Thursday, September 2, 2010

UNIFEM KUWAPATIA WAGOMBEA WANAWAKE MBINU ZA KUSHINDA UCHAGUZI


NA MWANDISHI MAALUM-NEW YORK

Wakati kampeni za kuwania nafasi za urais, ubunge na udiwani zikiwa zinaendelea kushika kasi nchini Tanzania. Mfuko wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Maendeleo ya Wanawake (UNIFEM), umetangaza kuendesha mafunzo ya uwezeshaji kwa wanawake waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Octoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa UNIFEM kwaajili ya maendeleo ya Kikanda Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika, Ni Sha. Inaeleza kuwa, mafunzo hayo yatakayoendeshwa katika kanda saba za uchaguzi yatafanyika mwezi huu wa septemba,lengo likiwa ni kuwajengea uwezo na kuwapa wanawake mbinu na mikakati ya kushinda uchaguzi.

“ Mafunzo haya yanalenga kuwawezesha wanawake wanaowania nafasi za uongozi na uwakilishi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Tanzania mwezi octoba, kuboresha mbinu za uzungumzaji katika mikutano ya hadhara, namna bora ya kushirikiana na kuwasiliana na vyombo vya habari, uratibu wa kampeni zao, namna ya kujieleza, uhamasishaji wa jamii na mbinu za ushawishi” anafafanua Ni Sha katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Wagombea hao wanawake pia watajifunza kuhusu nafasi ya mwanamke katika siasa za Tanzania, masuala mbalimbali ya kisiasa yanayohusiana na uchaguzi wa mwaka huu, majumu ya Bunge , Baraza la Wawakilishi , Halmashauri, Sheria na Taratibu mbalimbali zinazohusu uchaguzi.

Taarifa hiyo ya UNIFEM, inabainisha pia kwamba, pamoja na Katiba ya Tanzania kutenga asilimia 30 ya viti vya ubunge kwaajili ya wanawake, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ni wanaweke 17 waliojitokeza kuwania nafasi za ubunge kati ya wagombea 232.

UNIFEM imekwisha kuwapatia mafunzo wakufunzi 30 watakao endesha mafunzo hayo, ambayo mbinu zake za ufundishaji tayari zimekwisha kufanyiwa majaribio na kukubalika. Mafunzo ya wakufunzi hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam kati ya tarehe 12 na 14 mwezi wa uliopita (wa Nane).

Katika hatua nyingine, UNIFEM kwa kushirikiana na UNESCO katika mwezi huu wa tisa pia itatoa mafunzo kwa waratibu wa vituo vya radio za jamii katika miji ya Arusha, Unguja na Pemba kwa lengo la kutoa ufahamu na uelewa kuhusu taarifa za wagombea wanawake katika maneo yao. Waandishi pia watafundishwa mbinu za kuandika habari zenye kutoa nafasi sawa na haki kwa wagombea wanawake.

No comments: