Wednesday, September 15, 2010

Slaa awasha moto upya

- Ataka majibu ya Kagoda, Tangold
- Asisitiza hatanyamaza hadi kieleweke
Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, ameibua mzimu wa kampuni ya Kagoda inayodaiwa `kukwapua’ Sh. bilioni 40 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Dk. Slaa amemtaka mgombea wa nafasi kupitia CCM, Rais Kikwete, kutafuta suluhu dhidi ya kashfa ya Kagoda, ili awatendee haki Watanzania.

Alikuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo mjini hapa.

Dk. Slaa alisema kikao kilichofanikisha ‘kuchotwa’ fedha hizo katika benki ya CRDB, kilifanyika chini ya uenyekiti wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mbunge wa Igunga aliyemaliza muda wake, Rostam Aziz.

Alidai kuwa Chadema imeshatoa ushahidi wa kina kuhusiana na wizi wa Epa, lakini katika hali ya kushangaza, Rais Kikwete amekuwa na kigugumizi kwa kampuni ya Kagoda.

“Kukaa kwako kimya kunamaanisha kuwa fedha hizo ndizo zilikuingiza madarakani...tunataka kujua, Kagoda ni kampuni ya nani, mbona unapata kigugumizi,” alihoji.

Dk. Slaa alisema hawezi kufunga mdomo bila asizungumzie kashfa hiyo mpaka hatua zitakapochukuliwa dhidi ya Kagoda na kampuni ya Tangold.

“Tangold ambayo tulielezwa ni ya serikali ilisajiliwa Mauritius na mmoja wa wanahisa ni Andrew Chenge, lakini tunaambiwa mwenye hisa anaweza kuzimilikisha kwa mke, mtoto au mpwa...hivi mpwa wa serikalini nani,” alihoji.

Dk. Slaa alifafanua kuwa Sh. bilioni 155 zilizopelekwa katika mgodi wa Buhemba kupitia Tangold, zingeweza kuboresha sekta ya elimu nchini.

Sitta ashutumiwa ‘kulindana’ Pia Dk. Slaa alimshukia mgombea ubunge wa jimbo la Urambo Mashariki (CCM), Samuel Sitta, na kumwita mnafiki katika masuala yanayohusu maslahi ya umma.

Alidai kuwa Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge lilimaliza muda wake, alitumia cheo hicho vibaya kuizima kashfa ya Richmond bungeni.

Pia alidai kuwa Sitta alimkataza (Dk. Slaa) kuzungumzia mishahara minono ya wabunge.

“Niliposimama bungeni kuhoji ni sehemu gani Tanzania petroli inauzwa Sh 2,500, Sitta alinitaka nikae kimya na akasema taarifa yangu isiingie kwenye hansard ...wabunge wanaelea kwenye anasa, Sitta anataka posho iongezwe,” alisema.

Alidai kumpigia simu Sitta, lakini hakupokea hivyo akalazimika kumwandikia ujumbe mfupi kumkumbusha namna elimu ilivyokuwa bure enzi za Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumzia mabango ya CCM, alidai kuwa na ushahidi kwamba yametengenezwa kwa fedha ya Ikulu ambazo ni kiasi cha Dola za Marekani milioni 1.5.

Makamba alipuliwa

Dk. Slaa alidai kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ndiye aliyesaini mkataba huo na kampuni ya Mediapix ya Canada, chini ya uratibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu.

Jimbo la Musoma Mjini ni moja kati ya majimbo yenye ushindani mkubwa hasa kwa kuzingatia kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Vincent Kiboko Nyerere ni mwanafamilia ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Tutaboresha gongo iwe halali

Wakati huo huo, Dk. Slaa, ameahidi kuruhusu matumizi ya teknolojia itakayoboresha pombe ya gongo, ili itambuliwe kisheria.

Dk. Slaa alisema hatua ya kuiweka gongo katika matumizi halali ya binadamu, itakuwa na manufaa kwa taifa na kusaidia kuwapunguzia askari polisi kazi ya kufukuzana na watumiaji wa kinywaji hicho ambacho hivi sasa ni haramu.

Alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika katika uwanja wa Getrude Mongela uliopo mjini Nansio, Ukerewe.

Licha ya gongo kuwa bidhaa haramu kwa mujibu wa sheria, watu wengi katika maeneo mbalimbali nchini, hasa wa kipato cha chini wanaitumia kama kiburudisho.

Pia, Dk. Slaa alisema pombe hiyo ikiboreshwa itawaongezea kipato Watanzania wanaoitegemea kama biashara kuu na kuliingizia taifa mapato yatakayotokana na kodi.

Alisema zipo pombe kali kama konyagi ambayo kiwanda chake kilianzishwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Nyerere, ambayo hivi sasa bei yake ni kubwa ikilinganishwa na bia.

Dk. Slaa alisema ikiwa atashinda katika uchaguzi huo, serikali yake itatafuta na kugawa bure kwa watengenezaji wa pombe hiyo, mashine za kisasa na kusimamaia viwango vyake ili watengeneze kinywaji kinachokubalika.

Akizungumzia mauaji ya watu 14 yaliyatokea usiku wa Januri 17, mwaka huu katika kisiwa cha Izinga, Dk. Slaa aliwapa pole wafiwa na kusema kwa kiasi kikubwa, tukio hilo lilichangiwa na uzembe wa serikali ya CCM.

Alisema serikali inawajibika kuwalinda raia wake, jambo ambalo si hisani bali limeanishwa miongoni mwa wajibu wa serikali.

Dk. Slaa alisema suala la ulinzi wa raia lina maslahi kwa umma, hivyo akawataka wananchi kuondokana na tofauti za itikadi zao ili wamuunge mkono na kumchagua kuwa Rais wa Tanzania.

Habari hii imeandikwa na Restuta James, Musoma na Jovither Kaijage, Ukerewe.


SOURCE: NIPASHE

No comments: