CHAMA cha waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC)
wamelaani vurugu zilizotokea juzi mkoani Iringa na kusababisha kifo cha
mwandishi wa habari wa kituo cha utangazaji cha Chanel Ten Daud
Mwangosi. Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa chama hicho Habel Chidawali
alipokuwa akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani hapa.
Chidawali amesema kuwa kamwe chama hicho hakikubaliani na nguvu kubwa
iliyotumiwa na jeshi la polisi kwa ajili ya kumwaga damu ya mwandishi
huyo ambaye hakuwa na hatia na kamwe Jeshi la Polisi haliwezi kujitetea
kwa kudai kifo cha mwandishi huyo ni bahati mbaya.
Amesema kuwa jeshi la polisi limekuwa liki onesha wazi wazi kuwa
linatumia nguvu, ubabe na matumizi mabovu ya silaha za moto ambayo
hayajaweza kusaidia siku zote na badala yake kinachoachwa ni maumivu na
vilio kwa wananchi. Katibu huyo amesema kama Jeshi la Polisi linatuliza
ghasia hakuna siku hata moja haijatokea wakamuua kiongozi yoyote wa
siasa ambao ni vinara wa mikutano mbalimbali.
Kwa upande wao wananchi mbalimbali mkoani hapa wamekemea nguvu kubwa
inayotumika na Polisi katika vurugu mbalimbali zinazotokea. Wamesema
tabia ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu na silaha za moto
ambazo zinasababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
Catheline Muhinte, amesema kuwa tukio lililofanywa na Jeshi la Polisi
la kumuua mwandishi wa habari linaonyesha dhairi kuwa kwa sasa jeshi
hilo linafanya kazi kwa kukiuka maadili ya malengo yao.
Amesema katika mwonekano wa picha ambazo zinaonekana katika vyombo
mbalimbali vya habari inaonyesha dhairi kuwa polisi walihusika moja kwa
moja na kifo cha mwandishi huyo.
No comments:
Post a Comment