Wednesday, November 21, 2012

Mabadiliko Ya Sheria Ya Habari Yasiachiwe MCT Pekee

Na: Daniel Mbega, Iringa
KWA takriban miaka 20 sasa, wadau wa habari wamekuwa wakipiga kelele kuhusu kuwepo kwa Uhuru wa Habari, hasa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Wanahabari kwa ujumla wake.

Jitihada za kelele hizo ndizo hasa kimsingi zilizozaa Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambalo lilisajiliwa rasmi mwaka 1997 likiwa na majukumu mbalimbali, ikiwemo kuwasimamia wanahabari nchini.

Hata hivyo, pamoja na majukumu mengi iliyonayo, MCT kwa kushirikiana na wadau wengine kama Misa-Tan, Tamwa, Nola, LHRC, TLS, TGNP, Leat, TEF, TUJ, na wadau wa nje kama Article 19 ya Uingereza na Commonwealth Human Rights Initiatives (CHRI) ya India, imekuwa ikipigania kutambuliwa rasmi Kikatiba kwa Uhuru wa Haki ya Kupata Habari pamoja na Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Hali hii inatokana na ukweli kwamba, Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, haitaji wala kuvitambua moja kwa moja vyombo vya habari na wanahabari, pamoja na kutambua uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.

Vuguvugu hilo ndilo lililotoa shinikizo kwa Serikali kuandaa Muswada wa Uhuru wa Kupata Habari wa mwaka 2006 ambao uliainisha haki ya kupata habari, huduma za vyombo vya habari, faragha, ulinzi kwa watoto na kashfa, ingawa serikali hiyo hiyo iliweka vifungu kadhaa vinavyominya usajili wa vyombo vya habari, jambo ambalo limeendelea kuzua mgongano mkubwa na wadau wa habari. 

No comments: