Kampuni ya Msolopa Investment Limited iliyopewa jukumu la kukusanya madeni ya Sh bilioni 199 zilizochotwa serikalini kupitia mpango wa Uagizaji wa Bidhaa Nje (CIS) imeomba ulinzi wa polisi kwa ajili ya kukamata na kutaifisha mali za kampuni 25 zinazodaiwa deni hilo.
Wakala huyo alitoa wiki mbili kwa baadhi ya wabunge na mawaziri wakiwamo wastaafu 40 ambao kampuni zao zimetaifishwa pia kuchota pesa hizo wawe wamelipa vinginevyo, atawaanika katika vyombo vya habari sambamba na kutaifisha mali zao.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ibrahim Msolopa alisema kati ya kampuni 30 (tofauti na hizo za wabunge na mawaziri) zilizopewa wiki mbili kulipa madeni hayo, kampuni tano pekee ndiyo zilijitokeza kuanza kulipa madeni.
Alizitaja kampuni tano zilizoanza kurejesha fedha kuwa ni Shela Beach Investiment, Chichi Enterprises, Paninye Investments, Simba Resources na Avicena Pharmaceutical.
Kampuni 25 ambazo wamiliki wake wameendelea kukaa kimya ambazo alisema zitakamatwa wakati wowote baada ya kupata ulinzi wa Polisi, ni Kiex Trading inayomilikiwa na Rajabu Maranda ambaye anatuhumiwa kuchukua fedha za Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) na mfanyabiashara Andrew Traders.
Nyingine ni K. Agencies International, Chawe Transport, Sikute Enterprises, Danico Ltd, Apemac, Dar es Salaam International School Trust Fund, Oriental Transport, Auxi Pharmaceutical, Family Care Clinic Pharmacy, Aliya Investiments, Agriculture Sales, Kashif Traders na Rein.
Alizitaja kampuni nyingine kuwa ni Twins Investments, Road Conqueres, Getca International, Dodoma Oil Mills, Shivji & Sons, Tyre Centre, Rela Investments, Amazon Trading, Transport Import & Export na Pharmavet. Kwa mujibu wa Msolopa, wameshamwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuomba ulinzi kwa ajili ya kuendesha operesheni hiyo ya kukamata kampuni hizo.
Alisema baada ya kumaliza kukamata na kutaifisha mali ili kufidia madeni, ifikapo Machi 15 mwaka huu, wataanza kukamata mali za mawaziri na wabunge walioko madarakani na waliostaafu, ambao wako ndani ya kundi la kampuni 40 waliokaidi kulipa madeni.
Alisema mawaziri na wabunge wanaendelea kulipa fedha zilizochotwa na wengine walianza kulipa baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwafuata bungeni katika Mkutano wa Bunge uliopita lakini wapo ambao hawalipi kabisa licha ya kuwa na taarifa za kudaiwa.
Akizungumzia kiasi cha fedha kilichokusanywa mpaka sasa, Mkurugenzi huyo alisema wameishawaandikia makamishna wa sehemu nne zinazotumika kulipia madeni, ili kutambua kiasi cha fedha kilichokusanywa ambacho watakitangaza kwa umma ili kukifahamu baada ya kampuni hiyo kuanza kazi ya kukusanya madeni hayo.
Alisema wadaiwa wa fedha hizo hulipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), benki za NMB, CRDB na ya Rasilimali Tanzania (TIB). Alisema serikali ilizikopesha kampuni 916 Sh bilioni 199 kwa lengo zuri lakini zilitumika kwa madhumuni yasiyokusudiwa, kampuni zingine 80 zilikuwa zimeishalipa fedha zilizokopa na nyingine ziliendelea kulipa isipokuwa hizo 30.
Daily News; Monday,February 23, 2009
1 comment:
kama kweli hili litafanyika nchi yetu inaweza kujikwamaua kutokana na hali mbaya ya kiuchumi amabayo imechangiwa na 'ujanja-ujanja' wa watu waliopewa dhamana ya kuongoza nchi yetu. unaweza ukajiuliza 'wakati hizo fedha zinaiibiwa wahusika walikuwa wapi?
Post a Comment