Profesa Issa Shivji |
TAASISI za kiraia zimesema mchakato wa kuunda Katiba Mpya bila
kuwa na dira ya mpango wa kitaifa unaweza kusababisha kupata Katiba
itakayohusisha mawazo ya watu wachache.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana katika ufunguzi wa tamasha la 10 linalohusisha asasi mbalimbali za kiraia nchini.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji alisema kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuunda Katiba Mpya alitegemea kungekuwa na dira ya mpango wa maendeleo katika Katiba hiyo.
Alisema bila kuwa na mpango huo kuna uwezekano wa kutengeneza Katiba itakayohusisha mitazamo ya watu wachache.
“Mimi nilidhani kwamba kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuunda Katiba Mpya kungekuwa na dira ya mpango wa maendeleo ili kujua tunataka Katiba ya aina gani,”alisema Profesa Shivji.
Profesa Shivji alibainisha kwamba vitu ambavyo ni muhimu kuwa katika Katiba Mpya ni pamoja na haki,usawa,amani,udugu, ujamaa na uhuru binafsi.
Katika hatua nyingine Profesa Shivji alisema suala la demokrasia katika Katiba Mpya ni vyema likazingatiwa kwa kupewa kipaumbele.
Akifafanua kuhusu demokrasia alisema kuna aina mbili za demokrasia ambazo ni demokrasia shirikishi na wakilishi.
Alisema ni vyema misingi ya demokrasia wakilishi ikazingatiwa kwani hapo ndipo inatoa uwezo wa kujitawala wenyewe.
No comments:
Post a Comment