Monday, September 6, 2010

Takukuru yageuka `bubu` kwa vigogo waliohusishwa rushwa kura za maoni

Utata umetanda kuhusu hatima ya watuhumiwa wa kashfa za rushwa katika mchakato wa kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Idadi kubwa ya watu wakiwemo viongozi wa serikali katika ngazi tofauti waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuwania ubunge, walikamatwa ama kuhojiwa kutokana na rushwa.

Wagombea wa ubunge na udiwani kupitia chama hizo walishiriki kampeni zilizofanyika kati ya Julai 22 hadi 31, mwaka huu na kura zikapigwa Agosti Mosi, mwaka huu.

Wakati wa mchakato huo, makamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wa mikoa mbalimbali, walitoa taarifa za kukamatwa ama kuhojiwa kwa wana-CCM waliotuhumiwa kwa rushwa.

Miongoni mwa waliotajwa ni aliyewahi kushika nafasi ya uwaziri kwa nyakati tofauti, Joseph Mungai na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), David Mwakalebela, ambao walifikishwa mahakamani.

Pia alikuwepo Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (Uvccm) mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo, aliyefikishwa mahakamani kutokana na tuhuma za rushwa.

Mkoani Kilimanjaro, mkanganyiko umeibuka katika ofisi ya Takukuru, baada ya Kamanda wa taasisi hiyo aliyehamishiwa hapa hivi karibuni, kutoa taarifa tofauti na zile za awali kuhusu wagombea waliotuhumiwa kwa rushwa.

Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Laurance Swema, ambaye amehamishiwa mkoani alisema hana taarifa rasmi kuhusu kukamatwa kwa wagombea watatu wa nafasi za ubunge na udiwani, makada wa CCM na viongozi wengine wakati wa kura za maoni.

Alisema suala hilo analisikia na kulisoma kupitia vyombo vya habari, na kwamba hana taarifa za kiofisi.

Kamanda huyo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akiongea na NIPASHE kwa njia ya simu.

NIPASHE ilitaka kujua hatua zilizofikiwa ikiwemo kufikishwa mahakamani, dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa na Takukuru wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Alisema ana muda mfupi tangu ahamishiwe mkoani hapa akitokea Dar es Salaam, na kati ya mambo aliyokabidhiwa ofisini, hajaelezwa juu ya watuhumiwa wa rushwa wakati wa kura za maoni.

“Mimi ndio nimehamishiwa hapa kutokea Dar es Salaam na kwa sasa nipo likizo, nimekuja kuchukua familia yangu...sijasikia jambo hilo ofisini kwangu zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari ambavyo mmeandika nyie,”alisema.

Hivi karibuni, aliyekuwa Kamanda wa Takukuru mkoani hapa na ambaye amehamishiwa mkoani Manyara, Alexanda Budigila, alikaririwa akisema kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa matukio hayo.

Budigila alisema watuhumiwa waliokamatwa ama kuhojiwa watafikishwa mahakamani ikiwa uchunguzi utawezesha kupatikana kwa ushahidi.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wetu, baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria, siku tunayowapeleka mahakamani tutawajulisha wanahabari,”alisema.

Waliokamatwa wakidaiwa kutoa rushwa ni pamoja na aliyeibuka mshindi wa pili kwenye ubunge wa Viti Maalum mkoani hapa, Betty Machangu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Wengine ni Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani hapa, Mariam Kaaya, Katibu wa UWT wilaya ya Moshi, Hadija Ramadhani,mfanyabiashara wa Moshi mjini, Hawa Sultani na dereva wa gari alilokuwa akilitumia mbunge huyo, SwaleheTwalibu.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika nyumba ya kulala wageni ya Safari Resort, ambapo kwa mujibu wa Takukuru, walikuwa wakigawa rushwa ya fedha na vitu kwa wajumbe kwa kila mmoja kuingia ndani.

Tarifa zilidai kuwa mgombea huyo na wafuasi wake walikuwa wakigawa kati ya Sh 50,000 na 100,000, kanga, asali, vipeperushi na kadi za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT mkoa.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya alikanusha madai ya kutoa rushwa na badala yake alisema walikwenda kwenye hoteli hiyo kwa ajili ya kupata chakula.

Machangu alidai kuwa walipokosa mahali pa kukaa, waliamua kuchukua chumba kimoja ili wakae kwa utulivu.

Akasema kuna dalili kwamba maadui zake wa kisiasa walihusika katika kutoa taarifa zilizosababisha kuzingirwa na maofisa wa Takukuru.

Pia Takukuru iliwakamata wagombea udiwani wa kata ya Shirimatunda, Elines Mwacha na watu saba kati ya 30 waliodaiwa kuwa mabalozi, wajumbe wa vijiji na makatibu wa CCM katika kata ya hiyo ambao wanadaiwa walikuwa wakila na kunywa na mgombea huyo.

Takukuru ilimkamata pia mgombea udiwani wa kata ya Majengo, Idd Juma, wakati akiwa na wanachama wa CCM na wenyeviti wa mitaa ya kata hiyo zaidi ya 15, katika baa ya Peters Club iliyopo eneo la Majengo kando kando mwa barabara kuu ya Moshi -Tanga.

Mkoani Arusha, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Ayub Akida, amesema watuhumiwa waliokamatwa ama kuhojiwa kutokana na rushwa wakati wa kura za maoni, bado hawajafikishwa mahakamani.

Akihojiwa hivi karibuni, Akida, akasema uchunguzi bado unaendelea na kwamba utakapokamilika, atatoa maelezo kwa umma.

Waliokamatwa ama kuhojiwa kutokana na tuhuma za rushwa wakati wa kura za maoni mkoani Arusha, ni mbunge aliyemaliza muda wake Felix Mrema pamoja na wanachama 21 wa CCM.

Tukio hilo lilitokea usiku nyumbani kwa mwanachama mmoja eneo la Olamuriaki, kata ya Sombetini mjini hapa baada ya maofisa wa Takukuru kuivamia nyumba hiyo.

Watuhumiwa hao walihojiwa na Takukuru siku moja baadaye, kisha kuachiwa kwa dhamana.

Akizungumzia tukio hilo, Akida akasema walipata taarifa ya kuwepo kwa mkutano wa wanachama hao muda wa usiku na kwamba walikuwa wakiutilia shaka.

Alisema maafisa wake waliizingira nyumba hiyo na kufanikiwa kuwatia mbaroni ingawa wanachama wengine walikimbia.

Mkoani Dodoma, kukamatwa kwa mkazi mmoja wa wilaya ya Kondoa, Ibrahim Mfala akigawa fulana na kofia bure.

Naibu Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Sosteness Kibwengo, alikaririwa wakati wa mchakato akisema kuwa Ibrahim alikamatwa akigawa fulana hizo zilizokuwa na nembo ya CCM.

Aidha, Takukuru waliwakuta watu zaidi ya 40 ndani ya nyumba ya balozi eneo la Msalato lililopo halmashauri ya manispaa ya Dodoma Mjini wakidai kuwa wanamsubiri mgeni kutoka mjini.

Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Eunice Mmari, alikiri kupata taarifa za kuwepo kwa mpango wa mgombea mmoja wa ubunge jimbo la Dodoma Mjini, aliyeandaa Sh. 470,000 kwa ajili ya kuwagawia wanachama 47 wa mtaa wa Nduka uliopo kata ya Chamwino.

Alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno ukitaka aelezee wamefikia wapi kuhusiana na uchunguzi huo, ujumbe ulionyesha kupokelewa lakini haukujibiwa.

Alipoulizwa Afisa Uhusiano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Doreen Kapwani, juu ya uchunguzi wa tuhuma za wagombea wanaodaiwa kutumia rushwa wakati wa kura za maoni za CCM, alisema kwa mujibu wa sheria ya taasisi hiyo, hawaruhusiwi kuzungumzia mwenendo wa uchunguzi unaofanywa na taasisi hiyo kabla ya suala husika kufikishwa mahakamani.

Habari hii imeandikwa na waandishi wetu kutoka Kilimanjaro, Dodoma na Arusha.

CHANZO: NIPASHE

No comments: