TAASISI ya utafiti ya Synovate imesema haijafanya utafiti wowote kuhusu wagombea wa nafasi za urais unaoonesha kuwa mgombea wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa anakubalika zaidi na wananchi.
Baadhi ya vyombo vya habari (si gazeti hili) jana vilimnukuu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema kuwa Chadema ina matokeo ya kura za maoni za Synovate yanayoonesha kuwa Dk. Slaa anakubalika kwa asilimia 45 akifuatiwa na Rais Kikwete mwenye asilimia 41.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mbowe anadaiwa kusema kuwa takwimu hizo hazikutolewa Septemba 14 walipotoa taarifa za namna vyombo vya habari vinavyoripoti kampeni za uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Meneja wa Synovate, Aggrey Oriwo alisema taarifa hizo ni za kughushi, hazina ukweli wowote na zinaupotosha umma kwa kuwa hawajawahi kufanya utafiti wowote unaohusu kukubalika kwa wagombea wa urais.
“Kauli ya Mbowe imetukera sana na magazeti yalioandika pia yametukera, hakuna ukweli wowote na sisi ni kampuni huru, hatuwezi kubania taarifa yoyote, hatuegemei upande wowote, tayari tumewasiliana na vyombo husika vya habari na tumeandika barua kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kulalamikia suala hilo,” alisema Oriwo na kumtaka Mbowe kuweka bayana ushahidi kuhusu takwimu hizo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya jana, Mbowe alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Sanya Juu, mkoani Kilimanjaro.
Alidai sababu za kutotolewa utafiti huo zinatokana na CCM kuikataza taasisi hiyo kufanya hivyo. Meneja huyo hakuwa tayari kuweka bayana kama watafanya utafiti kuhusu wagombea hao kwa madai kuwa wakati huu wa kampeni utafiti kama huo una hatari.
Alisema kazi zao zina mipaka na utafiti kama huo ukifanyika, watautoa kwa jamii kupitia vyombo vya habari kama ambavyo wamekuwa wakifanya.
No comments:
Post a Comment