Mkazi
wa Ndembezi mjini Shinyanga amepigwa na mumewe hadi kuzirai na
kukimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutoa ushirikiano kwa
karani wa Sensa ya Watu na Makazi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa huo, Evarist Mangala, alisema jana kuwa mwanamke
huyo, Esther Zablon (40) alipigwa juzi saa mbili asubuhi baada ya
mumewe, Ismail Yahya kupata taarifa kuwa karani wa sensa alifika
nyumbani kwao na mkewe kukubali kuhesabiwa na kutoa takwimu za familia
yao.
Akisimulia,
Kamanda Mangala alisema karani huyo alipokwenda nyumbani hapo, mume
hakuwapo na kama mkuu wa kaya, Esther akazungumza na kutoa taarifa.
Alisema
baada ya mume kurudi nyumbani na kugundua kuwa mkewe alikubali
kuhesabiwa, alimshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha mke huyo
kupoteza fahamu.
Kutokana na kipigo hicho, kwa mujibu wa Kamanda Mangala, Esther alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi na matibabu.
"Wakati
mwanamke huyo akichukua fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kituoni kabla
ya kufikishwa hospitalini, huku akilia kuwa sababu ya kipigo ni yeye
kukubali kuhesabiwa, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa dini ya
mumewe (Uislamu)," alisema Kamanda Mangala.
Hata hivyo, Kamanda alisema Esther alitoroka wodini kwa kuhofia mumewe kukamatwa na hatimaye kufungwa.
Kamanda Mangala alisema Polisi wanaendelea kumtafuta Yahya na akipatikana atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
No comments:
Post a Comment