Julius Magodi, Dodoma
BUNGE limeandaa kanuni za maadili ili
kuwadhibiti wabunge ambao wanatumia mianya ya kanuni zilizopo kufanya
makosa mbalimbali ikiwamo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Habari
zilizopatikana mjini Dodoma na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Idara ya
Shughuli za Bunge, John Joel zinaeleza kuwa hatua hiyo ya Bunge
inatokana na kuongezeka kwa wabunge kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali
wanayoyafanya wakiwa nje na ndani ya Bunge.
Joel alisema masharti hayo mpaka sasa yapo katika hatua ya kuchapwa na kwamba muda siyo mrefu maadili hayo ya kanuni yatatoka.
“Tupo katika hatua ya kuichapa code of conduct (Kanuni za maadili) hiyo na kwamba muda si mrefu itatoka na kuanza kutumika.”
Alisema
wamegundua kuwa baadhi ya wabunge wanatumia kanuni za Bunge zilizopo
kuzikwepa na kufanya mambo yasiyofaa ambayo yanashusha hadhi ya Bunge,
hivyo masharti hayo mapya yatawabana zaidi.
Kauli hiyo ya Joel
inakuja siku mbili baada ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa
Azzan Zungu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa
madai ya kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazazi
uliomalizika jana mjini hapa.
Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala,
alikamatwa na makada wengine wa chama hicho saa 4:30 usiku katika kituo
cha mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa
mkutano huo wa wazazi.
Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa
Dodoma, Eunice Mmari juzi alikaririwa akisema vijana wake walimtia
nguvuni Zungu katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake
wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa wazazi.
Mbunge mwingine ambaye ana kesi mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa ni Omar Badwel wa Bahi.
Badwel anatuhumiwa kuomba rushwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga mkoani Pwani, Zipora Liana.
Hatima ya Zungu, Badwel
Kuhusu
kukamatwa kwa Zungu, Mkurugenzi huyo wa Idara ya Shughuli za Bunge,
alisema kuwa Bunge halitamchukulia hatua yoyote na badala yake
linaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake.
Joel alisema suala la
Zungu bado ni tuhuma hivyo, ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge na
Mbunge wa Ilala hadi hapo kama itathibitika kuwa ametenda kosa
mahakamani.
Alisema suala lake ni sawa na la Mbunge Badwel ambaye
ana kesi mahakamani ya kutuhumiwa kujihusisha na rushwa, lakini bado
anaendelea kuwa mbunge.
Hatua hii ya Bunge pia inakuja wakati bado
ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge
kujihusisha na rushwa wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu, ikisubiriwa
kusomwa bungeni.
Agosti 2, mwaka huu Spika Makinda aliunda kamati
ndogo ya kuchunguza tuhuma za rushwa zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya
wabunge ambao walidaiwa kwamba walihongwa ili kuikwamisha Bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini.
Kuundwa kwa kamati hiyo, kulitanguliwa
na tukio la kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Julai 28,
mwaka huu pia kutokana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, kujihusisha
na rushwa na wengine kutumia nafasi zao kujinufaisha kwa kufanya
biashara na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo lipo chini ya
kamati hiyo.
Mabilioni ya Uswisi
Katika hatua nyingine, Serikali
imeanza kufanya uchunguzi wa kina ili kujua ukweli na kuwachukulia hatua
watu wote walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi.
Waziri Mkuu alisema bungeni jana kuwa, mara baada ya uchunguzi huo kukamilika Serikali itatoa taarifa kuhusu uchunguzi huo.
Pinda
alikuwa akijibu swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu
jana asubuhi.
“Jambo hili kwa uzito wake, tumeanza kulifanyia
uchunguzi ili kujua ukweli wake na hatua stahiki za kuchukua, tukimaliza
tutatoa kauli kama ilivyo kawaida yetu, “ alisema.
Mbowe katika
swali lake alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kuhusu taarifa za
kuwapo kwa mabilioni ya fedha katika akaunti za benki mbalimbali nchini
Uswisi ambazo zimewekwa na baadhi ya vigogo serikalini na viongozi
wastaafu.
Katika Bunge la Bajeti lililopita, Kambi ya Upinzani
ililiibua suala hilo wakati wa hotuba yao ya Bajeti wakieleza kuwa kuna
jumla ya Sh360 bilioni zilizofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki
mbalimbali nchini Uswisi.
Taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi
inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo
hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo nchini.
Jumanne wiki hii,
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alipokuwa akichangia azimio la kuridhia
marekebisho ya pili ya Mkataba wa Ushirikiano kati ya Jumuiya ya Nchi za
Ulaya na Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP), alisema Serikali
iutumie ushirikiano huo kurejeshwa mabilioni yaliyofichwa nchini Uswisi.
Naye
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara
Rombo, mkoani Kilimanjaro Oktoba 26 mwaka huu, alimlipua Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk
Edward Hoseah, akidai kuwa bosi huyo ameandika barua Uswisi, akieleza
kwamba Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika
benki za nchini hiyo.
Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha akisema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment