Monday, September 27, 2010

CUF, Chadema vyafanya mdahalo wa wagombea vijana

MDAHALO wa wagombea wa ubunge vijana wa vyama vya CUF na Chadema umefanyika na kufana bila kuwepo kwa wagombea ubunge wa CCM.

Mdahalo huo ulioongozwa na mwanaharakati Jenerali Ulimwengu, ulitoa nafasi kwa wagombea hao kuonesha uwezo wao wa kutetea ilani za vyama vyao tofauti na ilivyokuwa ikidaiwa na CCM ambayo imekataza wagombea wake wasigombee.

Katika mdahalo huo, wagombea hao walipewa nafasi ya kuelezea sera za vyama vyao na ahadi zilizopo katika ilani za vyama vyao kuhusu changamoto kadhaa za kijamii na kiuchumi kabla ya wananchi kupewa fursa ya kuwauliza maswali.

CCM katika maelezo yake ya kukataa kushiriki katika midahalo yote ya wagombea, moja ya sababu za kufikia uamuzi huo ilisema kuwa ni kutokana midahalo hiyo na kutawaliwa na malumbano na matusi kuliko fursa ya wagombea kutangaza sera.

Lakini jana katika mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV, kila chama kilipewa muda sawa na kingine kujibu hoja kwa kueleza ahadi zilizoko katika ilani zao za uchaguzi kwa wananchi na kuonesha uwezo wa vijana hao kujibu hoja.

Katika hoja ya Muungano, mgombea wa Chadema katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye aliongoza upande wa chama hicho, alisema chama hicho kitaimarisha Muungano ili utumike kama mfano katika kujenga muungano wa Afrika Mashariki na hatimaye Muungano wa Afrika.

Alisema lengo la kuimarisha Muungano, ni kutimiza ndoto za waasisi wa dhana ya Muungano wa Afrika, Kwame Nkrumah na Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa upande wa CUF, mgombea wa ubunge wa Ubungo kupitia chama hicho, Julius Mtatiro ambaye alionekana kuongoza upande wa chama hicho, alisema wamedhamiria kuanzisha serikali tatu ili kuondoa malalamiko ya kero za Muungano.

Kuhusu serikali zao zitakavyotekeleza sera za kutoa elimu na afya bure, Mtatiro aliwataka Watanzania wawape kura wagombea wa CUF, ili waoneshe namna ya kubana matumizi na kupeleka fedha zinazopotea katika kutoa huduma hizo.

Alisema katika Serikali ya CUF, ikibidi mawaziri watapanda teksi ili kubana matumizi.

Kwa upande wa Chadema, Zitto alisema kama Nyerere aliweza kutoa elimu na afya bure kwa kutumia fedha za katani na kahawa, chama hicho kitatoa huduma hizo bure kwa kutumia fedha za dhahabu, gesi na Tanzanite.

Umahiri wa kujibu hoja wa wagombea hao, ambao CUF walikuwepo wawakilishi watatu na Chadema wawakilishi watano, ulimfanya msimamizi wa mdahalo huo, Ulimwengu kuhitimisha kwa kauli kuwa vijana wanaweza.

“Mdahalo huu umeonesha vijana wanaweza kutetea taifa lao...wao ni taifa la leo, kesho na kesho kutwa wakati wazee ni taifa la leo, jana na juzi,” alisema.

No comments: