Joachim Mushi, Thehabari.com
BAADHI ya walimu wa shule za msingi wilaya za
Korogwe na Moshi wamelalamikia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala
kwa shule za msingi pamoja na idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa
madarasa ya chini, kuwa yamekuwa yakiwachanganya wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni walisema mabadiliko ya
mara kwa mara kwa mitaala yanayofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi bila maandalizi yamekuwa chanzo cha vikwazo cha kufanya vizuri
kwa sekta hiyo.
Akizungumza hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu Mkuu
Msaidizi wa Shule ya Msingi Gerezani, mjini Moshi, Khadija Mtui alisema
mabadiliko ya mitaala ya mara kwa mara yanawachanganya wanafunzi pamoja
na walimu hivyo kuwa kikwazo.
Alishauri kuwepo na maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na
kuwashirikisha walimu ambao ni wadau wakubwa wa sekta ya elimu kabla ya
mabadiliko ya mitaala hiyo. Alisema pamoja na hali hiyo mabadiliko ya
vitabu vya masomo bila utaratibu mahususi ni tatizo pia katika mafanikio
ya sekta hiyo kitaaluma.
“Mabadiliko ya mitaala na mchanganyiko wa vitabu bila utaratibu mahususi
ni tatizo, kwa sasa hivi kila shule ina kitabu chake katika somo
fulani…hata hivyo licha ya mabadiliko ya mara kwa mara hakuna
maandalizi, mimi tangu nimalize chuo 1979 sijaenda semina yoyote wala
mafunzo kujiandaa na mabadiliko ya mitaala hii. Hili linachangia pia,”
alisema mwalimu Mtui.
Akifafanua zaidi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Muungano,
ya wilayani Moshi, Ashati Elihaki alisema mbali na mchanganyiko juu ya
suala la vitabu vya masomo mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya
masomo kubaki kama ‘kiini macho’ jambo ambalo ni tatizo kwa walimu.
“…angalia kwa mfano somo kama la Tehama linaloanza kufundishwa darasa
la tatu hadi la saba somo hili lipo kinadharia zaidi, hakuna walimu
ambao wameandaliwa kufundisha somo hili lakini linatakiwa kufundishwa
eti kwa kutumia mwongozo wa mwalimu kimsingi hii si sawa,” alisema
Elihaki.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe,
Theodolph Karigita alisema tofauti na ilivyokuwa hapo awali mitaala ya
sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo ambalo linawachanganya walimu na
hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya vizuri.
“…Mitaala imevurugwa sana, kunamchanganyiko wa masomo nadhani
unakumbuka kuna kipindi baadhi ya masomo yaliunganishwa kama Jiografia,
Historia na Uraia wakaita maarifa ya jamii…kipindi hiki wanafunzi
walifanya vibaya sana hivyo ikabadilishwa sasa watoto wanafanya vizuri
tofauti na awali,” alisema Karigita.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani,
Youze Mbwambo alisema idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa darasa la
kwanza hadi la tatu ni chanzo kingine cha wanafunzi hao kufanya vibaya
kwani wamekuwa wakibebeshwa mzigo pasipo sababu za msingi.
Akizungumzia hoja hizo zilizotolewa na baadhi ya walimu, Ofisa Elimu
Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema mabadiliko
yanayofanywa na wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na
changamoto kadhaa maeneo tofauti.
No comments:
Post a Comment