WAZIRI
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka wanaotangaza
kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi kuwataja
mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala ya
kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni
Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa,
wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni
pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.
Utafiti
uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial
Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini
limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini
Awamu hii ya Nne imetia fora.
Utafiti
huo uliofanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika
utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola
za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Akizungumza
katika mahojiano maalumu, kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania
isiendelee kufilisiwa na watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na
watu hao kuogopa na kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale
inapokuwa wahusika ni vigogo wa Serikali.
Alisema
vigogo hao ni sababu ya watu kupata kigugumizi katika hili akihoji :
“Kwa nini linapokuwa ni suala linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo
hawatajwi?”
Sitta
ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti,
alisema haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje
ya nchi huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha
magumu.
“Watajwe!
Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni
kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba
huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa
nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Alisema
njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja na vyombo husika
kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni msumeno, haipaswi
kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa katika nchi.Sitta
ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali la kwa nini
hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”
Alisema
amesikia na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja
wahusika iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu
yoyote ya mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.
“Haiwezekani
kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa
Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”
Alisema
hata kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango
hicho hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”
Tuhuma
hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani
kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja
ikiwa Serikali haitafanya hivyo.
Chanzo http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment