Chama Cha Walimu Tanzania (CWT),
kimesema bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyosomwa
bungeni na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, haina jipya kwa
sababu imeshindwa kuzungumzia madai ya walimu yaliyowafanya wagome.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekia Oluoch,
alisema bajeti hiyo imewashangaza sana walimu kwa kushindwa kuzungumzia
madai yao ambayo waliahidiwa na serikali kuwa yangetekelezwa tangu Juni,
mwaka huu.
“Tunamshangaa sana Dk. Kawambwa, kwa bajeti yake ambayo haina jipya.
Imeshindwa kuzungumzia madai ya walimu ambayo yaliwafanya wagome na yeye
mwenyewe ndiye aliyesababisha na kushindwa kulieleza Bunge,” alisema.
Alisema bajeti yake pia haijazungumzia juu ya walimu 900 kutoka vyuo vya ukufunzi ambao walitakiwa kupanda daraja.
Bajeti hiyo pia juzi ilipingwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Suzan
Lyimo, kwa takwimu za serikali kuonyesha kiwango cha elimu kimepanda
wakati wanafunzi 5,200 hawajui kusoma na kuandika walichaguliwa kujiunga
kidato cha kwanza.
Lyimo alisema serikali ilitumia nguvu na vitisho kushughulikia madai ya
walimu kama njia ya kuwanyamazisha badala ya kuwasikiliza na kufikia
mwafaka.
No comments:
Post a Comment