Tuesday, February 3, 2009

Pinda yuko sahihi lakini...



WIKI iliyopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara mahususi katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga na Tabora akiwa na ajenda moja kuu: mapambano dhidi ya mauaji yanayoshamiri nchini ya walemavu wa ngozi (Albino).

Sitaki kurejea yale yote yaliyojiri kwenye ziara hiyo ila jambo moja kubwa ambalo limezua mjadala katika jamii. Hili ni kauli yake ya ‘jino kwa jino’ kwa maana kwamba wauaji wa walemavu wa ngozi pindi wanapokamatwa ‘red handed’ basi hakuna haja ya kuwapeleka polisi (ila nao wauwawe).

Hii ni kauli nzito kutolewa na kiongozi mzito wakati huu ambao nchi iko katika hekaheka ya kujaribu kukomesha mauaji ya hawa ndugu zetu ambao kwa miaka mingi tumeishi nao bila matatizo.

Nianze kwa kukiri kabisa kwamba kwa mtu yeyote ambaye ni muumini wa utawala bora kwa maana ya utawala unaoheshimu na kuzingatia sheria, kuua ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya msingi ya binadamu ambayo ni kuishi. Hii hahitaji kuwa mwanasheria ili kuwa mtetezi wa haki za binadamu na utawala bora.

Lakini kuna jambo moja la msingi ambalo mpaka sasa linatatiza sana kuhusu hizi haki za binadamu na watu wanaozitetea kwa nguvu zao zote. Kwamba kuua mtu hakuna tatizo ila kuua mtu aliyeua ni kosa kubwa!

Hapo ndipo ninapoungana na Waziri Mkuu Pinda. Kwamba iweje mtu mmoja awe na haki ya kuua lakini abaki na haki yake ya kuishi? Hivi huyu aliyeuawa hakuwa na haki ya kuishi? Na kama anayo kwa nini asitetewe basi? Na kama amenyimwa haki yake ya kuishi kwa nini huyu aliyemnyima naye asipokonywe (auawe) haki yake kama alivyomfanyia mwenzake?

Mnaliangaliaje suala hili wanaharakati wenzangu?

No comments: