Tuesday, November 20, 2012

Jaji Warioba: Wananchi zaidi ya 900,000 watoa maoni Katiba Mpya

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema hakuna chombo chochote kilichowahi kuwafikia watu wengi nchini zaidi ya tume yake, ambayo hadi awamu ya tatu ya kazi yake ya kukusanya maoni inamalizika, imekwishafikiwa na wananchi zaidi ya 900,000 kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya katika mikoa 24 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kwa lengo la kutoa tathmini baada ya tume yake kumaliza awamu ya tatu na kuendelea na awamu ya nne, ambayo ni ya mwisho ya kazi yake ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.

Alisema katika awamu zote hizo, tume imefanya jitihada kubwa kuhakikisha inakutana na kila kundi katika jamii, wakiwamo makundi tisa ya watu wenye ulemavu, ambao alisema wote wamepata maoni yao.
“Hakuna chombo kilichowahi kupata watu wengi kama tume hii. (Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba) Aniambie ni chombo gani katika nchi hii kilichowahi kuwafikia watu wengi? Anataka tume ifanye kazi kulingana na mawazo yake na siyo kwa kufuata sheria,” alisema Jaji Warioba.
Alisema awamu ya tatu ya kazi ya tume yake ilifanyika kuanzia Oktoba 8 hadi Novemba 6, mwaka huu katika mikoa ya Rukwa, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Mtwara, Kilimanjaro, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.

Jaji Warioba alisema awamu ya kwanza ilifanyika kati ya Julai 2-30, mwaka huu na kwamba, ilihusisha mikoa ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Alisema katika awamu ya pili, iliyofanyika kuanzia Agosti 27 hadi Septemba 28, mwaka huu, tume ilitembelea mikoa ya Kigoma, Lindi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Katavi na Ruvuma.
Jaji Warioba alisema katika awamu ya tatu iliyomalizika Novemba 6, tume ilifanya mikutano 522 katika mikoa yote tisa ingawa ilipanga kufanya mikutano 496.

Alisema hali hiyo ilitokana na mahitaji mapya katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo na kuifanya tume kuitisha mikutano ya ziada ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi.
Jaji Warioba alisema katika awamu ya pili, tume ilifanya mikutano 449 wakati awamu ya kwanza ilifanya mikutano 388.

Alisema katika awamu ya tatu, wananchi 392,385 walihudhuria mikutano na kwamba, wananchi 21,512 walitoa maoni yao kwa kuzungumza katika mikutano hiyo na wananchi 84,939 walitoa maoni ya kwa maandishi.

Aidha, alisema katika awamu hiyo, wananchi 1,639 walitoa maoni yao kwa kuzungumza na pia kwa maandishi katika mikutano hiyo.

Kutokana na hali hiyo, alisema tume inaridhika na kazi inavyoendelea na namna wananchi wanavyojitokeza kutoa maoni kwa njia mbalimbali zilizotolewa na tume.

Alisema tume yake haitaingilia misimamo ya vyama vya siasa vinavyominya uhuru wa wafuasi wao kutoa maoni na kusema kazi ya tume ni kuchukua maoni na kwamba, yeyote anayetoa maoni popote aliko watayachukua.  
CHANZO: NIPASHE

No comments: