Monday, September 20, 2010

Kampeni Pemba kuwa za kitanda kwa kitanda

MGOMBEA mwenza wa urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk. Mohammed Gharib Bilal amewaomba wananchi wa Pemba wampigie kampeni ya kitanda kwa kitanda, nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa mgombea wa kiti cha urais Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein ili aingie Ikulu kwani uwezo wa kuongoza anao.

Naye Dk. Shein amewaambia wananchi hao kuwa safari yake ya kwenda Ikulu imeanza, huku akidai wakimchagua atahakikisha anaweka sawa yale ambayo yamekuwa yakiwatatiza.

Kauli hizo zilitolewa jana kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale mjini hapa, ambapo chama hicho kilikuwa kinazindua kampeni za mgombea huyo wa urais upande wa kisiwa cha Pemba baada ya juzi kufanya hivyo Viwanja vya Kibandamaiti upande wa kisiwa cha Unguja.

Huku akishangiliwa na wananchi waliofurika kwenye viwanja hivyo kutoka maeneo mbalimbali ya Pemba, Dk. Shein alisema safari yake ya kwenda Ikulu ilianza jana kwenye viwanja hivyo upande wa Pemba kama ilivyokuwa kwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume mwaka 2000 alipoanzia safari yake ya kwenda Ikulu kwenye viwanja hivyo.

"Safari yangu ya Ikulu imeanza leo Gombani ya Kale, sasa ni pakubandika pa kubandua, moja mbili, wahedi thinina (Kiarabu) na Kiingereza one..two mpaka Ikulu.

Nasema mambo ya Pemba sasa yatakuwa bomba," alisema Dk. Shein na kufafanua kuwa mwaka 2000 Rais Karume alifika kwenye eneo hilo na kuwaomba wananchi wampe kazi ya urais awatumikie naye pia amefanya hivyo.

Aliwaomba wakazi wa Pemba wamuombee dua ashinde na pia aweze kuwatumikia Wazanzibari kwani uwezo huo anao na ataendeleza yote yaliyofanywa na Rais Karume.

Alisema huu si wakati wa Wazanzibari kufanya makosa, kwani nchi imefikia hatua nzuri kimaendeleo, hivyo wasirudi nyuma badala yake wampe yeye nafasi afanye mambo mazuri zaidi na kama wapo wanaohitaji kunong'onezwa ili wampigie kura lifanyike, wanaohitaji kupigiwa hodi vyumbani nao pia wafanyiwe hivyo.

Alieleza kuwa kwa jinsi alivyofanya kazi na Rais Jakaya Kikwete na anavyomfahamu Dk. Bilal wakishinda itakuwa ni mteremko tu, ni kama maji kushuka kwenye mlima.

Naye Rais Karume akizungumza kabla ya kumkaribisha Dk. Shein alisema CCM imemteua kuwania nafasi hiyo kwa vile inamuamini kwamba anaweza kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kwa ufanisi.

Aliwaeleza wananchi kuwa Dk. Shein ni mtu mzuri, muungwana, shupavu, hodari na ana uwezo wa kufanya kazi, jambo ambalo ndilo kubwa na kuwakumbusha wananchi wa Pemba jinsi mwaka 2000 Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi alivyosimama kwenye viwanja hivyo kumpigia debe yeye akisema ni mtu makini na mwenye uwezo.

"Mzee Mwinyi alisema maneno mazito na namnukuu alisema, namfahamu vizuri Karume ni mtu mzuri, anaweza kusuluhisha nyoyo za Wazanzibari.

Nawauliza nyie hapa leo, tumefanya hilo au hatukufanya?" Alihoji na kuitikiwa na kauli ya ndiyo, hivyo kuongeza kuwa naye ana imani na Dk. Shein.

Alisema mambo mbalimbali yaliyofanywa na serikali yake anaamini Dk. Shein ndiye anayeweza kuyaendeleza, hivyo ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake na kufanya kampeni ili Dk. Shein amiminiwe kura.

No comments: