Friday, February 20, 2009

Trekta kwanza vitambulisho visubiri

BAADA ya miaka mingi ya danadana kuhusu uanzishwaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatimaye Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza kwamba kampuni sita zimepita kwenye mchujo wa awali wa wazabuni wanaopendekezwa kutengeneza vitambulisho hivyo. Mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani Sh. bilioni 222.

Tunafahamu hii ni habari njema, kwa wakati huu, kwa kuzingatia kuwa mradi huo umekuwa kwenye kauli zaidi kuliko vitendo, ukitawaliwa na utata, kificho na danadana nyingi, tena kwa muda mrefu mno. Tunasema ni habari njema kwa wakati huu, kwa sababu mchakato wa kuzichuja kampuni hizo sita zilizoingia kwenye kinyang’anyiro cha mradi huo, bado unaweza kuchukua muda mrefu na kuingiwa na danadana nyingine zaidi.

Lakini pia, kwa mtazamo wetu, kwa kuzingatia matakwa ya nchi hivi sasa, tunaona suala la Vitambulisho si kipaumbele cha maendeleo kwa sasa. Tulipaswa kuangalia matakwa ya sasa ya wananchi, na mazingira tuliyomo, ya mtikisiko wa uchumi duniani na upungufu wa chakula kutokana na baadhi ya vyakula kutumika kama nishati.

Kwa maana hiyo, kwa maoni yetu kwa kuangalia mahitaji ya sasa ya nchi, mradi wa Vitambulisho vya Taifa unaweza kuwekwa pembeni, na wala tusidhurike, ili hizo Sh. bilioni zaidi ya 200 zitumike, kwa mfano, kununulia matrekta yatakayoongeza kasi ya kilimo nchini yakituzalishia chakula na fedha ili tukiwa na shibe na tuna ‘vijisenti’ katika mifuko yetu hapo tuulizane nani ni nani.

Kwa nini tunasema haya leo? Kwa miaka mingi, tangu wazo la kwanza la kuwa mradi huu lilipoota, hakuna kitu kilichofanyika, badala yake watu wamekuwa wakikodoa macho kutaka kuona nani atafaidi nini kutokana na mradi huu, na Mungu bariki, kwa miaka yote hakuna Mtanzania aliyeteseka kwa kuwa hana kitambulisho; na hiyo ni pamoja na ukweli kwamba huo ndio wakati ambao nchi hii ilijaa watu: wakimbizi kwa malaki, ambao sasa wamerudi makwao.

Bila Vitambulisho vya Taifa, nchi imeendelea na mambo yake kama kawaida ikizama katika matatizo yetu makubwa lakini ya kawaida: njaa, afya, elimu, miundombinu, na mengineyo.

Sisi tulidhani sasa wakati umefika wa kuachana na mradi huu, pamoja na umuhimu wake wote, walau kwa muda, ili tuelekeze nguvu zetu katika mambo kipaumbele.

Sasa tunakabiliwa na njaa, tena katika mikoa ambayo huko nyuma ilikuwa ni aibu kuitaja kuwa ina njaa, badala ya Vitambulisho fedha hizi zitumike kwenye zana na pembejeo za kilimo, ziboresha elimu yetu ambayo imepanuliwa bila vifaa na miundombinu ya kutosha, ziboreshe huduma za afya, ujenzi wa barabara na usambazaji wa nishati.

Hatuwezi tukajitokeza hadharani leo hii, mbele ya ulimwengu, tukiwa vifua mbele, tukadai kuwa Vitambulisho vya Taifa ni bora zaidi kuliko matrekta na pembejeo kwa wakulima, au hata maabara, vitabu na walimu kwenye shule zetu. Kwa hakika, tukiwa na mawazo hayo tutashangaza watu.

Wakati mwingine dhana nzima ya Vitambulisho hakika inaghilibu akili. Hebu fikiria vitambulisho hivyo vitatumia teknolojia ya kisasa, hii maana yake ni kwamba vitahitaji umeme au mitambo inayoendeshwa kwa umeme.

Lakini sehemu kubwa ya jamii yetu ipo vijijini, ambako umeme bado ni kitendawili kikubwa, ni huko pia kwenye zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote, wanaotegemea kilimo, hata kama bado ni kilimo duni. Kitambulisho kinachotumia teknolojia hiyo kitatumikaje na kitamsaidia nini mkulima huyu ambaye haoti kupata umeme leo wala kesho?

Inatosha kuwa wazi kwamba sasa tuangalie mambo ya kipaumbele kwa maendeleo na faida ya jamii pana. Inawezekana Vitambulisho vya Taifa vilikuwa kipaumbele nyakati fulani siku zilizopita. Kwa leo, ukichanganya na anguko la uchumi duniani kote, hakika kununua vitambulisho ni kati ya matumizi yasiyokuwa ya lazima. Si kipaumbele cha maendeleo. Tunasubiri kuona huyo Mtanzania atakayenunua kitambulisho sampuli hii, ilihali kwake hakuacha mchango wa meza.

Raia Mwema, 18 Februari, 2009.

2 comments:

Anonymous said...

kweli kabisa vitambulisho hivi sio 'dili' kiivyo kama viongozi wetu wanavyojaribu kung'ang'ania kutueleza, naungana na mtoa hoja kwamba ni heri tukaelekeza nguvu zetu katika kilimo zaidi, kuliko vitambulisho hivi vya kisasa...
mdau.

Anonymous said...

Nimesoma na kutafakari kwa makini maoni yaliyotolewa hapo juu. Kwa hakika suala la vitambulisho siyo kipaumbele hivi sasa na kamwe taifa haliwezi kuadhirika kivyovyote hivi sasa kwa kutokuwa na vitambulisho. Msukumo wa kuchapisha vitambulisho hivi sasa ni tamaa binafsi zilizojikiita miongoni mwa hao walafi na wabakaji wa rasilimali fedha za wananchi kwa faida na manufaa yao binafsi. Tunayo matatizo lukuki kitaifa, yakiwemo ya kielimu, kiafya na mengine kadha wqa kadha yanayoikumba jamii. Tunayomatatizo ya upungufu na mfumuko wa bei kwa mazao ya chakula kutokana na kupanda bei kwa pembejeo za kilimo na gharama za usafirishaji. Bado tunayo matatizo makubwa ya nishati vijijini ambayo mwisho ni vigumu kutabiriwa; na hata mijini ambako miundo mbinu za umeme zinaporomoka siku hadi siku. Bado tunayo migogoro hata katika mifumo ya usimamizi ya utoaji wa elimu ya juu kwa watoto/vijana wetu hususan wale wanaotoka katika familia zetu za kimaskini. Yapo mengi ambayo tunaweza kuandika makala kwa makala kudhihirisha kuwa yanastahili kipa-umbele kuliko kuangaika na vitambulisho hivi sasa. Kama serikali inasikiliza kilo chetu iachane na mpango huo wa vitambulisho vya kifaifa ambao lengo lake nikuwanufaisha hao manyang'au na mafisadi wa rasilimali fedha za Watanzania.