Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste lililopo Idiwili Kata ya Iyula, wilayani Mbozi anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na mabaki ya mwili wa binadamu yaliyokuwa yakiuzwa Sh milioni 30.
Cosmas Mwasenga (39) alikamatwa Februari 13 mwaka huu akiwa na Luseshelo Mwashilindi ambaye inadaiwa alikuwa ameyahifadhi nyumbani kwake mabaki hayo. Mabaki hayo ambayo Polisi inahisi kuwa ni ya albino, ni vipande vinne vinavyosadikiwa kuwa sehemu ya mikono.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen alisema leo kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika eneo la Mlowo, Mbozi. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Zelothe alisema Februari 12 mwaka huu, polisi walipata taarifa kuwa kuna kikundi cha watu Mlowo, wana vipande vya mabaki ya mwili wa mwanadamu vinavyosadikiwa kuwa ni mabaki ya mwili wa albino.
Alisema taarifa hizo zilidai kuwa kikundi hicho kilikuwa kinatafuta wateja ili kuwauzia vipande hivyo na kwamba watu waliokuwa wanatafuta wateja waligawanyika katika Wilaya ya Mbozi na baadhi ya mitaa ya Jiji la Mbeya.
“Tuliweka mtego na kukutana na watu hao ambao walisema wanauza viungo vya ‘kunguru mweupe’ wakimaanisha albino, ambapo walikubaliana na kukutana na Mwashilindi ambaye alikuwa anahifadhi viungo na kufikia makubaliano ya kuvinunua kwa Sh milioni 30,” alisema.
Alisema Februari 13, taratibu za kupata kiasi hicho cha fedha zilikamilika na walipofika kwa Mwashilindi alitoka akiwa na vipande vinne vya mabaki ya binadamu vikiwa vimefungwa katika karatasi, na Polisi wakamkamata. “Baada ya kupekua katika nyumba ya Mwashilindi tulifanikiwa kupata dawa za binadamu, maji ya kuchanganya na dawa na koti jeusi mali ya Mchungaji Mwasenga,” alisema.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wote wawili wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika. Kamanda Zelothe alisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa Polisi na kusema kwa kufanya hivyo, ndipo vitendo vya mauaji ya albino vitapungua. “Tunapenda kuwaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za siri kwa viongozi wa juu, ili ziweze kufanyiwa kazi haraka,” alisema.
Daily News; Tuesday,February 17, 2009
1 comment:
mwanzoni wengi tulidhania labda watu kama waganga wa jadi ndio walikuwa wakihusika na ukatili dhidi ya wenzetu hawa, kumbe mtu yeyote anaweza kuwa ni mhusika mkuu katika ukatili na unyama huu!
Post a Comment