Na Joachim Mushi, Thehabari.com
TAASISI ya HakiElimu leo jijini Dar es Salaam
imewakutanisha baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu ambapo waliishuhudia
bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu ikiwasilishwa ‘live’ mjini
bungeni mjini Dodoma kabla ya kutoa maoni yao.
Wadau hao wa elimu kwa pamoja waliishuhudia kupitia king’amuzi bajeti
ya Wizara ta Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwasilishwa ‘live’ wakiwa
kwenye mkutano kisha baadaye kutoa maoni yao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Elimu, Dk.
Shukuru Kawambwa kuwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2012/13,
Mhadhiri wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo alisema ameshangaa bajeti hiyo
kutouona mgomo wa walimu wa juzi pamoja na migomo ya wanafunzi wa vyuo
vikuu kama ni tatizo kwa elimu na kuiingiza kama changamoto.
“Binafsi kati ya vitu ambavyo vimenishangaza ni bajeti hiyo kutotaja
mgomo wa walimu katika bajeti iliyopita kuwa ni miongoni mwa changamoto
za wizara hiyo…na hata migomo ya vyuo vikuu,” alisema Dk. Mkumbo
alipokuwa akijadili katika mkutano huo.
Alisema wizara imetaja kufanya vizuri katika elimu upande wa msingi na
sekondari kwa kidato, lakini imekwepa kutoa mafanikio kwa kidato cha
tano na sita eneo ambalo limefanya vibaya kwa matokeo ya hivi karibuni.
Alikosoa kiwango cha uwiano kati ya wanafunzi na walimu kilichotatolewa
kwa sasa (1:46) kwani idadi kubwa ya walimu wapo shule za mjini huku
hali mbaya ikiwa vijijini.
Aidha aliongeza kuwa wizara pia imeshindwa kuona migomo ya wanafunzi
wa vyuo vikuu ya mara kwa mara ni changamoto hivyo kushindwa kueleza
katika bajeti yake. “…karibu asilimia 80 ya migomo ya wanafunzi wa vyuo
vikuu imesababishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, lakini hili
halikutajwa katika bajeti ya waziri,” alisema msomi huyo.
Kwa upande wake Mhadhiri Adolf Mkenda kutoka Idara ya Uchumi ya UDSM
akizungumza katika mkutano huo alisema bajeti iliyowasilishwa ni ya
kawaida hivyo ni vigumu kumaliza changamoto lukuki za elimu
zinazoikabili wizara hiyo.
Alisema bajeti imejivunia ongezeko la idadi ya vyuo vikuu lakini
imeshindwa kuonesha ubora wa vyuo hivyo jambo ambalo ni hatari endapo
litaachwa, bila udhibiti. “…Twaweza kuwa na vyuo vingi lakini suala la
ubora ni tatizo lingine. Pia uandikishaji wa idadi kubwa ya wanafunzi
unatakiwa kulinganishwa na waliokusudiwa kuandikishwa…maana twaweza
jivunia kiwango kinapanda kumbe tunadanganywa na ongezeko la idadi ya
watu,” alisema msomi huyo.
Akizungumza kwenye mjadala Meneja wa Kitengo cha Habari wa HakiElimu,
Nyanda Shuli alisema Serikali haiwezi kufanikisha elimu bora bila
kuaandaa walimu bora katika utoaji wa elimu husika. “Huwezi kutegemea
elimu bora pasipo na walimu bora, binafsi sijaona mkakati wowote
mahususi wa kuboresha elimu,” alisema Shuli.
Ameishauri wizara ya elimu kujiandaa vizuri kimipango kabla ya
kutekeleza mpango wa kuwa na shule ya kidato cha tano na sita kwa kila
tarafa ili kuepuka madudu yaliojitokeza katika mpango wa uanzishwaji
shule za kata.
Hata hivyo kabla ya kuishuhudia bajeti hiyo ikiwasilishwa Dk. Mkumbo
na Mkenda wakiongozwa na mhadhiri mwenzao kutoka Shule Kuu ya Uandishi
wa Habari na Mawasiliano, Ayoub Rioba waliwasilisha mada zilizokuwa
zikiiangalia elimu ya Tanzania na majaliwa yake.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu tayari imewasilisha makadirio ya
mapato na matumizi kwa mwaka 2012/13 ambapo jumla ya sh. 724,471,937,000
ili zitumike kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake. Huku sh.
18,561,689,000 zikiwa ni fedha za ndani na sh. 74,019,627,000 kutoka kwa
washirika wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment