je, Rais Barrack Obama ana mipango gani kuhusu elimu, afya na sheria mpya ya maadili kwa viongozi na watumishi wa serikali?

Kwa hiyo katika mkutano huo wa IMF-Afrika uliofanyika Dar es Salaam, watawala wetu Tanzania hawakuwa na jipya. Lakini yote tisa, kumi ni kitendo cha mpigania haki za kisiasa, Bob Geldof kutoa karipio na kumkatisha Rais Kikwete wakati anazungumza. Je, Kwa nini Bob Geldof hakukanywa? Ni kwa sababu ya ugeni, rangi, au utajiri wake?

Mbona baadhi ya wazee waliostaafu wanapotoa ushauri kama huo huo tena kwa lugha ya kistaarabu, wanaambiwa kwamba wanatolea ushauri vijiweni? Je ni kwa sababu ya rangi, uenyeji, au umasikini wao? Matendo haya yanalinda heshima na utu wetu?

Mafisadi kuamua nani awe rais 2010?



-Mbunge wa CCM asema nchi iko rehani
MBUNGE wa Kishapu, Fred Mpendazoe, amesema kutokana na matajiri mafisadi kuachwa wakitamba watakavyo, zipo dalili za wazi sasa kwamba wamejipanga kuamua nani awe rais wa nchi, mbunge, waziri na hata diwani; wakipora jukumu hilo kutoka kwa wananchi.

Akionyesha kukerwa na mwenendo wa mambo na hasa kuimarika kwa matabaka miongoni mwa wananchi, mbunge huyo amesema mafisadi hao wameweka mizizi yao ndani ya serikali, na nchi inaelekea kuwekwa rehani kwao.

“Kinachofanyika sasa kinazidi kutoa harufu ya ufisadi kwenye serikali. Upo msemo wa kisambaa unaosema kama unataka kuepuka nzi tupa kibudu cha mzoga. Kama Serikali inataka kuepuka harufu ya ufisadi, ishughulikie vyanzo vya ufisadi na iviondoe la sivyo itaendelea kuandamwa na kashfa,” anasema Mpendazoe katika mahojiano na gazeti hili ambayo yamechapishwa kwa kina.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, tatizo kubwa linaloitafuna serikali ya sasa ni uteuzi kufanyika katika misingi ya urafiki; hali inayowakwaza wenye mamlaka ya kuteua na hatimaye kushindwa kuwawajibisha wateule pale wanaposhindwa kutimiza wajibu wao.

“Upo msemo kwamba A friend in power is a friend lost; yaani rafiki yako akipata madaraka na dhamana kubwa ya kuongoza anakoma kuwa rafiki,” anasema na kufafanua kuwa;

“Anakoma kuwa rafiki yako ili aweze kutekeleza majukumu yake bila kuwa na upendeleo wowote. Nchi nyingi zinazoendelea zina tatizo hili. Mtu anapopata madaraka utakuta anaweka rafiki zake kwenye sehemu nyeti akidhani watamsaidia kumbe huwa ni kinyume chake.”

Akizungumzia kuhusu nchi kuwekwa rehani, mbunge huyo alisema ni jambo hatari sana, “maana yake serikali itaongozwa na matajiri na hivyo haitawajibika tena kwa wananchi na demokrasia itakoma na udikteta utaanza.

“Serikali haitakuwa ya watu na kwa maana hiyo haitachaguliwa na watu na haitawajibika kwa wananchi. Matajiri wataamua nani awe rais, nani wawe wabunge kwenye majimbo,” anasema na kuongeza kuwa;

“Wananchi hawatachagua madiwani wanaowataka. Baadaye matajiri wataamua nani awe waziri, jaji na wakuu wa vyombo vya dola ili kuhakikisha maslahi yao yanalindwa sehemu zote kwa mwavuli wa maslahi ya Taifa.

Na zipo dalili za kuelekea huko. Serikali inapochelewa kuchukua hatua haraka juu ya ufisadi unaotendeka si dalili nzuri.”

Katika kushauri nini kifanyike, mbunge huyo alisema; “Mfumo wa utawala tulionao unaotokana na Katiba hautoi fursa kwa watendaji kuwajibishana bali unatoa nafasi kubwa ya kulindana.

Ni mfumo wa viongozi kulindana badala ya kuwajibishana inapobidi.”

Akiweka wazi msimamo wake kuhusu sakata la ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans, na hususan kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, mbunge huyo alimshauri waziri huyo kuwasilisha hoja yenye malalamiko yake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ili yajadiliwe.

Katika hatua nyingine, alitonya kuwa kuna uwezakano wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu suala la Dowans, na alipoulizwa lini hatua hiyo inaweza kufanyika alijibu kwamba ni katika mkutano ujao wa Bunge.

Raia Mwema,18 Machi,2009.

Friday, March 20, 2009

Mrejesho wa GDSS- Elimu ya Mtoto wa Kike: Elimu ya Msingi Kanda ya Mashariki

Semina hii ilifanyika jumatano ya tarehe 18/03/2009 katika viwanja vya ofisi za TGNP Mabibo na kuhudhuriwa na washiriki kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani, na Dar es salaam pamoja na wanaharakati wengine walio katika sekta ya elimu nchini. Wawezashaji walikuwa ni Mama Shekilango na Rehema Mwaiteba(TENMET).

Mada ililenga kuangalia elimu kwa watoto wa kike katika mikoa mitatu ya kanda ya mashariki ambayo ni Dar es salaam, Morogoro, na Pwani. Watoa mada walitoa mrejesho wa utafiti uliofanywa na TENMET mwaka 2008 katika mikoa hiyo mitatu. Utafiti huo ulikuwa na Lengo la kujionea hali halisi ya elimu ya mtoto wa kike katika mikoa hiyo ili kuweza kubaini changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike katika kupata elimu ya msingi, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kampeni inayoendelea ya kumpatia elimu mtoto wa kike.

Utafiti huo ulilenga kuangalia mambo makuu manne katika elimu ya wasichana ambayo ni; upatikanaji wa elimu(accesibility), kuendelea na masomo(continuation, kupanda darasa moja hadi lingine(transition), na kumaliza kwa elimu ya msingi(completion). Katika maeneo hayo manne yameonyesha bado kuna upungufu mkubwa, kwa mfano upatikanaji wa elimu bado ni wa tabu katika maeneo mengi yaliyofanyiwa utafiti-mf; shule nyingi za serikali hazina vyoo, vitabu ama walimu wa kutosha hivyo elimu inayopatikana haitoshelezi. Pia wasichana wengi wameshindwa kumaliza/kuendelea na shule kutokana na vikwazo kama utoro, mimba, kuzidiwa na kazi za nyumbani hasa za kutafuta kipato na kutunza wagonjwa, nk.

Michango kutoka kwa washiriki ni pamoja na;

• Bado kuna upungufu wa shule za awali-chekechekea serikali hajaweka shule hizi za awali ingawa sera inasema kwamba kila shule ya msingi ni lazima iwe na vyumba vya madarasa ya awali, lakini maeneo mengi bado yanaonyesha hayana madarasa hayo. Shule za awali za binafsi zipo lakini wananchi wengi wa hali ya chini wameshindwa kupeleka watoto wao katika shule hizo.

• Upatikanaji wa elimu bora unategeamea sana na mazingira ya shule, afya bora ya mwanafunzi, mwamko wa jamii husika juu ya elimu, utamaduni/mila potofu za jamii kuhusu kumsomesha mtoto wa kike, hali ya uwezo wa familia husika, na mahusiano ya walimu na wanafunzi, lakini kutokana na utafiti bado jamii yetu imeshindwa kutoa mazingira mazuri kama haya kwa ajili ya kuwapatia elimu watoto wa kike.

• Urasimu katika usajili wa shule za watu binafsi pia ulitajwa kama mojawapo ya chanzo cha upungufu wa shule za awali katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano mshiriki mmoja kutoka Morogoro alisema, Morogoro kuna shule zaidi ya 40 za awali ambazo zinasubiri usajili, hali imesababisha upungufu wa shule hizi.

Nini Kifanyike
• Wanaharakati waishinikize serikali isifunge shule za bweni kwa kushindwa kuwalipa wazabuni wa chakula. Serikali inapaswa kutoa elimu kwa raia wake wote bila kubagua, ili waje kulitumikia taifa lao. Serikali inapaswa kuwalipa haraka wazabuni hao na kuendeleza shule hizo za bweni kama awali.

• Wanaharakati walipendekeza kianzishwe kitengo cha ushauri kwa watoto wa kike katika shule za watu binafsi na serikali ili kiwasaidie wasichana wanapopata matatizo wanapokuwa shuleni, na pia waweze kupata elimu ya kujisitiri wanapokuwepo mashuleni.

• Wanaharakati waishinikize serikali iongeze bajeti ya wizara ya elimu kutoka 18% ya mwaka jana, na kuangalia upya mgawanyo wa fedha hizo ili nyingi zitumike katika maendeleo ya elimu nchini.

• Jamii inapaswa ielimishwe umuhimu wa kumuelimisha mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kujisomea pindi awapo nyumbani, pamoja na kumpunguzia kazi ambazo zinawezwa kufanywa hata na wavulana mf. kuteka maji, kufua, usafi wa mazingira nk.

• Wanaharakati watoe tamko la pamoja juu ya jambo hili, ikiwa na pamoja na kulipeleka jambo hili katika majukwaa mengine ya wanaharakati kama breakfast debate za policy forum nk.

• Nafasi za Halmashauri ziweke bayana katika kuimarisha elimu ya msingi nchini hasa elimu ya wasichana. Kwa sasa halmashauri ndizo zinazosimamia shule za msingi nchini lakini zimeshindwa kuleta maendeleo husika katika sekta hiyo.

Semina hiyo ilifungwa na kuacha majukumu ya ufuatiliaji kwa wanaharakati, ambapo maadhimio hayo yalitakiwa kutolewa mrejesho kwa wanaharakati katika siku za usoni.

Ukiwa kama mwanaharakati na mdau wa elimu kataka nchi yetu, unafanya nini ili kuhakikisha elimu ya msingi kwa watoto wa kike inaboreshwa?

Wednesday, March 18, 2009

ATCL yaomba kustaafisha 70

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepeleka serikalini mchanganuo wa maombi ya fedha kwa ajili ya kustaafisha kwa maslahi ya umma wafanyakazi wapatao 70 wa kampuni hiyo, kutokana na kuelemewa kiutendaji kwa idadi kubwa ya wafanyakazi.

ATCL yenye wafanyakazi 300 ina jumla ya ndege tano na mbili kati ya hizo aina ya Bombadia Dash 8 zenye uwezo wa kubeba abiria 50 ndizo zinazofanya kazi kwa sasa, jambo lililoelezwa kutowiana na uwezo wa gharama za uendeshaji.

Mchanganuo huo utakapokubalika serikalini, utahusu wafanyakazi wenye umri mkubwa, wanaokaribia kustaafu, wasio na taaluma yoyote na wakatisha tiketi, watu wa mapokezi bila kugusa wataalamu, wakiwamo marubani na wahandisi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ATCL, Balozi Mustafa Nyang’anyi alisema leo bila kutaja kiasi walichoomba serikalini, kuwa tayari wamewasilisha mchanganuo wa fedha zinazohitajika kwa kazi hiyo na kwamba wanasubiri na kuwa habari zilizoandikwa juzi na gazeti moja la kila siku (si HabariLeo) kuwa wanapeleka likizo na kustaafisha wafanyakazi takriban 150, si za kweli.

“Hakuna mazungumzo wala hatua yoyote iliyofikiwa ya kupeleka watu likizo bila malipo na hatua ya kustaafisha watu ni kwa maslahi ya umma na si ya sasa, maana inahitaji fedha nyingi, hatujui Serikali itatoa fedha lini, pengine mwaka ujao wa fedha,” alisema Balozi Nyang’anyi.

Kwa upande wake, kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU), tawi la ATCL, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alithibitisha kufanyika vikao vya mchakato wa kupunguza wafanyakazi kwa kuwastaafisha na kukazia kuwa mpango wa likizo bila malipo walishaukataa na endapo ukiibuliwa, watagoma upya.

Mwishoni mwa mwaka jana, ATCL ilipata msukosuko baada ya kunyang’anywa leseni ya kurusha ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kutokana na kubainika dosari katika nyaraka muhimu na baada ya kufunguliwa, ilipewa na Serikali Sh bilioni 4.5 za uendeshaji, lakini ulizuka mzozo baada ya menejimenti kuwatangazia wafanyakazi kuwa watapewa likizo bila malipo, kutokana na uhaba wa fedha.

Baada ya suala hilo kufutiliwa mbali kwa vikao vya ndani vya kampuni, Bodi na wafanyakazi, hivi sasa Serikali ipo katika mazungumzo na kampuni ya China iitwayo China Sonangol International Limited (CSIL) kwa ajili ya kuingia nayo ubia baada ya kuvunja mkataba na Kampuni ya Afrika Kusini (SAA) miaka mitatu iliyopita kutokana na kubaini hali ya kampuni hiyo kuwa hatarini.

Tuesday, March 17, 2009

Hii ni demokrasia inayopanuka

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha uamuzi kuwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani sasa watakuwa wakipigiwa kura za maoni na kila mwanachama, badala ya utaratibu wa zamani uliokuwa ukiwaruhusu wajumbe wachache kushiriki kupitia mikutano mikuu ya majimbo.

Kwamba, utaratibu mpya unatoa nafasi kwa kila mwanachama wa chama hicho kupiga kura katika tawi lake na hivyo kuwa vigumu kwa wagombea kuwahonga wanachama katika matawi yote katika jimbo husika.

Sambamba na uamuzi huo, CCM pia imepitisha uamuzi wa kuongeza uwakilishi wa wanawake katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, ili idadi ya wanawake katika vyombo hivyo iwe asilimia 50 ya wabunge au wawakilishi wote wanaochaguliwa.

Tunachukua fursa hii kupongeza uamuzi huo uliofanywa na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kwa sababu ni njia mojawapo ya kuziba mianya ya rushwa ambayo ilikuwa ikitumiwa na baadhi ya wagombea kuwarubuni wapiga kura, kwa kuwa walikuwa wachache na walikuwa wakipatikana kwenye eneo mmoja.

Kitendo cha kuwakutanisha wanachama wachache wa CCM kwenye mkutano mmoja wa jimbo kilikuwa kinatoa fursa miongoni mwa wagombea kutoa fedha kwa urahisi na hivyo kuifinya demokrasia ya kupata viongozi bora na waadilifu.

Utaratibu huo mpya pia unapanua demokrasia kwa kuwashirikisha watu wengi zaidi katika kupiga kura za maoni na hivyo kupanua nafasi ya kila mwanachama kumchagua kiongozi anayemtaka, badala ya utaratibu wa kuwakilishwa kwenye mikutano ya majimbo, ambako wanachama wenye uchu na fedha walirubuniwa kwa urahisi.

Lakini pia tunachukua fursa hii kupongeza juhudi za kuongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya kutunga sheria kufikia asilimia 50 ya wabunge, wawakilishi na madiwani. Hii pia ni hatua nzuri ya kupanua demokrasia na kuongeza sauti za wanawake katika vyombo hivyo vya wananchi.

Jambo la msingi ni kwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupokea mapendekezo ya CCM ili kurekebisha katiba za pande hizo mbili na sheria zake za uchaguzi, mapema iwezekanavyo, ili mabadiliko hayo yaweze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao, tupate safu nzuri za viongozi.

Tunachukua nafasi hii pia kuvishauri vyama vingine vya siasa kuwa na taratibu za wazi za kupanua demokrasia kwa kushirikisha wanachama wao wengi zaidi katika michakato ya kupata viongozi wa vyama na hata wabunge, wawakilishi na madiwani.

Ni kwa njia hii sisi kama nchi tutakuwa na haki ya kujivunia mifumo yetu ya kupata wawakilishi wa wananchi na hata viongozi katika ngazi mbali mbali nchini.

Katika haya yote, yu wapi Kikwete?

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete aliwajia juu viongozi wa zamani wanaoikosoa serikali yake “vijiweni”.

Ingawa hakutaja majina ya viongozi hao, ni dhahiri alikuwa akiwazungumzia kina Joseph Warioba, Cleopa Msuya, Joseph Butiku, Hassy Kitine, Bakari Mwapachu na wengine kadhaa ambao katika siku za karibuni walitumia haki yao ya kikatiba kuzungumzia namna nchi inavyoendeshwa.

Kwa kuamua kutumia neno “vijiweni” (wanaikosoa serikali ‘vijiweni’), Rais Kikwete alilenga katika kuwafanya Watanzania wawapuuze viongozi hao wastaafu, kwa sababu, kwa mtazamo wake, hawana hoja.

Je, Watanzania tunapaswa kukubaliana na Rais Kikwete kwamba viongozi hao wastaafu ni wa kuwapuuza? Je ni kweli hawana hoja katika kila walichokizungumzia, na kwamba ushauri wao si chochote wala lolote?

Sitaki kuzungumzia alichozungumzia Jenerali Ulimwengu, wiki iliyopita, kwamba watawala wetu wakishakamata madaraka hujaribu pia kuhodhi fikra na kujiona ni wao tu ndiyo wanaojua kila kitu; lakini napenda nikite katika kile kilichozungumzwa (‘kijiweni’?) na mmoja wa viongozi hao wa zamani ambao Rais Kikwete anataka tuwapuuze.

Namzungumzia Bakari Mwapachu ambaye ameitumikia Serikali ya Tanzania kama waziri kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Katika mahojiano na gazeti hili, Mwapachu alilalamika, miongoni mwa mambo mengine, kwamba mambo hayaendi vizuri kwa sababu tunatumia muda mwingi mno wa utendaji kwa kupiga domo!

Kwa hakika, kauli hiyo si mpya; kwani ilishapata kutolewa huko nyuma na Jaji Warioba ambaye alilalamika kuwa nchi sasa inaendeshwa kwa malumbano. Kwamba badala ya viongozi serikalini na katika chama tawala kushughulikia masuala ya kimsingi ya maendeleo, wamejikita katika kulumbana wenyewe kwa wenyewe.

Je, si kweli kwamba walichokisema Warioba na Mwapachu ni sahihi; hata kama walikisemea ‘vijiweni’? Na kama si sahihi, utayaelezeaje haya tunayoyaona yakiendelea hivi sasa katika mihimili mitatu ya dola; yaani Serikali, Mahakama na Bunge?

Nazungumzia malumbano kati ya Bunge na Serikali, Mahakama na Bunge, na hata kamati moja ya bunge dhidi ya kamati nyingine ya bunge ndani ya mhimili huo. Kwa hakika, hata mhimili wa nne (press) nao haujasalimika katika malumbano haya.

Tumefika mahali pa kutisha ambapo kamati mbili za bunge moja, chini ya spika mmoja, zinalumbana zenyewe kwa zenyewe hadharani; kama tulivyoshuhudia hivi karibuni katika sakata hili la ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans.

Tumefika mahali pa kutisha ambapo mhimili wa Mahakama unalumbana hadharani na mhimili wa Bunge kuhusu ni nani hasa championi wa kusimamia haki; huku kila upande ukitumia katiba kuhalalisha nguvu iliyonayo dhidi ya mwenzake.

Tumefika mahali hatari ambapo utendaji wa serikali unagubikwa na usanii; kiasi kwamba kauli zake sasa haziaminiki tena moja kwa moja.

Leo, Waziri (Ngeleja) atasema kamwe Serikali haitanunua mitambo chakavu ya Dowans, lakini kesho waziri huyo huyo atasema mitambo hiyo lazima inunuliwe!

Tumefika mahali Rais (Kikwete) anasema hakuna mwanafunzi wa chuo kikuu atakayeshindwa kusoma kwa sababu ya ukosefu wa ada, lakini miezi kadhaa baadaye watoto wa wakulima masikini wanatimuliwa vyuoni kwa sababu baba zao hawana fedha za kuchangia gharama za kuwasomesha!

Tumefika mahali mbunge kijana aliyekuwa championi wa kutetea sheria na haki (Zitto) katika kutetea hoja yake ya kunuuliwa mitambo chakavu ya Dowans anasema sheria ya manunuzi iliyopitishwa na bunge si msahafu, na hivyo isiwe kikwazo cha ununuzi huo!

Wakati (Zitto) akiyasema hayo, mbunge mwenzake (Dk. Mwakyembe) naye anajitokeza hadharani na kumjibu kwamba ni heri nchi ikae gizani kuliko kununua mitambo hiyo chakavu ya Dowans ambayo mpaka leo umma haujatajiwa mmiliki wake halisi!

Na katikati ya malumbano haya ya wabunge (Zitto vs Mwakyembe na Shelukindo) Spika wao, Samuel Sitta naye anajitokeza hadharani na kuungana na Shelukindo na Mwakyembe kwa kusema kwamba kama Serikali itanunua mitambo hiyo chakavu ya Dowans, itakiona cha moto bungeni!

Kauli hiyo bila shaka ndiyo iliyomchochea mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuliambia gazeti la Mtanzania, toleo la Jumamosi iliyopita,kwamba Sitta na Mwakyembe ni maadui wa CCM! Je, wanakuwa maadui wa chama chao kwa sababu tu ya kuishauri serikali iachane na mpango wa kununua mitambo chakavu ya Dowans (binamu wa Richmond, kwa mujibu wa Spika Sitta!)?

Katikati ya malumbano hayo, Ikulu ya Rais Kikwete ikatoa taarifa kuhusu kikao ambacho Rais alikifanya na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini; taarifa ambayo dhahiri inaonyesha kuwa hata Ikulu nayo imeingia katika malumbano hayo ya Dowans.

Aya “D” ya taarifa hiyo ya Machi 3, 2009, inasomeka hivi kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Rais Kikwete katika kikao hicho: “Ziongezwe juhudi katika uzalishaji wa umeme nchini kwa sababu programu ya taifa ya uzalishaji umeme bado iko nyuma na bado liko pengo kubwa katika mahitaji halisi ya umeme nchini na umeme unaozalishwa kwa sasa.”

Nayo aya “E” inasomeka hivi: “Dhana ya tenda na Sheria ya Manunuzi isiruhusiwe kuwa kikwazo katika miradi mikubwa mikubwa ya miundombinu ya nishati….”

Ukitafakari kwa makini aya “D” na aya “E” unaona wazi kwamba kauli ya Rais inafanana na iliyotolewa na Zitto Kabwe kwamba Sheria ya Manunuzi si msahafu. Kwa maneno mengine, kauli hiyo ya Rais inabariki kununuliwa kwa mitambo hiyo ya DOWANS; hata kama ni kuizunguka sheria ya nchi iliyopitishwa na Bunge.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Salva Rweyemamu alilumbana na gazeti la Mwananchi akidai kwamba taarifa yake haikugusia kabisa suala la Dowans. Ni kweli, lakini Mtanzania yeyote mwenye akili anajua kwamba aya “E” ya taarifa hiyo ilikuwa inalenga mitambo ya Dowans; vinginevyo ni manunuzi gani mengine yenye utata ambayo katika siku za karibuni yamehusishwa na Sheria ya Manunuzi kama si mitambo hiyo ya Dowans?

Au tuamini kwamba ilikuwa ni coincidence tu kwa Rais Kikwete kuitaja, hivi sasa, sheria hiyo ya manunuzi katikati ya mjadala huo wa Dowans? Kwa mtazamo wangu, ingekua vyema kama Rais Kikwete angelijitokeza wazi wazi na kueleza msimamo wa Serikali yake kuhusu manunuzi hayo ya mitambo chakavu ya Dowans, badala ya kuchomeka kijembe ambacho kinaendeleza tu malumbano. Ni nani asiyejua kuwa kauli ya Rais ni ya mwisho, na wala halazimiki kufuata ushauri wa Bunge?

Lakini funga-kazi katika sakata hili la mitambo ya Dowans ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Idriss Rashid aliyoitoa mwishoni mwa wiki. Yeye ameamua kuzira na kuitoa Tanesco katika mpango huo wa kununua mitambo hiyo. Amefanya hivyo si kwa hoja, bali kwa kuzira na kususa; huku akisema wananchi watajijua wenyewe nchi itakapogubikwa na giza!

Dk. Idriss aligoma kujibu maswali ya waandishi wa habari, na yalikuwa mengi ambayo mpaka leo hayana majibu – Ni nani mmiliki wa Dowans? Kwa nini Tanesco ing’ang’anie kununuliwa mitambo chakavu ya Dowans badala ya kuishauri serikali ianze mchakato wa haraka (fast track) wa kununua mipya?

Kutojibiwa kwa maswali hayo na mengine mengi kunajenga hisia kwamba kuna kitu ambacho Serikali inajaribu kuuficha umma, na hisia hizo ndizo zinazofanya malumbano haya yapambe moto; kama yalivyokuwa mengine huko nyuma.

Kwa ufupi, unaweza kuandika kitabu kizima kabisa cha jinsi Serikali ya Rais Kikwete ilivyotawaliwa na usanii na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005.

Nimezungumzia mifano hiyo michache ya karibuni ya malumbano, na sikutaka kabisa kuzungumzia mingine iliyopata kuibuka huko nyuma kuanzia ya Buzwagi, Bulyanhulu, Meremeta, Balali na EPA, Kagoda na EPA, Richmond, Kiwira, Majengo Pacha ya BOT, TICT, OIC, Vyuo Vikuu n.k

Kwa hiyo, Mwapachu anaposema tunapiga domo na kulumbana badala ya kukaa chini na kupanga mikakati ya kuendeleza nchi yetu na kuwapunguzia wananchi wetu umasikini, anachosema ni kweli kabisa; hata kama anakisemea ‘kijiweni.’

Kama yasingekuwa yanaathiri uchapaji kazi wa Serikali, pengine malumbano haya yangekuwa yanafurahisha, na kwa wengine ingekuwa ni burudani ya aina yake inayoonyesha kukomaa kwa demokrasia yetu na jinsi tunavyoheshimu uhuru wa kujieleza na kukosoana!

Lakini ukweli ni kwamba yameathiri mno utendaji wa Serikali. Vitu vya msingi vimewekwa pembeni; wakati usanii, malumbano na scheming za ki-mitandao zikiendelea!

Na mfano mzuri ni ziara ya ghafla ya Rais Kikwete ya hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam ambako alikuta maagizo yake aliyoyatoa miezi mitatu iliyopita hayajatekelezwa. Ni nani alipaswa kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Rais?

Bila shaka ni Waziri wa Miundombinu. Alikuwa wapi muda wote huo hadi Rais mwenyewe kulazimika kwenda, ni swali ambalo nawaachia wenyewe mjibu; kwani sote tunaijua nguvu ya ki-mtandao ya TICT katika bandari hiyo.

Liko suala hili jingine (kwa mfano) la matrekta ambayo tuliambiwa yataagizwa kwa pesa za EPA zilizorejeshwa na mafisadi. Je yameshanunuliwa? Na kama jibu ni ndiyo, ni matrekta mangapi? Utaratibu wa kuyapata ni upi? Bei itakuwa ni nafuu au itakuwa ni bei ya soko?

Hakuna mwenye majibu ya maswali haya ambayo, bila shaka, wakulima wangependa kuyajua. Hakuna majibu kwa sababu watawala wanaopaswa kutoa majibu hayo wako kwenye malumbano na scheming za ki-mtandao!

Chukua mfano mwingine. Mwanzoni mwa mwaka huu Rais alitembelea mkoa wa Mbeya. Alipofika Mbarali alisikitika baada ya kuona mwekezaji, aliyeuziwa kwa bei chee mashamba ya mpunga yaliyokuwa ya umma, ameamua kuyageuza kuwa ya kilimo cha mibono (jatrofa) badala ya mpunga kama mkataba unavyosema.

Kwa kujua wazi kwamba hatua hiyo itaathiri kiasi cha mpunga unaozalishwa mkoani Mbeya (hutoa asilimia 60 ya mpunga wote unaozalishwa nchini), Rais aliagiza mwekezaji huyo aache mara moja kulima mibono na kama hataki kulima mpunga, basi, mashamba hayo yarejeshwe tena kwa umma. Muda mrefu umeshapita tangu atoe agizo hilo, je hilo limefanyika?

Nina hakika agizo lile liliishia pale pale Mbarali; kwani wanaopaswa kulitekeleza wako bize na malumbano ya ufisadi na scheming za ki-mtandao!

Majuzi hapa, Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Strauss Khan alitahadharisha kwamba kipindi cha Nchi Zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, kuanza kuathirika na anguko la uchumi wa dunia kimewadia, na hivyo zianze kuwa makini. Alisema kwamba kuna awamu tatu za kuathirika – ilianza Marekani, zikafuatia nchi nyingine tajiri zilizoendelea, na sasa ni kipindi cha Nchi Zinazoendelea zikiwemo za Afrika.

Je, watawala wetu Tanzania wameisikia tahadhari hiyo ya Strauss Khan? Sitashangaa kama hawakuisikia; kwani wako bize na malumbano ya ufisadi na scheming za ki-mtandao!

Lakini swali kuu la kujiuliza ni hili: Katikati ya malumbano haya, mwenye kigoda (Rais Kikwete) kasimamia wapi? Ni muhimu kujiuliza swali hili kwa sababu Rais ana nguvu na mamlaka makubwa yanayomwezesha kukomesha mara moja malumbano haya na kuirejesha nchi katika mwelekeo sahihi.

Je, amejaribu kufanya hivyo? Siamini kama amejaribu kufanya hivyo; kwani hata kukemea tu hatujamsikia akikemea malumbano haya na scheming hizi za ki-mtandao ambazo zinaathiri utendaji wa serikali yake.

Binafsi, kuna wakati napata hisia kama vile anayafurahia malumbano haya na scheming hizi za ki-mtandao zinazoendelea ndani ya serikali, asasi za umma na ndani ya Bunge.

Nimalizie tafakuri yangu kwa kusema kwamba, mpaka hapo atakapowakemea watendaji wake kuacha malumbano haya na scheming hizi, na kuwahimiza watendaji wake warejee katika uchapaji kazi, hana uhalali wa kuwajia juu kina Warioba, Butiku, Msuya, Mwapachu, Kitine nk wanaojaribu kukemea hali hii inayotukwaza; hata kama wanakemea kwenye ‘vijiwe’.

Tafakari.

Raia Mwema,Machi 11, 2009

Friday, March 13, 2009

Mrejesho wa GDSS - Ukuaji wa Uchumi wa Tanzania Unamsaidiaje Mtu wa Chini?

Mrejesho wa Semina wa GDSS iliyofanyika jumatano ya tarehe 11/03/2009 katika ofisi za TGNP Mabibo. Mada ilikuwa ni Ukuaji wa Uchumi wa Tanzania Unamsaidiaje Mtu wa Chini? Mada hii ambayo ilikuwa na lengo la kuendeleza mjadala kuhusu zahama/mgogoro wa uchumi duniani na kufanya tathimini iwapo ukuaji wa Uchumi wa Tanzania unamnufaisha mwananchi wa hali ya chini, iliwakilishwa na Bubelwa Kaiza kutoka Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA).

MJADALA KWA UREFU.
Mtoa mada alitafsiri neno Uchumi ambapo alisema ni mahusiano yaliyopo kati ya mwananchi na shughuli za uzalishaji kwa kuangalia mambo yafuatayo.
i) Mapato/shughuli inayoleta ujira. Mfano: Kazi za kuajiriwa, Shughuli za kilimo na Biashara.
ii) Uwezo wa kununua. Mfano: Manunuzi ya bidhaa/ kupata huduma.
iii) Uwezo wa kuchagua bidhaa/ huduma husika.

Alisema, takwimu za IMF zinaonesha kukua kwa uchumi nchini kwa zaidi ya 7%, lakini ukuaji huu hauendani kabisa na kupungua kwa umasikini kwa watanzania,na hivyo kushindwa kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi walio wengi na kupelekea kuongezeka kwa pengo la kipato kati ya “Walionacho” na “Wasionacho” pengo ambalo limetajwa kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Bubelwa katika uwasilishaji wake huo, alionesha wasiwasi mkubwa kwa jinsi ambavyo vigezo katika ukuaji wa uchumi nchini vinavyoangaliwa na taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani. Ailisema “Wakati wanapoangalia mauzo ya jumla hapa nchini kama kigezo kimojawapo katika ukuaji wa uchumi, hali ni tofauti kabisa kwani hakuna uhalisia kabisa katika matumizi ya bidhaa husika kwa mtanzania wa hali ya chini”.

Huku akisikiliza michango ya mawazo kutoka kwa wana GDSSS ambao nao hawakukubaliana na vigezo vimumiwavyo namashirika husika katika kutoa tathmini ya ukuwaji wa uchumi nchini, mtoa mada aliendelea kubainisha vigezo vingine vinavyotumia katika kupima ukuaji wa uchumi na ufanisi wake kutia shaka hapa nchini kuwa ni pamoja na:-

i) Uwiano uliopo katika utoaji wa huduma, ambapo alisema kuwa ni mdogo kati ya watoa huduma na wapewaji na kutolea mfano wa uchache wa madaktari na wauguzi katka sekta ya afya, hivyo kutostahili katika tathmini hiyo hapa nchini na kuonyesha shaka kuwa yawezekana vinatumika kwa ajili ya kuonyesha utukufu wa sera kandamizi za IMF na washirika wake.
ii) Utoaji wa elimu kwa kuzingatia ubora, nacho kama kigezo kingine kilikuwa na dosari nyingi kama wana GDSS walivyo bainisha kutokana na kutokuwa na uhalisia na maisha ya wananchi wa kawaida. Ulitolewa mfano wa ujenzi wa shule nyingi za sekondari usioendana na idadi ya walimu waliopo, hivyo kupelekea kuanzishwa utaratibu wa mafunzo ya muda mfupi ambao kwa hakika hawana uwezo wala sifa za kufudisha watoto na kusababisha kiwango cha elimu kushuka siku hadi. siku.
iii) Pengo la kipato kwa wananchi ambalo imechangiwa na watu wachache kujilimbikizia mali isivyo halali, ukosefu wa ajira, kukosa udhati kwa serikali katika kutoa fursa ya biashara za kazi kwa wananchi wazawa na kudorora kwa sekta ya kilimo nchini.
iv) Uwajibikaji, Uwazi na fursa ya kuhoji utendaji wa serikali pia kimekuwa ni kitendawili maana sasa kila mtu anafanya atakalo. Mikataba mibovu kila kukicha tena katika sekta nyeti na viongozi kutokupenda kuwajibika hata pale yanapobainika matatizo waliyotusababishia mpaka litoke shinikizo kutoka kwa IMF na washirika wake.
v) Uwezo katika maamuzi/uthubutu wa taifa katika maamuzi ndicho kigezo ambacho wana GDSS walikipinga zaidi kwa utamua uwezo mdogo wa kimaamuzi uliopo na hivyo kutoa majumuisho ya jumla kuwa hawakubaliani na takwimu za IMF kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa bali kwa kuzingatia igezo hivyo wanaamini uchumi umeshuka kwa kiwango kikubwa.

NINI KIFANYIKE
Baada ya mjadala mrefu kufanyika, wana GDSS kwa pamoja walitoa mapendekezo kadhaa kwa serikali na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha juhudi za makusudi zinafanyika na kunusuru mamilioni ya watanzania ambao wanaishi maisha ya duni kutokana na serikali kukumbatia sera za mabepari. Hivyo katika muktadha huo yafuatayo yaliazimiwa katika semina hiyo:-
i) Ufanyike mjadala wa kitaifa kujadili/kuhoji utekelezaji wa sera za IMF na WB nchini kwetu ili kubaini ukweli juu ya dhamira yao kwetu na kupanga mkakati madhubuti kwa kuishinikiza serikali yetu kubadili mtazamo wa utekelezaji wa mipango yake kwa kujali zaidi maslahi ya wananchi wake kuliko maslahi ya wachache.
ii) Tupinge kwa nguvu zote utekelezaji wa sera/mipango yote isiyo na tija kwetu hivi sasa kutoka kwa taasisi zote kubwa za fedha duniani kama IMF na Benki ya Dunia(WB) na nchi tajiri wakati tukishinikiza kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa taifa letu.
iii) Kuongeza ushawishi kwa umma/ wananchi wengi zaido ili kushirikisha maisha yao na uchaguzi wa viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali.
iv) Kufanya mabadiliko katika uongozi wa serikali kuu kila tunapoona malengo tuliotarajia hayakufikia matarajio/baada ya kushindwa kuleta maendeleo stahili na hali bora kwa wananchi walio wengi.
v) Kuanzisha mtaala wa elimu kuhusu uzalendo na kuwa na malengo ya kitaifa.
vi) Kuhimiza wasomi na wataalamu wengine nchini wajitoe muhanga katika kuleta maendeleo nchini badala ya kuwaachia wanasiasa peke yao.

HITIMISHO
Wakati wa kufanya hitimisho la semina, ilikubaliwa na washiriki wote kuwa pamoja na kuitaka serikali yetu itazame upya utekelezaji wa sera za mashirika makubwa ya fedha duniani na nchi wahisani lakini ni jukumu letu pia kuwa na macho ya umakini kwa viongozi tunaowachagua ili kuzuia/kuepuka mfumo wa uwakala/kibaraka ambao kwa kiasi kikubwa umeifanya serikali yetu kuwajibika zaidi kwa IMF, WB na mashirika mengine makubwa ya fedha ama nchi tajiri duniani kuliko wananchi wake jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limeathiri hata utendaji katika ngazi ya serikali za mitaa.

Ukiwa kama mwanaharakati unashiriki vipi kuhakikisha Ujumbe huu unawafikia walengwa?

Ripoti imetayarishwa na Ally Nindi.

Mrejesho wa Kamati ya GDSS Iliyoundwa kufuatilia Mkutano wa IMF na Afrika

Mrejesho na kamati iliyoundwa tarehe 18/2/2009 ili kufikisha mawazo mbadala kwa Serikali, Shirika la Fedha Duniani(IMF) na washirika wao kutoka kwa Wanaharakati wa Maendeleo na Jinsia na wananchi kwa ujumla kuhusu zahama/mgogoro wa uchumi duniani na kufanyika kwa mkutano wa IMF nchini tarehe 10–11/3/2009. Katibu wa kamati hiyo Hashim Luanda alisema, kimsingi kamati hiyo kwa kushirikiana na asasi nyingine za kiraia (AZAKI) walipanga kufanya maandamano pamoja na kuandaa tamko maalumu na kulifikisha kwa walengwa.

MATOKEO YA KAMATI
Kupitia mwamvuli wa Policy Forum, Human Development Trust (HDT) na Tanzania AIDs Forum, kamati ya GDSS kwa pamoja na asasi nyingine za kiraia za ki-Tanzania walikutana katika ukumbi wa Dar es salaam International Conference Center (DICC) na kutoa tamko lenye madai yafuatayo:-
• Kuitaka IMF kushirikisha wadau katika utungaji sera za uchumi kwa nchi husika na kupinga sera za jumla kwa makundi mbalimbali ya nchi kwa sababu ya utofauti wa mazingira.
• IMF ipunguze/kulegeza masharti yake kwa kuzingatia maoni ya wadau kwa kuzishauri nchi kuunda sera ambazo mahitaji ya watu wake. Mfano: Iruhusu serikali iweze kutumia fedha ipatazo kutoka kwa wafadhili kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini badala ya kuzitumia katika kuongeza akiba ya fedha za nje.
• Kuitaka serikali ya Tanzania ibadili mtazamo wake kwa wadau wa maendeleo nchini kwa kutoa kipaumbele kwa AZAKI katika kutunga, kuridhia, kusimamia na kutathmini sera za uchumi wa nchi na hatimaye kuzifanya sera za uchumi kuwa mali ya wananchi.
• Kuitaka serikali kutoa fursa ya ushirikishwaji katika ngazi mbalimbali za mipango na utekelezaji wake ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Mfano: Katika Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) ambao unaangalia na kusimamia mapambano dhidi ya umasikini.
• Kuitaka serikali kupunguza pengo kubwa lililopo kati ya “Walionacho” na “Wasionacho” ili kupunguza uwezekano wa nchi kuingia katika machafuko yatakayosababishwa na kukata tamaa kwa wananchi walio na kipato cha chini.

Katibu wa kamati alisema, hawakufanikiwa kuandaa maandamano kutoka na ufinyu wa muda na badala yake kamati ya GDSS ilishiriki katika mkutano mbadala kuhusu zahama / mgogoro wa uchumi duniani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa British Council ambao pia uliratibiwa na asasi zilizotajwa hapo awali.
Mkutano huo ambao ulishirikisha wanaharakati, wataalam wa uchumi na wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam (UDSM) na Mzumbe, ulijadili kwa kina ili kupata takwimu sahihi katika ukuaji/kuanguka kwa uchumi nchini.

Mwisho alisema, katika mambo yote waliyoshiriki walipata mapokeo mazuri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na kuelezea matumaini ya kamati yake kuwa ujumbe utawafikia walengwa. Hivyo aliwataka wananchi kwa ujumla wao kutumia fursa ya msukumo ambao uliooneshwa na wanaharakati ili kuongeza nguvu katika kuihoji serikali katika ngazi mbalimbali za uongozi.

Ripoti imetayarishwa na Ally Nindi.

Friday, March 6, 2009

Mrejesho wa GDSS - Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8/03/2009.

Katika kuadhimisha siku hii muhimu ya harakati za kumkomboa mwanamke kimapinduzi, GDSS waliandaa big-bang ambayo ilijumuisha wanaharakati kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini, na kupambwa na vikundi vya sanaa na buradani, uimbaji wa nyimbo na ngonjera, maandamano madogo, na watoa ushuhuda. Mgeni rasmi katika sherehe hiyo alikuwa ni naibu waziri wa afya, Dr. Aisha Kigoda. Big bhang hiyo ilifanyika katika viwanja vya TGNP siku ya tarehe 4/03/2009 kuanzia saa sita mchana. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuwahudumia wanaoishi na VVU ni jukumu letu sote sote Wanawake, Wanume na jamii kwa ujumla”

Mchangiaji wa kwanza katika tamasha hili dada Mary Rusimbi, alisema, uchaguaji wa kauli mbiu hiyo ya mwaka huu umetokana na juhudi za wanawake na wanaharakati kutaka mchango wa wanawake katika kazi za kijamii kupewa kipaumbele na kuthaminiwa, tofauti na sasa ambapo wanawake wanafanya kazi nyingi lakini hazithaminiwi. Kazi ambazo wanawake wamekuwa wakizifanya ni pamoja na kutafuta kuni na maji, kuhudumia wagonjwa na wazee, kulea watoto, kazi za kilimo, na kutunza familia kwa ujumla.

Kazi zote hizi zimeshindwa kutambulika katika mfumo wa hesabu za kiserikali na kusababisha wanawake kufanya kazi ambazo hazina malipo kwa muda mrefu. Kuanzishwa kwa mfumo wa kuwahudumia wagonjwa wa VVU majumbani kunamaanisha wanawake kuendelea kuongezewa mzigo wa kazi ambazo hazina malipo. Mfumo wa mila za jamaii yetu umekuwa ukichangia kuendeleza hali hii ya ukandamizaji wa wanawake. Pia dada Mary alieleza mchango wa mashirika ya kijamii-CSOs, ambapo aligusia juhudi zilizofanywa na kuendela kufanywa na mashirika haya katika kuifanya jamii itambue mchango huu wa wanawake. Mwaka 2005 CSOs ziliweza kuishawishi serikali kupitia National burue of statistic-NBS kufanya takwimu za matumizi ya muda kwa wanawake, wanaume, wazee, na watoto. Nia ya utafiti huu ilikuwa ni kutambua matumizi ya muda miongoni mwa wanajamii na kuifanya jamii itambue mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo ya taifa, ambao wanachangia karibu asilimia 60 ya pato lote kupitia kazi ambazo hazina malipo.

Mchangiaji wa pili dada Neema Duma Kutoka Shirika la WOFATA-Women Fight Aids Tanzania-, yeye aligusia juu ya changamoto wanazokutana nazo katika kazi zao za utoaji wa huduma kwa wagonjwa waliopo majumbani. Ambaye pamoja na mambo mengine aligusia juu hali ya usiri kwa wagonjwa inayotokana na unyanyapaa katika jamii, na kushindwa kwa serikali za mitaa kutoa misaada/ushirikiano kwa wagonjwa ama mashirika yanayohudumia wagonjwa hao. Mchangiaji wa tatu, dada Salama kutoka Bagamoyo, yeye alitoa ushuhuda wa kuishi na VVU. Alijigundua kwamba anaishi na VVU mwaka 2000 na kuendelea kupambana navyo mpaka sasa. Alitoa wito kwa serikali na mashirika ya misaada kuongeza misaada ya chakula kwa wagonjwa, kwani wagonjwa wengi hawapati lishe bora kwa vile hawana fedha za kununulia chakula bora.

Kwa upande wake mgeni rasmi-Aisha kigoda- aliwapongeza wanawake kwa kuanza kuamka na kupigania haki zao, ambaye alisema ni tofauti na awali ambapo ilikuwa si rahisi kwa wanawake kusimama na kusema jambao lolote mbele ya hadhara, mfumo ambao ulilelewa na mila zetu. Pia alitaka wanaume nao waelimishwe ili waweze kutoa huduma kwa wagonjwa majumbani badala ya kuwaachia wanawake pekee yao. Waziri alikiri kuwepo na upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya ambao unafikia asilimia 50, na kuahidi kuwa serikali inafanyia kazi kufidia upungufu huo. Alisema serikali imetoa mtaala ambao utasaidia kuwaongoza watoa huduma majumbani, kutolewa kwa mtaala huo ni juhudi za serikali katika kupunguza mzigo kwa watu wanatoa huduma kwa wagonjwa waliopo majumbani. Changamoto iliyopo mbele yetu alisema mgeni rasmi ni “jinsi ya kufikisha taarifa hizi kwa watu wengi zaidi na kuwafanya washiriki katika harakati hizi za kupunguza mzigo wa kazi kwa akina mama”

Baada ya mgeni rasmi kuongea, walifuata watoa ushuhuda kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao walielezea uzoefu wao juu hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa majumbani katika maeneo yao wakielezea changamoto wanazokumbana nazo na nini kifanyike ili kuboresha utoaji huduma katika maeneo hayo. Baada ya watoa ushuhuda ikafuatiwa na michango kutoka kwa washiriki wa tamasha hili, kabla ya muungozaji wa tamasha-dada Gema Akilimali- kuhitimisha kwa kuwashukuru wote walioshiriki.

Ukiwa kama raia/mdau unashiriki vipi katika harakati hizi? Nini mchango wako kuhakikisha mzigo wa kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI linakuwa ni jukumu la watu wote katika jamii?

Wiki ya Wanawake Duniani


Serikali ina jukumu kubwa kuhakikisha huduma za afya hasa vituo vya afya, wataalamu, madawa na elimu kwa wanaoishi na VVU nyumbani zinawafikia

Thursday, March 5, 2009

Wiki ya Wanawake Duniani


Juhudi za kuwatunza wanaoishi na VVU wasiachiwe watoto kwani inawaathiri kielimu na maisha yao baadaye.

Wednesday, March 4, 2009

Wiki ya Wanawake Duniani



UJUMBE WA LEO:

Jukumu la kuwatunza wanaoishi na VVU nyumbani ni letu sote, na sio la watoto, wanawake na wazee wa kike peke yao.

Jamii:
Ina wajibu wa kusaidia kwa hali na mali kaya zinazotunza wagonjwa wa VVU nyumbani.

Serikali za Mitaa:
Zina wajibu wa kuhakikisha huduma zote muhimu, kama elimu ya msingi ya utunzaji wa wagonjwa wa VVU, zahanati, maji n.k. zinapatikana ili kurahisisha utunzaji wa wagonjwa wa VVU nyumbani.

Serikali Kuu:
Ina wajibu wa kutoa na kufuatilia matumizi ya rasilimali zinazoelekezwa kwenye Serikali za Mitaa, ili kusaidia utunzaji wa wagonjwa wa VVU nyumbani.