Friday, February 6, 2009
Waziri Masha atajiuzulu?
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha, anaweza kulazimika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu au kulazimishwa kujiuzulu, kama Bunge litaridhika kuwa ameingilia mchakato wa zabuni ya kumpata mchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa.
Taarifa za hivi karibuni zaidi kuhusu suala hilo la Vitambulisho vya Taifa, zinasema ya kuwa Waziri Masha yupo katika mtanziko wa ama kujiuzulu kabla ya kushambuliwa kwa hoja kali za wabunge au kusubiri mashambulizi hayo ndani ya ukumbi wa Bunge.
Taarifa zinasema kwamba juzi Jumatano, Waziri Masha aliitwa mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge, inayoongozwa na Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi, iliyokusudia kumhoji kwa kina kuhusu tuhuma za uingiliaji anaodaiwa kuufanya na kama Kamati hiyo itaridhika kuwa ameingilia mchakato huo, basi Kamati italazimika kuwasilisha suala hilo katika Kamati ya Uongozi ya Bunge, ambayo itapanga muda wa kulijadili.
Mfumo huo wa mahojiano unaomnyemelea Masha ni mithili ya ule uliotumika wakati wa uchunguzi wa kibunge wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Kwa upande wake, Masha alipohojiwa na Gazeti la Raia Mwema alithibitisha kuitwa na kamati hiyo ya Masilingi akisema amepewa taarifa ya kuitwa na atakwenda na kwamba asingeweza kuingia katika undani wa jambo hilo linalohusisha uvujaji wa nyaraka za siri.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza bungeni kujibu maswali kuhusiana na Vitambulisho aliweka bayana kuwa kuna tatizo katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwamba kuna nyaraka zimenyofolewa katika moja ya mafaili wizarani hapo.
Hata hivyo, alisema kunyofolewa kwa nyaraka hiyo si suala la msingi bali kwamba tatizo la msingi ni kuingiliwa kwa mchakato huo.
Pinda alimweleza Dk. Wilbroad Slaa, aliyekuwa amehoji mchakato wa Vitambulisho katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kuwa alikuwa amewahi mno kuuliza suala hilo kwa kuwa mchakato wa zabuni bado haujafika mwisho.
Akashauri kuwa ni vema mchakato ukafika mwisho na hapo ndipo Waziri Masha anaweza kubanwa vizuri kwamba ameingilia mchakato huo au la.
Hata hivyo, kuna uwezakano mkubwa kwa suala hilo kujadiliwa ndani ya Bunge kutokana na madai ya kuwapo kwa vielelezo thabiti vinavyomuhusisha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye anadaiwa kulalamikiwa na Waziri Masha kwamba amefanya uamuzi bila kumtaarifu yeye kama waziri wa wizara husika.
Waziri Masha anadaiwa kuandika barua kwa Waziri Mkuu Pinda akimlalamikia Luhanjo kuwa amefanya uamuzi kwa kumpa maagizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, bila ya yeye kutaarifiwa.
Baadhi ya wazoefu wa masuala ya Bunge wanaeleza kuwa huenda suala hili likafikia hatua ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ambayo ina madaraka ya kuhoji watu katika mfumo wa kimahakama.
Katika utaratibu wa kawaida, anayeitwa kuhojiwa na Kamati Teule ya Bunge hulazimika kula kiapo na akibainika kudanganya anaweza kushitakiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment