Watu 73 wamefikishwa mahakamani kwa
kosa la kuwashambulia, kuwazuia polisi kufanya kazi yao, kuvamia maeneo
ya watu na makosa mengine kufuatia operesheni ya kuwaondoa wananchi
waliovamia maeneo yanayomilikiwa na wengine iliyoendeshwa na manispaa ya
Kinondoni, huko Nakasangwe, Kata ya Wazo wilayani Kinondoni.
Aidha watu wengine 50 wanashikiliwa na polisi kufuatia operesheni hiyo,
kwa ajili ya mahojiano zaidi wakituhumiwa kutokuwa na uraia wa Tanzania.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, aliiambia NIPASHE jana
iliyotaka kufahamu maendeleo ya operesheni hiyo, ambayo mwishoni mwa
wiki ililikumba pia eneo la Benaco lililoko katika kata ya Wazo jijini
Dar es Salaam.
“Kwa hawa 50, kuna timu maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kuwafanyia
mahojiano zaidi kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa huenda si
Watanzania, bali raia kutoka nchi jirani, na kwa hali hiyo, timu
inayofanya kazi hii ya kuwahoji, inawajumuisha pia maofisa uhamiaji
ambao ndiyo haswa wenye eneo lao,” alisema.
Kamanda Kenyela alisema kimsingi watu hao walikamatwa katika eneo
walilolibatiza kwa jina la ‘Mungiki no go area’ lililoko kitongoji cha
Kaza Raha huko Nakasangwe ambacho kilikuwa hakifikiwi na mtumishi yeyote
wa serikali, mfanya biashara au mwananchi asiyefahamika nao kwa kuwa
walikuwa wakiwakamata, kuwapiga na wengine kuwabaka.
Alisema kuwa kitendo cha watu hao kuwarushia mishale, mashoka na mapanga
polisi kama ilivyotokea siku ya kwanza ya operesheni si tabia ya
Watanzania na kwamba, miogoni mwa watu waliofanya kitendo hicho ni hao
53 wanaoshikiliwa.
Aliwaasa wananchi wote waliovamia maeneo katika Manispaa ya Kinondoni
kuondoka kwa amani kwa kuwa, polisi wapo kwa ajili ya kusimamia
utekelezaji wa sheria.
No comments:
Post a Comment