Thursday, February 19, 2009

Mrejesho wa GDSS

Katika semina za GDSS jumatano ya tarehe 18/02/2009 mada ilikuwa ni juu ya “Mawazo Mbadala Kuhusu Mgogoro wa Kiuchumi wa Dunia na Mkutano Mkuu IMF na Afrika wa Machi 10-11” Wawasilishaji mada walikuwa ni Bashiru Ally (UDSM) na Morjorie Mbilinyi (TGNP) na washiriki kuweza kuibua hoja mbalimbali.

Bashiru(pichani) aliuhusisha mfumo wa sasa wa soko huria na chanzo chake ambacho ni enzi za biashara za utumwa, ukoloni, ukoloni mamboleo, mpaka utawandazi wa sasa. Tangu mwanzo mfumo huu wa kinyonyaji haukuwa na mafanikio mazuri, na umekuwa na migogoro mara kwa mara na kuyafanya mataifa ya kibepari-ubeberu kuendelea kubuni mbinu mpya ya kuendeleza unyonyaji wao. Waafrika na mataifa mengine duniani kote ambayo yalikuwa yakinyonywa na mabepari hao waliendeleza mapambano ya kudai haki zao zilizokuwa zikichukuliwa kwa nguvu. Mbinu mbali zilitumiwa na waafrika na mataifa haya ya duniani ya tatu, baada ya uhuru ule wa bendera wa miaka ya 1960, kwa mfano hapa Tanzania tulifuata mfumo wa usawa na kujitegemea.

Mgogoro wa uchumi unaoendelea dunia, unamaanisha kwamba mfumo wa kibepari-ubeberu unaendelea kushindwa kama ulivyoshindwa huko awali. Kwa maoni yake(Bashiru), mgogoro huu una sura mbili kwa Watanzania na Afrika. Sura ya kwanza; Watanzania wanaweza wakashindwa kabisa kujinasua katika mgororo huo, na mfumo wetu wa kiuchumi kuumizwa vibaya. Sura ya pili; mgogoro huu unaweza kutoa fursa kadhaa, ambazo ni pamoja na; kuweza kutambua kwamba kuathiriwa kwetu vibaya katika kipindi hiki kumetokana na kufuata mfumo wa utegemezi kuendesha serikali na nchi yetu, njia tuliyoshauriwa na IMF/WB na hivyo kupata fursa ya kujipanga na kutafuta njia mbadala. Fursa ya pili ni kwamba tunaweza kupunguza utegemezi na kuweza kupanga mipango ya maendeleo kulingana na mazingira, mifumo, taratibu na changamoto zetu zinazotukabili. Fursa ya tatu ni kuepuka kupanga mipango ya uchumi na maendeleo kwa kutegemea wawekezaji na wafadhili katika utekelezaji, kitu ambacho Bashiru alikiita ni kupanga mipango ya kiuchumi ya “kikamali”. Furasa nyingine ni kuweza kujiamini na kupata uwezo wa kufanya maamuzi magumu zaidi hivyo kujiletea maendeleo halisi.

Morjorie naye aligusia juu ya hatua/mbinu zinachukuliwa na mataifa tajiri katika kupambana na mgogoro huu wa kiuchumi ambazo alizitaja kuwa ni pamoja na; kupunguza riba; kutoa mikopo; serikali kuendelea kuungilia uchumi na biashara ya nchi husika; ambaye yeye (Morjorie) aliona hatua hizi ni sawa na kuanzisha mfumo wa Ujamaa kwa matajiri.

Alitaja madhara ya mgogoro huo wa kiuchumi kwa Afrika ni pamoja na; kukosekana kwa masoko kwa bidhaa za Afrika na kushuka maradafu kwa bei za bidhaa hizo, kukosekana kwa mikopo kwa wafanyabiashara, fedha za kigeni kupungua zaidi, bei ya chakula na nishati-hasa mafuta kuendelea kuongezeka, vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kuongezeka maradufu, biashara haramu za ngono na ya kusafirisha watu kushamiri, na maliasili zetu kuendela kuporwa na wageni.

Pia Morjorie alielezea kuhusu migogoro inayeondelea hapa nchini na harakati za wananchi kugombea mgawanyo bora na sahihi wa maliasili zilizopo, na kuoanisha migogoro hiyo na mgogoro wa kiuchumi duniani. Kwa mfano; Migomo katika sekta ya elimu, wananchi kuzuia misafara ya viongozi, DC aliyewachapa viboko walimu, na mapigano ya wakulima na wafugaji. Na kuongeza, “hali hii isipodhibitiwa mapema itakuwa na madhara makubwa katika kipindi hiki cha mgogoro mkubwa wa kiuchumi duniani”

Tufanye nini?
Katika tufanye nini wanasemina walikubaliana mambo makuu ambayo ni muhimu yakafanyika katika siku hizi mbili za mkutano huu wa IMF na Afrika Machi 10-11.
1. Wanasemina walipendekeza maandamano ama mkutano kwa siku mbili nje ya jengo la mkutano huo na kuishinikiza IMF iondoe sera zake za ukandamizaji dhidi ya Afrika na Tanzania.
2. Liandaliwe tamko kwa vyombo vya habari ambalo litakuwa na msimamo na Ujumbe wa wanaharakati kwa IMF na washirika wao duniani kote.
3. Wanaharakati watumie vyombo vya habari kwa ajiri ya kutandaa na kuweza kufanya harakati za pamoja za kupingana mfumo huu kinyonyaji na kusaidia watu wengi kupata taarifa zaidi za mfumo huu wa unyonyaji na mkutano huu mkuu, hivyo kuwawezesha kushiriki katika harakati hizi za ukombozi huu wa pili wa bara la Afrika!

Harakati Daima!

Habari zaidi bofya:
http://www.imf.org
http://www.changes-challenges.org/

1 comment:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nilipenda dada maji alivyokuwa akijaribu kuinua hasira za wana GDSS ktk mkutano huo. eti anachukia ujio wa wachina wakati sisi kama watz tunamkaribisha kila mtu mwema aje kama ilivyo kwa warusi, nk.

na mimi natamani kumuoa mchina kama mjomba M alivyomuoa mrusi, sasa wakija wengi ntajipatia kamoja.

katika vita hii ni bora kwanza kuangalia nani yuko upande wetu na tuanahitaji wazalendo wa kweli sio watafutaji