Sasa tujiandae kushuhudia watoto wetu wakikimbilia utumwani kwa maelfu. Wazazi na ndugu wa karibu wa vijana wa Afrika wanatakiwa wajiweke tayari kisaokolojia kukabiliana na upotevu wa vijana wao watakaoondoka hivi punde kujipeleka katika utumwa wa hiari.
Wanakwenda wapi? Si kwingine bali ni kule kule Marekani ambako walipelekwa mamilioni ya Waafrika waliouzwa huko kama punda wabeba mizigo, Waafrika ambao ndio waliojenga ukwasi mkubwa wa Marekani.
Sasa Marekani wanaye rais mweusi, ambaye ushindi wake umeshangiliwa sana na Afrika na dunia nzima kwa ujumla. Sasa, huyu rais mweusi anataka watu wengi wa kujitolea, hasa weusi, kwenda kumsaidia kupigana katika vita ambazo vijana wa Marekani wenyewe wanazikacha, kama hii ya Afghanistan.
Marekani wanasema sasa kwamba kijana ye yote asiyekuwa raia wa Marekani anayetaka kuwa raia atapewa uraia ndani ya miezi sita, MIEZI SITA TU, alimradi awe tayari kujiunga na majeshi ya Marekani kwenda kupigana Afghanistan na kwingineko kulikoungua shoka ukabaki mpini.
Utaratibu huu ulikuwa haujafanyika tangu mwisho wa vita ya Vietnam, ambayo, kwa ukali wake, ilihitaji vijana kutoka mataifa mengi duniani, hasa kutoka dunia ya tatu, na waliojitolea wakahongwa biskuti ya uraia.
Habari hizi bila shaka zitakuwa na ladha ya Bongo Flava kwa vijana wetu wanaopita wakisema, “Bora mbwa Ulaya kuliko Mswazi Bongo”. Watahamia Marekani, tena kwa wingi, siyo tu kwa sababu wameitwa kwenda huko bali pia kwa sababu nchi hii haielekei kujua ni nini inataka kufanya na vijana wake. Wameachwa wanamea kama magugu katika mahame. Hawajajengewa matumaini katika maisha yao ya baadaye na ni kweli kwamba wanaweza kuamini kwamba ni bora kuwa mtumwa Ulaya kuliko kuwa “huru” Afrika.
Ndivyo stori kutoka barani kote Afrika zinavyoonyesha, kama kule Senegal, ambako vijana wanasema, kama kufa na wafe, lakini hakuna kubaki Afrika, na mama zao wanakubaliana nao!
No comments:
Post a Comment