Monday, November 5, 2012

Prof. Maghembe Ataka Kuundwa Kitengo Cha Uratibu Miradi ya Maji

WAZIRI wa Maji Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe ameitaka wizara kuunda kitengo maalum cha kuratibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya miradi ya maji ili kufanikisha malengo ya milenia ya upatikanaji wa huduma hiyo ifikapo mwaka 2015, hususan maeneo ya vijijini.

Kauli hiyo imetolewa jana na Profesa Maghembe wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa saba wa wadau wa sekta maji unaoendelea katika hoteli ya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo alisema utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo ya vijijini, miji midogo na wilayani bado kunachangamoto ya kutimiza malengo ya milinea hivyo kitengo hicho kitawezesha miradi hiyo kukamilika kwa haraka na gharama nafuu.

“Tunahitaji kuwa na kitengo hiki ili kuweza kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji. Nitaka uundaji wa kitengo hiki ukamilike katikati ya mwezi huu na kianze kufanya kazi mwishoni mwaka huu,” alisema Profesa Maghembe.

Kitengo hiki kinatakiwa kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo ya, vijijini, miji midogo na wilayani ili kuweza kutimiza azma hiyo.

Profesa Maghembe aliongeza kuwa ili kuhakikisha malengo ya milinea yanafanikiwa wizara yake inatakiwa kuwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Aidha alisema upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini ni asilimia 57. 8, wakati malengo ya milinea itakiwa kufikia asilimia 65 ifikapo mwaka 2015. upatikanaji wa huduma hiyo maeneo ya mjini umefikia asilimia 84, lakini lengo la milinea ni asilimia 90 – 95 ifikapo kipindi hicho.

Kwa upande wake mwakilishi wa wadau wa maendeleo ya sekta ya maji, Balozi wa Ujerumani Klaus –Peter Brandes aliipongeza wizara hiyo kwa kujitahidi kusimimia matumizi fedha za miradi ya maji na kutaka uendelea kufanya hivyo ili sekta hiyo iwe mfano bora.

Alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa wataangalia usimamizi bora wa kiufundi katika miradi hiyo. Naye mwakilishi wa Mtandao wa wadau wa sekta ya maji (TAWASANET, Mathew Halla alisema suala ya upatikanaji ya huduma hiyo ni haki kwa kila mwajamii.

Aliishauri serikali iharakishe uundaji ya sera ya maji safi na salama. Naye Waziri wa TAMISEMI, Aggrey Mwanri alisema wizara iko tayari kutoa ushirikiano huo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ipasavyo, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutekeleza miradi hiyo pale unapohitajika.

No comments: