Na Joachim Mushi, Thehabari.com
MSINGI mbovu na dhaifu wa elimu kwa madarasa ya
awali umebainika kuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi
mkoani Kilimanjaro na Tanga kumaliza elimu hiyo huku hawajui kusoma na
kuandika.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni katika
Wilaya ya Moshi (Manispaa) umebaini idadi kubwa ya shule za msingi
awali hazikuwa na madarasa ya awali kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi
kujiunga na darasa la kwanza, jambo ambalo liliilazimu shule kupokea
wanafunzi wa darasa la kwanza toka nje ya shule wengine wakiwa
hawajaandaliwa kikamilifu.
Taarifa zimebaini vituo vingi vya shule za awali ambavyo baadhi ya
shule za msingi zilikuwa zikitegemea kupokea watoto wa darasa la kwanza
vilikuwa havina walimu wenye taaluma ya kuwaandaa watoto katika vituo
hivyo kwa ajili ya kujiunga na darasa la kwanza.
Uchunguzi uliofanyika katika baadhi ya shule za katikati ya Mji wa
Moshi (Manispaa) na pembezoni umebaini shule nyingi hivi sasa
zimeanzisha madarasa ya awali ikiwa ni shinikizo la Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi la miaka ya hivi karibuni.
Shule ya Msingi Magereza ni miongoni mwa shule zinazofanya vibaya
katika Manispaa ya Moshi, shule hii inashika nafasi ya 45 kiwilaya kati
ya shule 46 za manispaa nzima. Kimkoa inashika nafasi ya 595 kati ya
shule 638 japo ipo mjini ukilinganisha na zile za vijijini.
Akizungumza mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Magereza alisema
awali haikuwa na darasa la awali bali ilikuwa ikipokea wanafunzi wa
darasa la kwanza kutoka nje ya shule. Alisema ilianzisha darasa la awali
rasmi linaloendeshwa na shule hiyo Machi 1, 2012.
Taarifa zaidi zimebaini licha ya madarasa mengi ya shule za awali
kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao huwa mzigo kwa mwalimu mmoja
anayefundisha, mengi ya madarasa hayo yana umri kati ya miaka mitatu
kushuka chini jambo ambalo linaonesha mafanikio yake hayajaanza
kujitokeza.
Hata hivyo hali hiyo imejitokeza katika Wilaya ya Korogwe mkoani
Tanga, kwani kati ya shule nne za msingi Silabu, Lwengera, Kitopeni na
Boma ambazo mwandishi amezitembelea ni moja tu (Boma) ndio yenye darasa
maalumu la wanafunzi wa awali. Uchunguzi umebaini kuwepo na shule zenye
wanafunzi wa awali lakini hakuna vyumba vya kufundishia wala waalimu
wenye sifa ya kufundisha kitengo hicho muhimu.
Akizungumza Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius
Mkwizu alisema kwa eneo lao bado suala la vyumba vya madarasa ni tatizo
hivyo idara hiyo inajitahidi kulishughulikia suala hilo kwa
kushirikiana na wazazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Manispaa, Leocadia Akaro alisema
idara yao inajitahidi kuhimiza ujenzi wa madarasa ya awali na mafanikio
ni makubwa kwani idadi kubwa ya shule za msingi zinamadarasa ya awali
tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa ushirikiano na taasisi ya HakiElimu
No comments:
Post a Comment