WATETEZI wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa
habari nchini, leo wameipa serikali siku saba kufungulia gazeti la
MwanaHALISI, vinginevyo wataitisha maandamano ya kupinga hatua ya
serikali kufungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana, kuminya uhuru wa
habari, haki za binadamu na utesaji wa wanaharakati.
Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI
ni MISA, Legal and Human Rights Centre, Tanzania Human Rights Defenders
Coalition, Human Rights National Association of Educators For World
Peace and Citizen Rights Watch.
Tamko la asasi hizo ni kama ifuatavyo hapa chini:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 22 Agosti 2012
YAH: KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI
KWA mara nyingine tena, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe
wetu huu kwa watawala. Ujumbe wenyewe unahusu kufungiwa kwa gazeti la
kila wiki la MwanaHALISI na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter
Pinda aliyoitoa bungeni, Alhamisi tarehe 16 Agosti 2012. Kama mnakumbuka
vema, wakati akijibu swali bungeni siku hiyo, Waziri Mkuu Pinda
alisema, “Serikali imechukua wajibu wake kulifungia gazeti hilo, na
kwamba kama wahusika hawakuridhika na hatua iliyochukuliwa na serikali
wana haki ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu.”
Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatukuridhika na majibu ya Waziri
Mkuu kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI. Majibu ya Waziri mkuu Pinda
yamelenga kuahirisha tatizo, siyo kutatua. Kwanza, Waziri Mkuu anatetea
uamuzi huo uliofanywa na sheria katili na kandamizi ya magazeti. Sheria
inayonyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa
kuwasiliana. Pili, Mheshimiwa Pinda anatumia sheria hiyo kutaka
kuliangamiza gazeti hili ambalo limesifiwa kwenye ripoti mbalimbali za
ndani na nje ya nchi ikiwamo ile iliyotolewa majuzi na Baraza la Habari
Tanzania (MCT) inayochambua Mwenendo wa vyombo vya Habari nchini kwa
mwaka 2011 inayosema katika ukurasa wa tisa:
“Pamoja na kusakamwa na serikali, MwanaHALISI limesimamia uandishi wake wa kuikosoa serikali.”
Serikali imelituhumu gazeti hili kwa kuchapisha habari ambazo inasema
“zinakiuka” vifungu 32(1) (a), (c) – (d); 32(1)(c) na 36(1) vya Sheria
ya Magazeti Na. 3 ya 1976. Habari hiyo inahusu kutekwa, kuteswa kinyama
na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande kwa kiongozi wa madaktari
nchini, Dk. Steven Ulimboka. Hii ndiyo habari ambayo serikali inaita ya
“uchochezi.” Yaani badala ya serikali inayojigamba ina mkono mrefu wa
kumfikia yeyote kuutumia mkono huo kutafuta watuhumiwa waliotajwa na
gazeti kuwa walifanikisha kutekwa kwa Dk. Ulimboka, imeamua kutumia
mabavu kulifungia MwanaHALISI huku wakiacha maisha ya Dk. Ulimboka na
wanaharakati wengine njia panda.
Serikali imechukua hatua hiyo, huku wakijua kuwa Ibara ya 18 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyorekebishwa na
Sheria ya Mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(2005), ilipanua haki ya kutoa, kutafuta, kupokea, na kusambaza habari.
Mabadiliko hayo yaliondoa kivizo cha “kwa mujibu wa sheria” Kila mtu-
anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya
kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao
uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano
yake.
Aidha, mabadiliko hayo yanatoa haki kwa kila raia ya kupewa taarifa
wakati wote kuhusu matukio muhimu mbalimbali kwa maisha na shughuli za
wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii. Hivyo basi haki na
uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari haina vipingamizi ambavyo
serikali inadai kuwamo katika Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
Vilevile, kuwekwa kwa Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa
Mwanadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya nchi yetu kulibadilisha
sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu. Vifungu vyote
tulivyovitaja hapo juu viliguswa moja kwa moja na Vipengele vya Haki za
Msingi na Wajibu wa Mwanadamu. Ibara ya 14 ya Katiba inalinda haki ya
kuishi na inaitaka jamii kutoa hifadhi ya maisha kwa kila mtu. Kana
kwamba hiyo haitoshi, Ibara ya 26(1) na (2) zinataka kila mtu na
serikali kutii Katiba ya nchi na vilevile kuchukua hatua za kuheshimiwa
haki na sheria za nchi.
Waziri mkuu anayajua haya vizuri. Anafahamu kuwa sheria iliyotumiwa
kufungia gazeti, ni sheria katili na imepitwa na wakati. Kuitumia sheria
hii kunaendeleza dhana ya kuwa serikali hii inatumia udhaifu wa Katiba
na baadhi ya sheria kukandamiza Haki za Binadamu na Uhuru wa Habari!
Mambo haya hayakubaliki.
Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:
1. Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja
na bila masharti, gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi.
Tunaitaka serikali ndani ya siku saba (7) kutekeleza hilo kwa kuangalia
maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya
viongozi wenye maslahi fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.
Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo, na kwamba asasi za
kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka wahusika waende
kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu zifuatazo:
Kwanza, sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa
Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa
wahusika kusikilizwa. Pili, Waziri Mkuu Pinda pamoja na sheria hiyo
kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya MwanaHALISI.
Hivyo kutoelekeza kwake tunakuchukulia kama njia ya kukwepa wajibu
wake.
Tatu, hatukubaliani na kauli ya Waziri Mkuu na wengine wanaoitaka
MwanaHALISI waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali
yenyewe haikutumia njia ya mahakama kufungia gazeti. Serikali inataka
kuitumia mahakama ili kuchelewesha MwanaHALISI kupata haki yake. Nyote
mnajua jinsi mahakama zetu zinavyokabiliwa na gonjwa kubwa la
ucheleweshaji wa kesi.
2. Serikali, baadala ya kushughulika na watetezi wa haki na
wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa
na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka. Ushahidi uliobainishwa na gazeti
hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama
serikali au watendaji wake waliotajwa (na waliohusishwa) wana mashaka
wangetumia ushahidi na taarifa zile kutafuta haki zao: kwanini wasiende
mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?
3. Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru
wa habari. Matendo aliyofanyiwa Ulimboka, habari zilizobainishwa na
MwanaHALISI juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha
mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru na haki.
Ikumbukwe pia kuwa, Kesi Na. 34/2009 iliyofunguliwa tangu 2009
kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuwafungia
MwanaHALISI haijasikilizwa mpaka sasa. Hii inaenda sambamba na serikali
kufumbia macho mahitaji ya sheria ya uhuru wa habari na kudharau
mapendekezo ya muswada wa habari tangu 2007 bila kupeleka Bungeni.
Kwa hoja hizo, sisi watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na
wadau wakuu wa habari nchini, tunaendelea kusisitiza kuwa serikali
itimize wajibu wake kwa kulifungulia mara moja gazeti hili na kufanyia
kazi yaliyobainishwa. Kama ikishindwa kufanya hivyo, tutaitisha
maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hili, kuminya
uhuru wa habari, haki za binadamu na uteswaji wa wanaharakati na
watetezi wa haki na kwamba tukifika hapo tunawaomba waandishi wa habari
mtuunge mkono kwa yafuatayo.
i. Msichapishe habari yoyote inayomhusu Waziri wa Habari,
Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, na pia Mkurugenzi wa Maelezo.
Tunawasihi wahariri wasiwatume waandishi katika Ukumbi wa Habari Maelezo
kwa ajili ya kuchukua habari kama ilivyo kawaida na badala yake
Watanzania wote wahakikishiwe kupata habari kwa njia nyingine mbadala.
ii. Tunawasihi wadau wote wanaoweza kutuunga mkono mara
tutakapohitaji msaada wao ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maandamano
na kupata mawakili ambao watasaidia katika uendeshaji wa shauri letu
mahakamani.
iii. Tunawasihi wanaharakati wote wasichoke wala wasirudi nyuma
katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi
wake.
Marcossy Albanie
Mwenyekiti wa Kamati
Asasi ambazo zimetoa tamko la kutaka serikali ifungulie MwanaHALISI
ni MISA, Legal and Human Centre, Tanzania Human Rights Defenders
Coalition, Human Rights National Association of Educators For World
Peace and Citizen Rights Watch.
No comments:
Post a Comment