TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MADAI YA WANAHARAKATI KUPINGA TAMKO LA WAZIRI WA SHERIA NA MAMBO YA KATIBA KUHUSU SHERIA YA MAKOSA YA KUJAMIIANA (SOSPA) YA MWAKA 1998.
UTANGULIZI
Mtandao wa wanaharakati wanaoshiriki semina za kila Jumatano za jinsia na maendeleo, ukombozi wa wanawake na haki za binadamu (GDSS) tunalaani vikali tamko la Mh. Mathias Chikawe Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba alilolitoa kwenye gazeti la Rai tarehe 8-14/1/2009 kutaka adhabu ya makosa ya kujamiiana ipunguzwe.
Mh. Waziri ameonyesha udhaifu wa kutafsiri sheria hiyo, kwa kutoa tamko bila kufanya utafiti wa kina kwa wahanga walioathiriwa na vitendo vya ubakaji mfano wanawake, watoto, vikongwe, watu wenye ulemavu nk.
Ikiwa ni miaka kumi (10) sasa tangu kupitishwa kwa sheria hii, Waziri anaposema sheria hii ni mbaya anaonyesha wazi kutotambua mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote hicho kwa jamii kuvunja ukimya na kuripoti matukio mengi ya ubakaji na watuhumiwa kuchukuliwa hatua, hata kiasi yeye mwenyewe kukiri kuwa wafungwa wa ubakaji ni wengi magerezani.
MADAI YA WANAHARAKATI
Kutokana na hayo tuliyoyaeleza hapo juu sisi wanaharakati tunadai yafuatayo:-
1. Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba iitishe mjadala wa Kitaifa kwa wadau wote ili kufanya upya mapitio ya sheria hii ili kuangalia mapungufu na mafanikio ya sheria hii, kabla ya kupelekwa Bungeni kama Waziri alivyoahidi.
2. Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto atoe tamko rasmi akielezea mafanikio ya sheria ya makosa ya kujamiiana tangu kuanzishwa hadi sasa.
3. Tumesikitishwa na matamshi ya Mhe. Waziri kwamba Bunge lilishinikizwa na wanaharakati kupitisha sheria hii ya makosa ya kujamiiana. Hivi waziri anammanisha nini hapa? Je? linafanya kazi kwa shinikizo la watu bila kufuata sheria na taratibu? Kwa hili tunamtaka Waziri aliombe radhi Bunge letu tukufu.
4. Sheri ya ndoa ya mwaka 1971 na sheria ya makosa ya jinai (Penal code) zifanyiwe marekebisho haraka ili zisikinzane na sheria ya makosa ya kujamiina ya mwaka 1998 na sheria ya elimu 1978.
5. Sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) itambue ubakaji ndani ya ndoa.
6. Kutokana na msongamano mkubwa wa kesi za makosa ya jinai katika mahakama zetu, tunaitaka serikali ianzishe mahakama maalum itakayoshughulikia kesi zote zinazohusiana na ukatili wa jinsia.
Sisi kama wanaharakati tunaamini kuwa kutiliwa mkazo kwa sheria ya SOSPA kutasaidia sana kupunguza matatizo mengi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kuwaepusha mabinti wanaotiwa mimba wakiwa shuleni jambo ambalo ni kilio kikubwa kwa Taifa letu.
Mwisho tunashauri viongozi wetu wawe makini pale wanapotoa matamko mbalimbali.
Imetolewa na Mtandao wa wanaharakati wanaoshiriki semina za kila Jumatano za jinsia na maendeleo, ukombozi wa wanawake na haki za binadamu (GDSS) na kusainiwa na
1.Kigogo Youth and Women Development Programme (KYWDP)
2.African Life Foundation
3.Youth Action Volunteers (YAV)
4.Mabibo Youth Center
5.Twitange Development
6.SHDEPHA + Mbagala
7.Afya kuu (KURASINI)
No comments:
Post a Comment