Tuesday, November 13, 2012

TIC:Wawekezaji 52 wapewa ardhi Tanzania

WAWEKEZAJI 52 pekee ndiyo waliopewa hati ya kumiliki ardhi kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Raymond Mbilinyi alibainisha hayo alipozungumza katika kikao cha kikundi kazi kilichojadili umuhimu wa kuwa na Benki ya Ardhi nchini jijini Dar es Salaam.

Mbiolinyi alisema kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya ardhi kwa shughuli za uwekezaji na mpaka sasa idadi hiyo ya wawekezaji ndiyo waliopata umiliki ardhi akiwataka Watanzania kuondokana na dhana kuwa ardhi yao inaporwa.

Katika kikao hicho kilichoandaliwa na TIC na kushirikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Tamisemi, suala la uharakishaji wa utoaji hati ya umiliki wa ardhi kwa wawekezaji pia lilijadiliwa.

“Watanzania waelewe na kuondokana na dhana potofu iliyojengeka kuwa ardhi yao inaporwa na wageni. Kwa mujibu wa sheria TIC ndiyo yenye dhamana ya kutoa ardhi kwa wawekezaji wa nje,” alisema Mbilinyi akieleza kuwa iwapo kuna mwekezaji amepata ardhi kwa njia ya udanganyifu bila kibali cha TIC taarifa iwasilishwe ili achukuliwe hatua za kisheria hata akiwa Mtanzania.

Alifafanua kuwa Tanzania ina ardhi kubwa kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli za maendeleo na kwamba ardhi iliyotolewa ni kidogo ikilinganishwa na iliyopo kwa shughuli za uwekezaji.

Kaimu Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kwa mazingira ya sasa, mwekezaji huchukua muda mrefu kupata ardhi ya uwekezaji na hati za umiliki jambo alilosema linapaswa kuangaliwa kwa umakini kuondoa ucheleweshaji na ukiritimba.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Ardhi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mjumbe wa kikundi kazi, Calister Lekule alisema wizara yake inaunga mkono mchakato wa kurahisisha upatakanaji wa ardhi na vibali vya umiliki ardhi na itashiriki kikamilifu kupima na kuyatambua maeneo kwa ajili ya uwekezaji.

Alisema kuwa kampuni za uwekezaji zinazokuja kuwekeza nchini zinahitaji ardhi hivyo ni lazima Tanzania nayo iweke mazingira kulingana na hali ilivyo ili kwenda na wakati.

Awali, akiwasilisha mada kwenye mkutano huo,Meneja Kitengo cha Ardhi wa TIC, Desderius Narwango alisema taarifa zinaonyesha kuwa mwaka 2010 hekta 1,996,067 .003 ziliainishwa kufaa kwa uwekezaji, kati ya hizo hekta 709,379 .644 zilikuwa zimepimwa na huku 1,286,687.359 zikiwa hazijapimwa na kulipiwa fidia.

No comments: