Tuesday, November 27, 2012

Hotuba Ya Mwenyekiti Wa WILDAF Kwenye Uzinduzi Wa Kupinga Ukatili Wa Kijinsia...!

Ukumbi wa Diamond Jubilee, TAREHE 26/11/2012

Ndugu Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Sheria na  Katiba,Mheshimiwa, Angelah Kairuki,

Mheshimiwa  Balozi wa Ireland, Fionnula Gilsenan

Waheshimiwa wawakilishi wa Balozi mbalimbali,

Mheshimiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema,

Wawakilishi wa Mashirika wahisani,

Ndugu Viongozi Vyama na Serikali,

Waandishi wa habari,

Wageni waalikwa,

Mabibi na mabwana,

Itifaki imezingatiwa.

Kwa niaba ya wanachama wa WiLDAF Tanzania na kwa niaba ya Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) na  Kikosi kazi cha kuandaa maandalizi ya siku 16 za Kupiga Vita ukatili wa kijinsia, ningependa kuchukua fursa hii kuwakaribisha rasmi kwenye uzinduzi huu wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Tunatoa shukrani za pekee kwako mgeni rasmi kwa kuitikia wito wetu wa kuja kujumuika nasi katika uzinduzi huu na hasa ukizingatia kwamba una majukumu mengi, na nyeti yanayohusu taifa letu.

Kweli unatuthibitishia kwamba wewe ni mwanaharakati mwenzetu.

Ndugu mgeni Rasmi,

Aidha ningependa kuchukua nafasi hii kipekee kabisa kulishukuru kwa namna ya pekee Shirika la Msaada la Ireland (Irish Aid), Shirika la Msaada la Marekani  USAID, UN –Women  na CONCERN kwa kutupa uwezo wa kiuchumi ili kuweza kuadhimisha siku hii.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru washiriki wote kwa kujumuika nasi katika uzinduzi wa Siku hizi 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu 2012.

Ndugu mgeni rasmi,

Naomba uniruhusu nikufahamishe kwa ufupi tu kuhusu  chimbuko la kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Kampeni hii ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1991 na Taasisi ya Kimataifa  ya Wanawake  katika  Uongozi, huko nchini Marekani kwa nia ya kuamsha ari ya kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake kwa kuzingatia haja  ya kuleta usawa wa kijinsia.

Ndugu mgeni rasmi,
Kampeni hii ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia  inaanza rasmi tarehe 25 Novemba ambayo ilichaguliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1999 kuwa ni SIKU YA KIMATAIFA YA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE . Hivyo basi, Umoja wa Mataifa unashauri serikali, mashirika ya Kimataifa na asasi zisizo za kiserikali kufanya shughuli zinazolenga kufahamisha jamii juu ya ukatili dhidi ya wanawake.Wanawake duniani kote wamekuwa wakikumbwa na ukatili ikiwemo kubakwa, vipigo, ukatili majumbani, ukeketaji na aina mbalimbali za ukatili. Tarehe hii ni ya kihistoria kwani ni kumbukumbu ya mauaji ya kinyama waliofanyiwa kina dada wa Mirabelle nchini Dominika mwaka 1960.  Wanawake hawa  waliuawa kikatili kwa kuwa walikuwa  wanapinga utawala wa kidikteta wa Rais wa nchi ya Dominika (1930-1961) Rafael Truijilo na kutetea haki  katika jamii yao.  Wakina dada hawa walifanyiwa vitendo vingi vya kudhalilishwa utu wao na mwishowe Raisi Rafael Truijilo aliamua wauawe.  Aidha Kampeni hii inahitimishwa tarehe 10 Desemba  ambayo  ni siku ya Kimataifa ya  TAMKO LA HAKI ZA BINADAMU ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya  wanawake na  haki za binadamu na  kutia msisitizo kwamba ukatili kama huu ni uvunjwaji wa haki za binadamu.

Ndugu mgeni rasmi,
Kati ya tarehe 25 Novemba na Desemba 10 kuna matukio mbali mbali ya kimataifa kama ifuatavyo:-

-  Tarehe 29 Novemba ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Wanawake.

-  Desemba 1 ni siku ya UKIMWI duniani.

-  Desemba 6 ni siku ya kukumbuka mauaji ya kikatili ya wanawake wahandisi mjini Montreal, Canada.

Ndugu mgeni rasmi,
Kwa kipindi cha tangu mwaka 1991 inakadiriwa kiasi cha nchi 156 duniani na mashirika zaidi ya 2,000 yanashiriki katika kampeni hii ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa kufanya yafuatayo:-

-    Kuhamasisha jamii juu ya ukatili wa kijinsia na masuala yanayohusu haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

-   Kuimarisha mshikamano wa kupambana na vitendo vyote vya ukatili  dhidi ya wanawake.

-   Kuanzisha ushirikiano wa dhati kati ya wanaharakati wa ndani na nje ya nchi ili kutokomeza ukatili wa kijinsia.

-  Kuandaa jukwaa lenye kuleta fursa ya kubadilishana  mawazo, uzoefu na kuweka mikakati thabiti kwa pamoja ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

-  Kuonesha mshikamano wa wanawake duniani kote na kuwa na sauti ya pamoja  katika kupinga ukatili dhidi ya wanawake.

-    Kuunganisha nguvu za wanawake pamoja ili iwe nyenzo thabiti kuishawishi serikali kutekeleza ahadi walizoweka ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Ndugu mgeni rasmi,
Nchini Tanzania katika  Siku hizi 16, mashirika, taasisi na idara mbali mbali chini ya  mwamvuli wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), Kikosi Kazi cha kuratibu maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yakiratibiwa na  WiLDAF yanaungana na wapenda haki wote duniani kuwakumbuka  wanawake na wasichana wote walioathirika na vitendo vya ukatili kama vile kupigwa, kubaguliwa kijinsia, kukeketwa, kuuawa, wajane kunyang’anywa mali, kunyimwa haki ya kumiliki ardhi na kadhalika.  Ni dhahiri kwamba, ukatili wa kijinsia ni dhana  pana inayogusa jinsi zote lakini kwa kiasi kikubwa wahanga  wakubwa wa ukatili huu ni wanawake.
Ndugu mgeni rasmi, kampeni ya mwaka huu imekuwa na muitikio mkubwa na msisimko wa aina yake kwani wadau wengi wamejitokeza katika kampeni hii. Mathalani, Jeshi la Polisi limekuwa na ushiriki mkubwa na wa kipekee. Kwa kutilia mkazo na kutekeleza nguzo ya Polisi Jamii, Jeshi la Polisi linaungana nasi kwa kufanya shughuli mbali mbali za kuhamasisha amani na usalama katika makazi yetu na maeneo ya barabarani. Kwa kutumia fursa ya rasilimali watu ambayo jeshi la Polisi linayo, watatoa elimu ya athari na madhara ya ukatili, watahamasisha jamii kukemea vitendo vyote viovu vinavyosababisha ukatili kwani ukatili wa kijinsia ni kosa la jinai na pia unachochea uvunjwaji wa amani katika nyumba zetu na Taifa kwa ujumla. Napenda kutumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua hizi. Pia nampongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspecta Generali Said Mwema kwa juhudi kubwa anazofanya. Inatupa faraja kubwa sisi wanaharakati kuona Jeshi la Polisi limevalia njuga kampeni hii. Hii inatoa ishara nzuri kwamba kwa kushirikiana nasi basi tutaweza kuutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
Ndugu Mgeni Rasmi, pamoja na Jeshi la Polisi, Mashirika mengine yanayoshirikiana nasi na yana shughuli mbalimbali katika kipindi hiki cha kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake ni kama ifuatavyo,
  • World Vision watakuwa na kampeni kuhusu afya ya mtoto sasa itakayofanyika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro, Kempiski
  • Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA) watakuwa na mjadala kuhusu ukatili wa kijinsia tarehe 29 katika ukumbi wa Diamond Jubillee
  • Equality for Growth (EFG) watakuwa na uzinduzi wa kupiga vita ukatili wa kijinsia kwa kutembelea masoko mbalimbali ya wilaya ya Ilala, tarehe 5/12/2012
  • Engender Health/Champion Project watakuwa na uzinduzi wa kupiga vita ukatili wa kijinsia tarehe 6/12/2012 kwa kutembelea vijiji 20 vya mkoa wa Iringa
  • Children Dignity Forum (CDF) watatoa msaada wa kisheria mkoa wa Pwani. Pia wataendesha shughuli mbalimbali kupiga vita ukeketaji tarehe 8/12/2012 katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.
  • Pamoja na mashirika mengine Action Aid, Concern, CSOs coalition na YWCA watakuwa na shughuli mbalimbali za kupinga vita ukatili wa kijinsia.
  • Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wataadhimisha siku ya Tamko Rasmi la Haki za Binadamu na kuhitimisha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia.
Ndugu Mgeni Rasmi, uwepo wetu leo hapa katika kuadhimisha uzinduzi wa kampeni ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia unaambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, maonesho ya programu mbalimbali za asasi zinazolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia, mada mbalimbali zinazohusiana na ukatili wa kijinsia. Aidha uzinduzi huu una shughuli mbili za kipekee. Kwanza uzinduzi wa Fomu ya Polisi namba 3 (PF 3), Fomu hii mpya ya Polisi imefanyiwa maboresho na kuongezewa vipengele muhimu pamoja na mambo mengine vinavyohusu ukatili wa kingono. Ni imani yetu kubwa kuwa Fomu hii mpya ya Polisi ni nyenzo muhimu na itasaidia katika ushahidi na hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.
Ndugu Mgeni rasmi

 Shughuli nyingine ya kipekee ni uzinduzi wa msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia (CARAVAN). Msafara huu umebeba Mabalozi kutoka makundi mbalimbali ya wanaume, wanawake, vijana na walemavu. Mabalozi hawa watatoa ujumbe na kuhamasisha jamii za kitanzania kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Aidha, wataunganisha nguvu za pamoja kwa kuhamasisha jamii zetu kuwa kila mtu mwanaume awe au mwanamke ana wajibu wa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Msafara huu utatembea katika kanda tatu (3) ambazo ni kanda ya Kaskazini, Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda ya Kati, Mkoa wa Singida, na Kanda ya Ziwa, Mkoa wa Mara-Tarime, ambapo takwimu zinaonesha kuna kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya wanawake hususan ukeketaji. Ni matarajio yetu makubwa kuwa msafara huu utakuwa ni chachu kubwa katika jamii zetu kuanza kuzungumza na kutoa taarifa ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake. Aidha utaamsha ari kwa jamii zetu kuweza kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia

Ndugu mgeni rasmi 
Kampeni hii ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia itafanyika kikanda. Kanda hizo ni Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, na Shinyanga) chini ya usimamizi wa Shirika la KIVULINI na ABC Foundation, Kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga) chini ya usimamizi wa NAFGEM,  Kanda ya Kati (Dodoma, na Singida) chini ya usimamizi wa  AFNET, Kanda ya Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa na Lindi) itaadhimisha  shughuli hii chini ya kituo cha wasaidizi wa kisheria Iringa na Kanda ya  Kaskazini (Tabora na Kigoma) chini ya Jeshi la Polisi wakishirikiana na WiLDAF. Aidha kampeni hii mikoani inazinduliwa rasmi leo  26/11/2012.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Tunafahamu kuwa serikali ya Tanzania imefanya juhudi mbalimbali za kuzuia na kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.  Juhudi hizi ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati  wa kitaifa wa  kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia wa mwaka 2001,  kutunga sheria na sera  mbalimbali zinazolenga kuleta usawa kwa mfano:-

-          Dira ya Maendeleo  ya mwaka 2025.

-          Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 inayolenga kuwaendeleza wanawake kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa.

-        Sheria ya Kanuni Za Adhabu Sura Na. 16 hususan vipengele vya makosa ya kujamiiana

-          Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5, zote za mwaka 1999 kama zilivyorekebishwa mwaka 2002 zinazolenga kutoa haki sawa ya umiliki wa ardhi kati ya wanaume na wanawake.

-         Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia unaolenga kuwa na jamii isiyokuwa na aina yoyote ya ukatili ifikapo 2015.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Pamoja na jitihada zote hizi nzuri zinazofanywa na serikali, vitendo vya  ukatili wa kijinsia bado vinakithiri katika jamii zetu. Hivyo basi, tuna sababu za makusudi kabisa kuishirikisha jamii katika kuzuia ukatili wa Kijinsia kwani kwa kiasi kikubwa jamii imekuwa ikichochea au ikikubali uwepo wa ukatili wa kijinsia.

Mathalani katika utafiti uliofanywa na WiLDAF mwaka 2012 katika magazeti, unaoonesha kwamba taarifa 6,001 za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa kwenye magazeti ikilinganishwa na taarifa 3,542 za mwaka 2011.

Ndugu Mgeni Rasmi, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake sio tu kwamba  vinawadhoofisha kiafya, bali pia vinaathiri  uwezo wao wa kushiriki na kuchangia katika kuleta maendeleo kiuchumi ndani ya familia zao na nchi kwa ujumla.
Aidha, jitihada za serikali katika kupunguza umaskini chini ya mkakati wa kuzuia na kutokomeza umaskini (MKUKUTA) na malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDG) hasa lengo kuu la tatu hayataweza kufikiwa iwapo hakutakuwa na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha kuwa ukatili dhidi ya wanawake unatokomezwa.

Ndugu mgeni rasmi mwaka huu kauli mbiu yetu ni “FUNGUKA! KEMEA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE. SOTE TUWAJIBIKE” Kauli mbiu hii ina maana kwamba sote tunatakiwa kuamka katika masuala ya kuzuia Ukatili. Ni vema kutafakari kwa kina  jinsi ambavyo ukatili wa kijinsia, hususan ukatili dhidi ya wanawake unavyoathiri maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla. Sote tunafahamu jinsi jamii inavyofumbia macho vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia vinapotokea, jamii kwa kiasi kikubwa haitoi ushirikiano kwa vyombo husika kuhakikisha tatizo hili linapotea.. Hatuwezi kuwa na Taifa imara bila kutokomeza ukatili wa kijinsia.  Hivyo basi, kauli mbiu inaweka msisitizo kuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzinduka na kukemea ukatili dhidi ya wanawake ili kudumisha taifa imara.
Ndugu Mgeni Rasmi,  katika utekelezaji wa kuzuia na kupambana na Ukatili  wa Kijinsia nchini Tanzania, WiLDAF pamoja na mashirika/taasisi  zingine zinazotetea haki za binadamu zinakabiliana na changamoto zifuatazo:-
  1. Mgongano wa sheria mbalimbali na sheria kandamizi ambazo bado zinatumika, Aidha ukosefu wa sheria mahususi dhidi ya ukatili majumbani.
  2. Ushiriki mdogo wa jamii katika kujihusisha katika utetezi na kukabiliana na matatizo ya ukatili wa kijinsia, hususan ukatili dhidi ya wanawake.
  3. Ukosefu wa fedha za kutosha za kutoa mafunzo na kujenga uelewa wa umma katika masuala ya ukatili wa kijinsia.
  4. Mtazamo hasi ndani ya jamii unaopelekea kuhalalisha vitendo vya ukatili  wa kijinsia uliojijenga kwenye mfumo dume.
  5. Ushiriki duni/hafifu wa Wizara mbali mbali na hivyo kutokutoa kipaumbele suala la ukatili wa kijinsia katika wizara zao.
  6. Ukosefu wa takwimu za kutosha kuhusu masuala yanayohusiana na ukatili wa kijinsia
  7. Ukosefu wa huduma bora za afya katika vituo vya afya kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia mathalani sehemu za kuwahifadhi waathirika hao.
  8. Uelewa mdogo na kutotilia maanani suala zima la ukatili wa kijinsia kwa watoa huduma katika jamii.
  9. Uchelewashaji wa kesi za ukatili wa kijinsia hivyo kupelekea waathirika kukata tama na kutokuwa na ushirikiano katika kutoa ushahidi na upatikanaji wa haki.

Ndugu mgeni rasmi
Pamoja na changamoto hizo bado tunayo nafasi ya kurekebisha  hali  iliyopo. Hivyo basi sisi wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia  tunaiomba wizara yako kuangalia mambo yafuatayo:-.

-          Kuchukua  hatua za makusudi za kutunga  sera zinazolenga kuleta usawa,  kubadilisha/kurekebisha Sheria ya Ndoa na kutunga sheria mpya ya mirathi pamoja na Sheria  dhidi ya  ukatili nyumbani.

-          Tunaomba Wizara yako iunde kitengo maalumu katika mahakama cha kusimamia kesi za ukatili wa kijinsia, ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa haraka, kwani haki inayocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa.

-          Wizara izidi kuweka msukumo ili serikali itenge fedha na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuelimisha wanajamii juu ya haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria na sera zilizopo. Pia kutoa fedha kwa mashirika yanayotetea haki za binadamu hususan haki za wanawake.

-          Serikali kuanzisha sehemu maalumu kwa ajili ya hudma za waathirika wa ukatili wa kijinsia (one stop centre)

-          Serikali ijenge hifadhi zitakazohudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia

Mwisho kabisa tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako na Mungu akubariki.


                              Mh. Naomi A.M. Kaihula

                                           MWENYEKITI

No comments: